MKALI wa muziki wa Bongo Fleva, Naseeb Abdul ‘Diamond’ (Diamond Platinum), amesema pindi atakapoacha muziki atatumikia siasa huku akitamani kuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Msanii huyo aliweka wazi mpango wake huo hivi karibuni alipohojiwa katika kipindi cha Papaso kinachoongozwa na mtangazaji, Di’jaro Arungu ambapo aliweka wazi kwamba akiingia katika siasa atalenga kuwa Waziri wa Michezo pindi Waziri Nape Nnauye atakapomaliza muda wake.
“Kwa hivi sasa bado sijaingia kwenye siasa ila nikiingia baadaye atakapomaliza Nape nafasi yake nitachukua mimi,’’ alieleza na kuongeza:
“Kile cheo nakiweza kwa sababu mambo ya mpira, movie nayaweza na nikiwa waziri nitavifanya viweze kuleta maendeleo makubwa,” alieleza bila kufafanua atabadilishaje viwe vya maendeleo tofauti na wanavyofanya viongozi wa sasa.
Hata hivyo, Diamond hakuweka wazi kwamba ataingia kwenye siasa kupitia chama gani na mwaka gani.