29.8 C
Dar es Salaam
Monday, October 7, 2024

Contact us: [email protected]

DIAMOND AMPA JARIBU LA TATU ZARI

NA SALMA MPELI

NI mwaka wa majaribu kwa mrembo wa Kiganda, Zarina Hassan ‘Zari The Bosslady’. Hivi ndivyo unavyoweza kusema kutokana na  majanga matatu yaliyotikisa maisha ya mlimbwende huyo kwa mwaka huu.

Majanga hayo yalianza kumwandama Mei 25, mwaka huu baada ya mumewe wa zamani, Ivan Semwanga maarufu kama Ivan Don, kufariki dunia akiwa nchini Afrika Kusini.

Ikiwa hata miezi miwili haijapita tangu kuondokewa na baba wa watoto wake watatu, mama yake mzazi, Halima Hassan, alifariki dunia Julai 20.

Baada ya majanga hayo mawili, mtu wa kumtia moyo kwa karibu alitarajiwa kuwa mzazi mwenzake, Naseeb Abdul ‘Diamond Platnumz’, badala ya kuwa hivyo ndipo kidonda cha kuondokewa na mama yake kilivyotoneshwa kabla ya hata miezi miwili kukamilika baada ya juzi Diamond kukiri kuzaa na mwanamitindo Hamisa Mabeto.

Mambo haya yote ndiyo yanayofanya mwaka huu kwa mlimbwende huyo kutokuwa mzuri, ingawa kupitia ukurasa wake wa Instagram ameonekana kutaka mashabiki wake kutoendelea kuchukulia kusalitiwa na Diamond kwa mtazamo hasi na badala yake walichukulie suala hilo kwa mtazamo chanya.

Hata hivyo, mrembo huyo hakuweka wazi kama baada ya Diamond kukiri kuzaa na Hamisa Mobetto, sasa ataendelea na mahusiano naye ili kuwatunza pamoja watoto wao wawili ama ataachana naye na kuendelea na maisha yake.

Zari kupitia mtandao wa Snapchat, amesema Diamond Platnumz amedanganya aliposema kuwa yeye (Zari) alikuwa na habari zote kuhusiana na mimba hiyo.

“Kamwe siwezi kujihukumu kwa kosa la mtu mwingine kwani kama ameamua kunidhalilisha, hiyo ni aibu yake mwenyewe lakini mimi naangalia maisha yangu yanasonga na natazamia zaidi katika kujifunza na kwenda mbele.

“Siwezi kulia kwa matatizo ya mtu mwingine, kikubwa ni maisha yangu na akaunti zangu benki zipo vizuri na wala sina wasiwasi,” alisema Zari.

Kwa upande wake pia msanii Diamond licha ya kwamba amesema yuko tayari kupiga magoti mpaka Afrika Kusini, kumuomba msamaha mzazi mwenzie huyo, bado atakuwa na mtihani wa kupima mambo yatakayomfanya aidha abaki na Zari ama Hamisa.

Zari ni nani

Zari mwenye umri wa miaka 37, ni mfanyabiashara ambaye anamiliki magari ya kifahari na yenye gharama kubwa kama Lamborghini Gallardo, BMW- 2006, Chrysler-2008, Audi Q7-2010 na Ranger Rover Sports.

Ni binti wa Halima Sultan Hassan na Nasur Hassan akiwa na asili ya Kihindi, Somalia, Burundi na Uganda.

Babu mzaa mama yake anatoka India, bibi yake anatoka Uganda, babu mzaa baba ni Msomali ambaye mkewe ni Mrundi.

Mrembo huyu alizaliwa Septemba 23, mwaka 1980 na amekulia katika Mji wa Jinja nchini Uganda.

Alivyokutana na Diamond

Uhusiano wa Zari na Diamond ulianza mwanzoni mwa 2015, ambapo Diamond Platnumz alikwenda Afrika Kusini kwenye tuzo za Channel O na kuibuka na tuzo tatu.

Shughuli ya utoaji tuzo hizo ilipokamilika, Zari alimwalika Diamond kushiriki katika ‘party’ maarufu ambayo mwanadada huyo huwa anaiandaa kila mwaka nchini Uganda inayoitwa ‘All White Ciroc Party’.
Baada ya sherehe hiyo, walifuatana kwenda nchini Rwanda na Burundi ambapo Diamond alikwenda kwa ajili ya kufanya maonyesho yake.

Baada ya muda mfupi picha zao zenye ‘harufu’ ya kimapenzi zilianza kusambaa mitandaoni na kuzua gumzo Afrika Mashariki, ambapo mrembo huyo alikuwa akijulikana zaidi na baadaye kuzama kwenye penzi na kufanikiwa kupata watoto wawili, Tiffah na Nillan.

Ivan Don afariki Dunia

 Mei 25, mwaka huu, Ivan ndipo alipofariki ambapo wakati bado wakiwa na uhusiano walipata watoto watatu, Pinto, Quincy na Didy.

Ivan Don alikuwa mfanyabiashara nchini Uganda na Afrika Kusini, alifariki dunia kwa ugonjwa wa shambulio la moyo katika Hospitali ya Steve Biko Academy huko Afrika Kusini.

Diamond kuchepuka na Dillish Methews

Mbali na Hamisa, wiki iliyopita katika mitandao ya kijamii, pia zilisambaa taarifa kuwa Diamond Platnumz alikuwa visiwani Zanzibar akila bata na mrembo Dillish Methews ambaye ni mshiriki wa shindano la Big Brother Afrika mwaka 2013, taarifa ambazo msanii huyo wa Bongo Fleva amezikanusha.

Hamisa Mobetto naye

Kwa upande wa mwanamke aliyezaa na Diamond, Hamissa Mabetto, sakata la ujauzito wake kuhusishwa na Diamond lilianza mapema mwaka huu, ingawa wawili hao walificha mpaka mtoto alipozaliwa ndipo picha na video zilipoanza kusambaa.

Licha ya kuwa baada ya mtoto kuzaliwa, Hamisa alianza kuweka vitu mtandaoni vilivyoonyesha mtoto huyo ni wa Diamond, msanii huyo alikana mpaka juzi alipovunja ukimya na kukiri kwamba aliyezaliwa ni mtoto wake.

Hamisa alizaliwa mwaka 1994 mkoani Mwanza na alianza masuala ya mitindo baada ya kuibuka mshindi wa shindano la Miss Xxxl Back To School Bash mwaka 2010 linaloandaliwa na kipindi cha XXL ya Clouds Fm.

Mwaka 2011 Hamisa alishiriki mashindano ya Miss Dar Indian Ocean na alifanikiwa kushika nafasi ya pili, mwaka huo huo alikuwa mshindi wa pili wa Miss Kinondoni na kufanikiwa kuingia kwenye nusu fainali za Miss Tanzania.

Mwaka 2012 Hamisa alishiriki kwenye mashindano ya Miss University Afrika na kuingia hatua ya 10 bora.

Kutokea hapo Hamisa amekuwa gumzo kwenye tasnia ya mitindo na filamu pamoja na kunogesha video za muziki ‘Video Vixen’ katika video mbalimbali kama My Baby ya Quick Racka My Baby.

Mwaka 2014 Hamisa alitokea kwenye cover page ya Pulse Magazine la Nchini Kenya.

Hivi sasa Hamisa ni mama wa watoto wawili ambao ni Fantasy na Abdulatif.

 

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles