24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

DIMPOZ AJIFUNZE KWA RAYVANNY, HARMONIZE

Na RAMADHANI MASENGA

OMMY Dimpoz hana tena maajabu katika muziki. Yuko kimya. Huwezi kumfananisha na yeyote aliyekuwa unafananishwa naye zamani.

Ukisikiliza habari za muziki na matukio yake, husikii jina la Dimpoz. Utasikia fulani kafanya shoo pale, mwingine kafanya shoo kule. Dimpoz kimya. Ila ukienda katika ukurasa wake wa mitandao ya kijamii utafurahi.

 Leo ataweka picha yuko Ibiza kisiwani kule Hispania kesho atapiga picha yuko falme za kiarabu.  Chini ya picha hizo hasemi kama alikuwa ameenda kupiga shoo ama colabo zaidi ataandika maneno ya kuashiria yuko katika starehe.

 Huyo ndiyo Dimpoz wetu wa siku hizi. Kazidisha mapozi katika picha kuliko nyimbo redioni. Dimpoz hana tena majabu tuliyodhani atatuonesha. Amekuwa Vasco Da Gama kuliko mwanamuziki. Ila kwanini Dimpoz siku hizi yuko hivi?

 Wengi wana majibu yao ila ukweli huenda tatizo la Dimpoz linaanzia pale alipokoroshifana na meneja wake, Mubenga. Dimpoz haonekani kuwa katika uongozi unaomfanya aendelee kuwa mwanamuziki mkali. Anaonekana yuko katika uongozi wa kishkaji usiofuata weledi wala kuangalia majaliwa yake kimuziki. Ndiyo maana yupo yupo tu kwa sasa.

 Kama utani jina la Dimpoz linaanza kuonekana la kawaida sana katika vinywa vya wengi. Nani anamzungumzia kama mwanamuziki mkali?

 Harmonize na Rayvanny ni watu wanaonekana kwenda juu ya Dimpoz kwa sasa. Wala haishangazi. Wakati Dimpoz akikesha katika mitandao ya kijamii kutuonesha miji na meneo mbali mbali duniani, wenzake wako bize kutoa hit baada ya hit.

 Watu siyo wajinga, kidogo kidogo wataanza kumwona Dimpoz mzugaji na kuuhifadhi katika vifua vyao muziki wa Rayvanny na Harmonize.

    Kama Dimpoz hatobadilika, nategemea kumwona akiomba kolabo kwa unyenyekevu kwa Aslay ili nyimbo yake iweze kuvuma. Inaonekana  kipindi hiki wakati wenzake wakipiga kazi usiku na mchana yeye amesinzia. Akiacha kuamka kwa hiyari ataamshwa na mshtuko na wa kujiona hata katika kumi bora za wasanii wa aina yake ya muziki hayumo.

   Watu waliokuwa wakimzunguka zamani Dimpoz hawaonekani kuwa naye sasa. Ni kama sasa anazungukwa na watu ambao yeye ndiye kiongozi. Hii ni hatari. Kwa msanii kama yeye, anatakiwa kuwa na watu makini wenye kumwongoza na siyo kukubaliana na kila anachokisema.

    Usingizi kama huu walilala wakina Nuruwelly. Mbali na ukali wao, wakaja kushtuka kuwaona wakina Stev R&B wakiwa juu yao na wao wakihesabiwa kama wasanii wenye bahati mbaya.

 Ommy Dimpoz anatakiwa kujifunza kwa akina Nuruwelly, kila mpenzi wa muziki mtaani anasema Nuruwelly mkali. Ukienda katika shoo, wanajaza wakina Steve R&B na Mataluma. Unashangaa. Ukiwaza kuwa wakina Steve R&B wanapendelewa huku wakina Nuruwelly wanabaniwa utakuwa unajikosea heshima kwa kujidanganya.

    Mbali na uchanga wao wa kipindi kile, wakina Steve walihangaika na matokeo yake wakakata mibuyu wakina Nuruwelly na kujitwaliwa ufalme wa R&B.

    Dimpoz muda si mrefu atakuwa msanii wa kawaida kama hatobadilika. Namwona akifanya shoo katika Bar  na Pub za mtaani. Namuona akianza lawama kuwa anabaniwa  akiona wakina Harmonize wakitamba Afrika na kuchukua tuzo kila uchwao. Endeleaa kulala Dimpoz. Muda bado unao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles