31.8 C
Dar es Salaam
Tuesday, January 31, 2023

Contact us: [email protected]

MTWARA, LINDI KUNUFAIKA NA MRADI KILIMO-BIASHARA

Na Jamila Shemni, Dar es Salaam

KATIKA jitihada za kuisaidia Serikali kuhakikisha nchi inakuwa na maendeleo endelevu ifikapo 2030, Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan (AKF) umezindua mradi uitwao ‘Kilimo ni Biashara’ ili kutengeneza fursa za kuongeza kipato na ajira kwa wanawake, wanaume na vijana  wa nchi za Afrika Mashariki.

Mradi huu unaendana na Mkakati wa Kukuza Uchumi na Kupunguza (Mkukuta) na unachangia katika Malengo ya Maendeleo Endelevu. 

Uzinduzi huo ulifanywa kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ) na mamlaka husika za Serikali za mitaa.

Akizungumza katika uzinduzi huo, Mkulima Kiongozi kutoka mkoani Mtwara, Makarani Shaweji, alisema mradi huo uko chini ya programu kuu ya E4D/SOGA – Ajira na Ujuzi kwa ajili ya Afrika Mashariki inayotekelezwa na Shirika la Maendeleo la Ujerumani (GIZ GmbH) na kufadhiliwa na Shirika la Misaada la Uingereza (UKaid), Shirika la Maendeleo na Ushirikiano la Norway (Norad) na Serikali ya Ujerumani.

“Mradi huu una lengo la kutengeneza na kuwezesha fursa za kiuchumi kwa wakulima wadogo na biashara za ndani ili kuzalisha, kusindika na kusambaza chakula kwa masoko ya nje, huku mkazo ukiwa kwa sekta ya maliasili,” alisema.

Alisema mradi huu utaigusa mikoa ya Lindi na Mtwara pamoja na uwezekano wa kufika katika maeneo mengine kulingana na uhitaji.

“Kutokana na mradi huu, takribani watu 5,000  pamoja na wanawake 2,000  watapata ongezeko la kipato, takribani watu 400 zaidi watapata ajira na takribani biashara 200 zitaanzishwa na kuwezeshwa,” aliongeza.

Alisema mkazo mkubwa wa minyororo ya thamani ni mbogamboga, kuku, mayai, mazao ya jamii ya kunde na mchele.

 Akifafanua zaidi, Mwakilishi Mkazi wa Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan, Abid Mallic, alisema: “Mradi huu utaandaa na kutoa mafunzo kwa wakulima ili wafanye kazi kama wafanyabiashara wazalishaji na kuzalisha bidhaa hizi kwa idadi na ubora unaohitajika katika masoko lengwa.

“Wakati huo huo mradi huu utakuwa chachu kwa makampuni ya biashara ndogo kabisa, ndogo na za kati yaliyopo kwenye mnyororo wa thamani ya chakula, ikiwa ni pamoja na biashara za usambazaji pembejeo, makampuni ya biashara ya uhifadhi na ukusanyaji, huduma za ufungashaji na mitambo ya usindikaji kama vile kukausha, kusaga na machinjio salama ya kuku.

Naye Tabu Likoko, Ofisa Kilimo Mwandamizi, alisema: “Mradi  huu umekuja wakati mwafaka na nawasihi wakulima wa Lindi na Mtwara kuitumia ipasavyo fursa hii.”

Ally Ahmed Msaki, Mkurugenzi wa Ajira, Tamisemi, alisema: “Kuendeleza kilimo-biashara ni kipengele cha msingi cha sera ya uchumi wa Serikali na hivyo mradi  huu ni hatua muhimu katika mwelekeo huo.”

Huku akitambua juhudi za Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan (AKF), Mkuu wa Wilaya ya Mtwara, alisisitiza ushirikiano kutoka serikalini.

 “Maofisa Ugani wa Serikali wataendelea kufanya kazi pamoja na wataalamu kutoka Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan ili kuhakikisha mradi huu unafanikiwa.”

Tangu mwaka 2009, programu kuu ya Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan (AKF) katika mikoa ya Lindi na Mtwara imekuwa ikifanya kazi na wakulima wadogo zaidi ya 100,000 katika kuboresha na kuongeza uzalishaji, uwezeshaji wa mitandao ya kimasoko na kusaidia upatikanaji wa fedha. Mafaniko makubwa ya mradi huu yamesababisha Mfuko wa Maendeleo wa Aga Khan kupanua wigo wake katika mikoa mingine, ikiwa ni pamoja na Arusha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
208,063FollowersFollow
561,000SubscribersSubscribe

Latest Articles