28.7 C
Dar es Salaam
Monday, October 25, 2021

D’JARO ARUNGU ASIMULIA MSOTO, MPETO

Na CHRISTOPHER MSEKENA

YUMO kwenye orodha ya watangazaji wa burudani wanaofanya vizuri kwa sasa kupitia kipindi chake cha Papaso kikiwa na msisimko unaowavuta wasikilizaji wengi wasikilize TBC FM kila siku za wiki saa 1- 4 usiku, huyu ni D’ Jaro Arungu maarufu kama Baba Mzazi.

D’ Jaro Arungu ni mzaliwa wa Rorya mkoani Mara akiwa ni mtoto wa kwanza kwenye familia yao, ni baba wa watoto watatu licha ya kwamba bado hajaoa.

Swaggaz limekutana na mtangazaji huyu na kupiga naye stori mbili tatu kuhusu maisha na mwenendo wa tasnia ya burudani kwa kuwa yeye ni mmoja wa wadau wenye ushawishi wa aina yake.

Swaggaz: Shabiki wa Papaso anataka kufahamu D’ Jaro ni nani, ametokea wapi na historia yako kwa kifupi.

D’Jaro Arungu: Safari yangu ilianzia Times FM nikiwa kama ripota wa habari za michezo kwa kujitolea baadaye nikaenda Kiss FM, Mwanza ila nilikaa kwa wiki mbili tu kwa sababu meneja wa vipindi aliniambia sina kipaji cha utangazaji ambapo hata aliyekuwa meneja wa vipindi wa Times FM aliwahi kunisimamisha licha ya kuwa nilikuwa najitolea.

Sikukata tamaa, nikakutana na Abdallah Mwaipaya wa Radio One, akaniambia niende PRT Radio (TBC FM kwa sasa), kwa kipindi hicho walikuwa na uhaba wa watangazaji, nilisita kwa sababu nilijiona sina vigezo kwa kuwa nilikuwa ndiyo nimemaliza kidato cha nne na kuchaguliwa kidato cha tano Benjamini Mkapa Sekondari ingawa sikumaliza kidato cha sita kwa sababu za kifamilia ambapo baba aliachishwa kazi akarudi kijijini na mama pamoja na wadogo zangu.

Mimi nikabaki Dar kuhangaika na maisha bila kusaidiwa na ndugu hata mmoja zaidi ya marafiki na watu baki.

Swaggaz: Ilikuwaje ulipofika kwenye usahili TBC FM?

D’Jaro Arungu: Usahili ulikuwa na watu wengi sana wenye elimu zao na ilikuwa inafanywa kwa awamu, mkiwa 100 mnachukuliwa watatu, baadaye kwa mtindo huohuo huo tukapatikana watu tisa.

Namkumbuka Jerry Muro, Gabriel Zakaria, Jamila Isdory na wengine na kati ya hao tukapita, mimi, Jerry Muro na yule dada.

Nawashukuru sana TBC kwa kuwa waliona kipaji changu na hawakunibania kama nilivyokuwa nabaniwa huko kwingine, ndiyo maana leo hii wengi wananitaka tena kwa dau kubwa ila nimekuwa mgumu kuhama TBC, naipenda kwa moyo wangu wote.

Swaggaz: Umefanya kazi na mastaa wengi, staa gani aliwahi kukuudhi katika kazi zako?

 D’Jaro Arungu: Waliniudhi kipindi naanza kutangaza, ukiwaita kwa interview wana-promise then siku ya siku hawaji. Baadhi yao ni Profesa Jay,  Juma Nature, Linex, Ali Kiba, Banana Zoro, MB Dog nk.

Niliwasamehe maana nilijua ipo siku watanitafuta wao, ila heshima sana kwa AY toka enzi hizo hadi sasa hakuwahi kukosa kipindi kama una interview naye na sasa wao ndiyo wanaomba waje tena foleni ni kubwa.

Swaggaz: Staa gani wa kike Bongo anakuvutia na je unatazama filamu za Kibongo na unawashauri nini wasanii?

D’Jaro Arungu: Kwanza sitazami kabisa filamu hivyo sina cha kuwashauri na mrembo anayenivutia ni Jokate Mwegelo.

Swaggaz: Umewahi kukutana na malalamiko ya wasanii kudai unawabania?

D’Jaro Arungu: Kwangu mimi hawajawahi kusema nawabania, wengi wamepita mkononi mwangu kama kina Diamond, Nay wa Mitego, 20%, marehemu Omary Omary na Dogo Mfaume, Timbulo, Best Naso, Chief Maker na wengine wengi na wanathamini mchango wangu.

Swaggaz: Watu gani ni muhimu kwenye safari yako ya utangazaji?

D’Jaro Arungu: Napenda nimshukuru mtangazaji wa Uhuru FM, Sigori Paul. Yeye na Paul James ‘PJ’ ndiyo walinipigania Times FM hadi nikaanza kuripoti habari za michezo kwa kujitolea ingawa nilipigwa chini baadaye.

Lakini leo hii ripoti za Ipsos zinaonyesha Baba Mzazi D’jaro Arungu ndiyo mtangazaji wa redio anayependwa zaidi na hata Tuzo za Watu zilionyesha  hivyo ndiyo maana nilishinda na hivi majuzi tuzo za Tanzania Instagram Awards nilishinda kipengele cha ‘Best Male Presenter’.

Swaggaz: Una ushauri gani kwa vijana ambao wanakata tamaa wakikutana na magumu kwenye maisha?

D’Jaro Arungu: Nawaasa kutokukata tamaa mapema, leo hii nisingekuwa hapa na nimejiendeleza kusoma mpaka sasa nipo Chuo Kikuu cha Tumaini, namaliza mwakani mwezi Oktoba, Shahada ya Mawasiliano ya Umma.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,099FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles