25.2 C
Dar es Salaam
Thursday, April 18, 2024

Contact us: [email protected]

ACHA KUMLILIA, YUPO ANAYEKUPENDA ZAIDI – 2

LEO tunamalizia mada yetu iliyoanza wiki iliyopita ambayo kwa kiasi kikubwa imekazia katika kuonyesha umuhimu wa kujua, kulinda na kuheshimu thamani yako. Lazima ifikie mahali ujikubali mwenyewe.

Kwa ambao hawakuwa nasi wiki iliyopita, nitaeleza kwa ufupi nilivyoanza. Nilianza na kisa cha Diana na Ben. Diana alikuwa kwenye uhusiano na Ben, lakini wa manyanyaso.

Alikutana nami ofisini na nikamshauri cha kufanya – kuchukua maamuzi magumu, kutokana na maelezo yake na namna alivyokuwa akiteswa na Ben.

Miezi michache baada ya kuamua kujikubali, akakutana na mtu mwenye mapenzi ya dhati kwake na kufunga naye ndoa.

Diana nilikutana naye wiki mbili zilizopita Mlimani City, Dar akiwa na mumewe na mtoto wao mdogo. Naamini sasa wasomaji ambao hawakunisoma wiki iliyopita wamepata mwanga.

 

MATATIZO HAYAVUMILIKI

Hapa nataka nieleze kwa uwazi kabisa kuwa, wahanga wakubwa wa hiki ninachozungumza hapa ni wanawake. Asilimia kubwa ya wanawake hung’ang’ania uhusiano hata kama anaona wazi hauna future, kwa madai kuwa mapenzi ni kuvumiliana!

Achana na hiyo misemo ya kizamani. Haukuingia kwenye uhusiano kwa ajili ya kupata matatizo. Yaani uteswe, umfumanie, ufume meseji za mapenzi kwenye simu yake… halafu uendelee kusema unavumilia.

Ni mjinga peke yake ndiye ambaye anaweza kukubali kuvumilia kwenye moto. Heshimu afya yako, jikubali. Haupo kwake kwa sababu ya bahati tu. Upo kwa sababu na kama sababu imeonekana haipo tena, chapa lapa.

Maisha hayapo kwake tu.

 

UCHUMBA WA MUDA MREFU

Kuna wale wenzangu ambao wanakuwa kwenye uchumba kwa miaka minne, mitano mpaka saba. Ndugu yangu, uchumba gani huo?

Mbaya zaidi, katika huo uchumba wenyewe, mwanamke anakwenda kwa mwanaume, anafua, anapika, anafanya usafi wa nyumba nzima. Kwani amekuoa? Itampa haraka gani ya kufikiria kukuoa ikiwa kila kitu unamfanyia?

Eti mchumba anakwenda kushinda kwa boyfriend, mwingine analala kabisa huko. Atakuwa na jipya lipi? Halafu baada ya miaka mitano, unasikia jamaa ameoa mwanamke mwingine.

Wewe unabaki kuwa mchumba wa miaka, halafu anachukua mke! Shtuka, usigeuzwe mwanamke wa majaribio. Ijue thamani yako na uilinde. Kama anakupenda afuate taratibu.

Ukiacha sababu ya masomo (chuo) ambayo hata hivyo haiwezi kuwa miaka mingi, hakuna sababu ya uchumba wa watu serious kuzidi miaka miwili, ukiona uko kwenye uchumba wa namna hiyo, tafakari.

Hakunaga mchumba wa miaka, ila kuna mke na mume wa miaka!

 

JIKUBALI

Hili sasa ni kwa wote. Mtazame kwa makini mwenzi wako. Ukiona ameanza vitimbi, unatakiwa ushtuke. Usikubali kupotezewa muda wako.

Kuwa makini kufanya uchaguzi wa mwenzi, lakini pata muda wa kumsoma. Usijishushe kwake, uwe kama umekwenda kwake kwa msaada… kwamba akikuacha, basi hapatakuwa na mwingine mwenye kukupenda.

Hayo ni mawazo mfu. Mawazo ya wasiojiamini, lakini kama unajiamini unaweza kuchukua hatua na maisha yakaendelea. Tena basi kwa taarifa yako, wakati unang’ang’ania kuwa na mtu ambaye anakufanyia vitimbi vya wazi kuonyesha kuwa hakutaki, unajifunga kwa mwingine mwenye nia ya dhati.

Kwanini ujizibie riziki yako kwa mtu ambaye anaonekana dhahiri hana nia ya dhati na maisha yako? Kwani yeye ndiye mwanaume pekee au mwanamke pekee?

Unaogopa kumuacha kwa sababu unampenda sana, kwani ulizaliwa naye? Hivi ikitokea leo ukasikia huyo unayemng’ang’ania amekufa, utakwenda naye?

Fikirisha akili yako kwa makini. Wewe una thamani kubwa. Jikubali. Jipe hadhi ya juu. Ukianza kujikubali mwenyewe kwanza, utawafanya na wengine wanaokuzunguka, wakukubali, wakuheshimu, wakupende na wakupe daraja la juu.

Kujikubali ndiyo kila kitu, lakini ukweli ni kwamba, hakuna atakayekukubali ikiwa mwenyewe hujikubali. Anza kujikubali kuanzia leo rafiki yangu.

Diana ametupa somo kubwa sana. Tujifunze kutoka kwake.

Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano, aliyeandika vitabu maarufu True Love, Let’s Talk About Love na Maisha ya Ndoa. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha SIRI ZA NDOA YENYE FURAHA kitakachokuwa mitaani hivi karibuni.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles