30 C
Dar es Salaam
Friday, January 27, 2023

Contact us: [email protected]

DCB BENKI YAJIWEKEA MALENGO MAKUBWA

Na CHRISTINA GAULUHANGA,

BENKI ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002, ikiwa na amana ya Sh bilioni 1.8 ambapo hivi sasa imefikia Sh bilioni 112.

DCB imefanikiwa kutoa mkopo wa Sh bilioni 515 kwa wateja wake 456, 036.

Kwa mwaka jana pekee, benki hiyo imefanikiwa kutoa mkopo wa Sh bilioni 60.6 ukilinganisha na Sh bilioni 1.02 zilizotolewa mwaka 2002.

“Tupo katika mkakati wa kuhakikisha tunajitahidi kuongeza mtaji ambao ndio muhimu kwa maendeleo ya benki yetu,” ndivyo anavyoanza kuelezea Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Edmund Mkwawa.

Mkwawa anasema benki hiyo inafuata miongozo yote ya Serikali ambayo ndiyo dira ya maendeleo ya kibenki na usalama wa fedha za wateja na wana hisa.

Anasema kwa sasa benki hiyo imeanzisha huduma za DCB Jirani na DCB Pesa, ambazo lengo kuu ni kuongeza idadi ya watumiaji wa huduma ya benki hiyo ambayo ilianzishwa maalumu kwa ajili ya wananchi.

Mkwawa anasema huduma ya Benki ya DCB  ya ‘Agency Banking’ ni huduma ya kisasa yenye manufaa makubwa kwa jamii.

“Ni imani yangu asilimia 80 ya Watanzania hawana akaunti benki, hivyo itapunguza wigo huu  wa kupeleka huduma za kibenki mitaani kupitia mawakala,” anasema Mkwawa.

Anasema katika kuhakikisha huduma hiyo inatolewa kwa viwango vinavyotakiwa, imeingia mkataba na mawakala 219 waliosambaa Dar es Salaam.

Pia anasema wamejipanga kufikisha huduma hiyo katika mikoa mbalimbali ikiwamo Pwani, Dodoma, Morogoro, Tanga, Mwanza, Geita, Shinyanga, Kahama, Mtwara, Arusha, Iringa na Mbeya.

“Kama benki tumejipanga Mungu akipenda kufikisha idadi ya mawakala 1,500 nchi nzima,” anasema Mkwawa.

Mkwawa anasema faida ya huduma ya DCB Jirani, itaongeza idadi ya wateja kwa kufikisha  huduma za kibenki kwa watu walio mbali na mjini ambao awali hawakupata fursa za huduma za kibenki.

Pia itasaidia kupunguza gharama za ujenzi wa matawi, kuwezesha kupata amana za kutosha, kupata amana kubwa zaidi na kumwezesha mteja kuweka, kutoa, kuhamisha fedha, kulipia bili mbalimbali.

Mkwawa anasema mteja anayetumia huduma za DCB Pesa, anaweza kuweka pesa kwenye akaunti yake ya DCB Pesa kutoka Tigo Pesa, M-pesa, Airtel Money na Halotel kupitia simu ya mkononi.

Changamoto

Anasema benki hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa amana ambapo agizo la Serikali Kuu kuzitaka manispaa na halmashauri zote kuhamisha benki na kuzipeleka Benki Kuu.

Mkwawa anasema kwa sababu lengo la uanzishwaji wa benki hiyo ni kuhudumia wananchi, wateja wakubwa walikuwa ni manispaa.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa DCB, Profesa Lucian Msambichaka, anasema bodi itahakikisha inabuni na kuanzisha huduma za kisasa zinazoendana na ukuaji wa teknolojia ulimwenguni, lengo likiwa ni kumwezesha mteja kuzipata kwa urahisi zaidi.

Anasema wataongeza mtandao wa matawi ya benki ambao una gharama kubwa, hivyo wamejipanga kutumia teknolojia za kisasa kuwafikia wateja wote kwa gharama nafuu.

Profesa Msambichaka anasema benki hiyo inakabiliwa na changamoto ya ukosefu wa  amana za muda mrefu kukidhi idadi kubwa ya mikopo inayoombwa na wateja kwa ajili ya kuendeleza biashara mbalimbali na kuboresha maisha yao.

Anasema bodi hiyo imedhamiria kwa dhati kushirikiana na uongozi wa manispaa  katika kuhamasisha kuendelea kutumia shughuli za kibenki kwa asilimia 100.

“Lengo letu ni kuona kuwa suala hili linapatiwa ufumbuzi kwa faida ya pande zote mbili, yaani benki na mwekezaji wote wapate gawio,” anasema Profesa Msambichaka.

Anasema wanashukuru manispaa za Mkoa wa Dar es Salaam kukubali kupitisha huduma za kibenki katika benki yao kwa mikopo ya wanawake na vijana.

“ Tunaomba manispaa ziendelee kuleta fedha ile asilimia 10 ya mapato yao zinazotengwa kwa ajili ya mfuko wa kuwakopesha wajasiriamali wanawake na vijana, kwani utekelezaji huu utatuwezesha kukabiliana na ushindani katika tasnia ya benki na kutoa mikopo kwa wingi na yenye gharama nafuu,” anasema Profesa Msambichaka.

Naye, Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kinondoni, Benjamin Sitta, anasema watahakikisha benki hiyo inatekeleza malengo iliyojiwekea.

Anasema uwepo wa benki hiyo umesaidia wajasiriamali wengi kuwezeshwa kiuchumi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles