23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

TFF, ZFA zazua sokomoko bungeni

Nape Nnauye bungeniNA KHAMIS MKOTYA, DODOMA

UHUSIANO wa kimajukumu baina ya Shrikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) na Chama cha Soka Zanzibar (ZFA), umeleta mjadala mpana bungeni.

Mjadala huo uliibuka bungeni jana kutokana na majibu ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Wasanii na Michezo, Nape Nnauye, kusema kwamba TFF ni chombo cha muungano ambacho kinawajibika hadi Zanzibar.

Majibu ya Nape yalitokana na swali la nyongeza lililoulizwa na Mbunge wa Konde, Khatibu Said Haji (CUF), aliyetaka kujua maana halisi ya neno TFF.

Mbali ya hilo, mbunge huyo alitaka kujua Serikali inachukua hatua gani dhidi ya watu wanaopeleka mahakamani masuala ya michezo, jambo ambalo ni kinyume na sheria za Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA).

“TFF ndiyo chombo kinachoshughulikia masuala ya soka nchini, nataka kujua neno TFF ile T ni Tanzania au Tanganyika? Kama ni Tanzania michezo si suala la muungano na kama ni Tanganyika kwanini TFF inaingilia masuala ya ZFA?” alihoji.

Akijibu swali hilo, Nape alijichanganya pale aliposema Tanzania Football Association, badala ya Federation ‘shirikisho’ na hivyo kuzua minong’ono, huku baadhi ya wabunge wakisikika wakisema, “hajui maana ya TFF.”

Baada ya minong’ono hiyo na Nape kusahihisha maneno yake alisema: “TFF mamlaka yake yanakwenda hadi Zanzibar, hiki ni chombo cha muungano.

“Kuhusu viongozi wanaopeleka masuala ya soka mahakamani hili ni kosa, kwani ni kinyume cha sheria ya FIFA, tutashughulikia wanaofanya hivi ili kuinusuru nchi isifungiwe na FIFA,” alisema Nape.

Kutokana na majibu hayo, baadhi ya wabunge walisimama kuomba mwongozo wa Spika, wakidai kuwa waziri amesema uongo bungeni kwa kusema TFF ni chombo cha muungano.

Mbunge wa Mkwajuni, Mzee Ngwali Zubeir alitaja kanuni ya 68 inayokataza mbunge kusema uongo.

“TFF si chombo cha muungano, lakini tumeshangaa majibu yaliyotolewa hapa, sasa kama waziri kasema uongo bungeni anafanywa nini?” alihoji mbunge huyo.

Naye Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), aliomba mwongozo na kusema kuwa waziri amesema uongo bungeni, huku akinukuu kanuni ya 63 (1).

“TFF haihusiki na masuala ya michezo ya Zanzibar kwa kuwa kule ipo ZFA na huku ipo TFF. Kimsingi ZFA ni mwanachama wa CECAFA na Chama cha Mpira wa miguu barani Afrika (CAF),” alisema.

Hata hivyo, Spika wa Bunge, Job Ndugai, alisema miongozo hiyo ameichukua na ataitolea uamuzi baadaye, huku akihitimisha hoja hiyo kwa kusema:

“Kwani ZFA ni mwanachama wa FIFA? Haya miongozo yenu nitaipatia majibu baadaye,” alisema Ndugai.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles