MSANII wa Bongo Fleva, Elias Barnabas ‘Barnaba Boy’, ameeleza kwamba wasanii wanaohofia kutoa albamu huwa hawaamini ubora wa kazi zao na pia hawajui soko la kuuzia albamu hizo.
Barnaba aliweka wazi hayo jana alipotembelea ofisi za Kampuni ya New Habari (2006) Ltd inayochapisha magazeti ya Mtanzania, Bingwa, Dimba, Rai na The African iliyopo Sinza Kijiweni.
Barnaba akiwa na timu yake ya wasanii, prodyuza na mtaalamu wa mitambo, alisema baadhi ya wasanii wamekuwa wakitoa nyimbo kila mara bila kuachia albamu kama wanavyofanya wengine kwa kuwa kazi zao siyo nzuri.
“Nashangaa kwanini mtu anakuwa hatoi albamu wakati anakuwa na nyimbo nyingi zinazomuwezesha kutoa albamu licha ya wizi uliopo wa nyimbo zetu, lakini pia kama una nyimbo nzuri na unajua mfumo mzuri wa kuuza nyimbo zako kupitia mitandaoni huwezi kuacha kutoa albamu,” alifafanua Barnabas.
Msanii huyo ambaye ana albamu tatu alisema mwaka huu anatarajia kuachia albamu yake nyingine itakayokuwa na jumla ya nyimbo nane.