26.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 27, 2021

DAR YAONJA MACHUNGU UKOSEFU VIWANDA VYA KUSINDIKA VYAKULA

Na ESTHER MNYIKA


KUPANDA kwa bei ya vyakula Dar es Salaam, kunaelezwa kuchangiwa kwa kiasi kikubwa na ukosefu wa viwanda vya kusindika vyakula ambavyo hupatikana kwa wingi kwa msimu.

Katika siku za hivi karibuni, Jiji la Dar es Salaam limeshuhudia ongezeko kubwa la bei ya vyakula lisilo la kawaida kwa bidhaa za chakula kama nyanya, vitunguu na nyinginezo.

Katika kipindi kama hiki mwaka jana, bidhaa kama nyanya zilikuwepo kwa wingi kuliko mahitaji katika masoko mbalimbali na wauzaji walilazimika kuzimwaga kwa kukosa wateja.

Wafanyabiashara na wananchi waliozungumza na MTANZANIA kwa nyakati tofauti, walisema kupanda kwa bei vya vyakula kama nyanya, vitunguu, viazi, mchicha kunatokana na ukosefu wa viwanda vya kusindika bidhaa hizo katika msimu ambao zinapatikana kwa wingi.

Khamisi Juma ambaye ni mfanyabiashara wa Soko la SM2000, anasema mwaka huu bei ya vyakula imekuwa juu sana tofauti na mwaka jana.

Anasema kupanda kwa bei za vyakula kumepunguza uwezo wa watu kununua na kwa hiyo wafanyabishara hawapati wateja wa kutosha.

“Mazao karibu yote yapo juu. Bei za jumla za nyanya kwa tenga kwa sasa ni Sh 50,000 hadi 70,000  wakati kipindi cha nyuma ilikuwa ni kati ya sh  15,000 na 20,000. Vitunguu gunia ni Sh 90,00 hadi 100,000 wakati kipindi cha mwaka jana ilikuwa kati ya Sh 50,000 na 60,000, huku gunia la viazi likienda kwa Sh100,000 hadi 120,000.

Anaelezea hatua ya kupanda bei imechangiwa na wakulima kukata tamaa ya kulima kwa wingi kwa kuwa mara nyingi mazao yao hukosa soko la uhakika na kuharibikia shambani.

Anasema ni zaidi ya miezi mitatu sasa tangu kuanza kupanda kwa bei za vyakula kwa kasi na baadhi ya wafanyabiashara wamefunga biashara kutokana na ukosefu wa wateja wa uhakika haswa kwa bidhaa zinazohabirika haraka.

Naye Herry Mwale, Mfanyabiashara wa nyanya katika  soko hilo, anasema nyanya ni aina ya mboga inayozalishwa kwa wingi na ni zao la kwanza katika mazao ya mboga linalolimwa na kutumika kwa wingi ukilinganisha na mboga nyingine.

 Mwale anafafanua kuwa, nyanya hutumika karibu katika kila mlo na kutokana na umuhimu wake, wakulima wamekuwa wakilima kwa wingi.

Hata hivyo, anasema zao hilo ni rahisi kuharibika haswa linapokuwa linazalishwa kwa wingi, huku asisitiza kuna haja ya kuwa na viwanda vya kusindika ili kuepusha hasara kubwa wanayopata wakulima na wafanyabiashara.

“Wakulima  mwaka jana walipata hasara kutokana na kulima nyanya nyingi ambazo zilikosa soko na kuharibikia shambani. Hapa  nchini bado hatuna viwanda vya kusindika vyakula, tukivuna shambani moja kwa moja vinaingia sokoni, kama kungekuwa na viwanda vya kusindika tusingefikia tulipofikia leo ambapo bei ya nyanya imepanda sana,” anasema Mwale.

Anasema kwa upande wa wafanyabiashara wa  matunda, wamefanikisha kutopata hasara kutokana na uwekezaji wa Kiwanda cha Bakhresa ambacho hununua matunda kwa ajili ya kutengenezea juisi.

Akitolea mfano wa nchi ya jirani ya Kenya, anasema nchi hiyo imefanikiwa katika kilimo kutokana na kuwa na viwanda vya usindikaji ambapo mazao yanapovunwa kiasi kikubwa hupelekwa viwandani kwa ajili ya kusindikwa

Anasema Serikali pamoja na wazo zuri la kuhimiza ujenzi wa viwanda, ni vizuri pia ikaangalia na uwezekanao wa kutengeneza mfumo bora wa masoko ya uhakika wa bidhaa za kilimo ili kuwavutia wakulima kulima kwa wingi.

Anasema Kiwanda cha Dabaga kilichoko mkoani Iringa hakitoshelezi, hivyo wanaiomba Serikali na wadau wengine wa maendeleo kufikiria namna ya kuwakomboa wakulima na wafanyabiashara.

Kwa upande wake, mama Adam mkazi wa Makuburi na mfanyabiashara wa genge la bidhaa mbalimbali  za vyakula vya rejareja, anasema ni kweli kuwa bei za vyakula zipo juu wakati hali ya kiuchumi ni ngumu. Anasema wanalazimika kupunguza bei ili wateja waweze kumudu na hivyo kujikuta wanapata faida ndogo sana.

Anafanua kuwa biashara imekuwa ni ngumu na analazimika kuendelea kufanya kwa sababu hana kazi nyingine zaidi ya genge hilo ambalo analitegemea kupata riziki.

 “Hadi sasa sielewi nini kinachopelekea vyakula kupanda bei, nyanya sasa hatuuzi kwa mafungu na badala yake tunauza moja moja, ambapo nyanya moja ni kati ya shilingi 200, 250 hadi 350. Kipindi cha nyuma bidhaa kama nyanya, vitunguu, ndimu, viazi na vinginevyo  zilikuwa ni nyingi na bei zake zilikuwa zipo chini,” anasema mama Adam.

Frolah Wiliam ambaye ni mkazi wa  Mabibo Sahara, anasema vyakula vimepanda bei sana lakini hawana jinsi na wanalazimika kununua kwa sababu ni moja ya mahitaji muhimu kwa binadamu.

Anasema kuna wakati analazimika kununua  nyanya za kopo kwa sababu bei yake ipo chini kidogo ambayo huchanganywa na nyanya za kawaida.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
163,388FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles