24 C
Dar es Salaam
Thursday, July 25, 2024

Contact us: [email protected]

Simba yatishia kugomea ligi

KIKOSI-1NA MWALI IBRAHIM, DAR ES SALAAM

KLABU ya soka ya Simba imetishia kugomea michuano ya Ligi Kuu Tanzania Bara ikiwa watafika raundi ya 20 ya ligi hiyo wakiwa wametofautiana idadi kubwa ya mechi na timu nyingine ikiwemo Azam FC inayoshiriki michuano maalumu nchini Zambia.

Uongozi wa klabu hiyo pia umelitaka Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kuhakikisha ligi inamalizika tarehe iliyopangwa, vinginevyo shirikisho hilo litalazimika kulipa gharama ambazo zitaongezeka na kuzidi bajeti waliyopanga kwa msimu huu.

Uamuzi wa Simba ulipitishwa juzi katika kikao cha Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo kilichokutana kujadili mwenendo wa Ligi Kuu pamoja na kuahirishwa kwa baadhi ya mechi kutokana na sababu mbalimbali.

Akizungumza Dar es Salaam jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema watawasilisha uamuzi waliofikia na msimamo kwa TFF ili wahakikishe ratiba ya ligi haipanguliwi hivyo ili michuano hiyo imalizke kwa wakati vinginevyo watakuwa wamezigharimu timu zinazoshiriki.

“Huu ndio msimamo wetu na tutaandika barua kwa TFF kuwaeleza kuwa kama tutapishana kwa idadi kubwa ya mechi hadi kufikia raundi ya 20, hatutakubali na hatutakuwa tayari kucheza ligi kwani kanuni zipo wazi lakini wameanza kuzikiuka kwa kuruhusu timu kwenda kushiriki bonanza.

“Kama timu ilikuwa na nia ya kupata mechi za kujipima nguvu kwa ajili ya maandalizi ya michuano ya kimataifa wangeweza kucheza mechi za kirafiki hapa nchini na si kuvuruga ratiba,” alisema.

Manara alisema kwa mujibu wa kanuni za ligi kifungu cha 9(a) kinaeleza kuwa timu inaweza kuahirishiwa mechi zake ikiwa idadi kubwa ya wachezaji wake wataitwa kuichezea timu ya Taifa.

Kifungu kingine cha 9(b) kinaeleza kuwa ili timu iharishiwe mechi zake za ligi ni lazima iwe inakabiliwa na michuano ya kimataifa na taarifa itolewe ndani ya siku 14, wakati kifungu cha 9(d) cha kanuni hiyo kinasema kwamba mechi zinaweza kuahirishwa kama kuna dharura ya kibinadamu.

“Kwa kutumia vifungu hivyo, ni dhahiri TFF imekiuka kanuni zake kwani ilipaswa kutoa taarifa siku 14 kabla kama ilipata barua, kama timu inashiriki mashindano yanayotambulika na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) au Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) si mbaya, lakini bonanza haiwezekani.

“Hali hii ya kuahirishwa kwa mechi za ligi bila sababu za msingi inatugharimu sana ndio maana tunaiambia TFF kama michuano hii isipomalizika kwa muda uliopangwa itabidi watulipe gharama zetu kwani tumeshajipanga kwa tarehe husika,” alisema.

Akizungumzia madai ya fedha za usajili wa mshambuliaji wa kimataifa wa timu hiyo, Daniel Lyanga, Manara alisema uongozi hauna matatizo na mchezaji huyo kama inavyoelezwa na mambo yote yanakwenda vizuri.

“Lyanga aliomba kwa uongozi ruhusa ya kwenda kwao Moshi na tayari amerudi na kujiunga na wachezaji wenzake mazoezini na hakuna matatizo yoyote kati yetu,” alisema.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles