29.2 C
Dar es Salaam
Wednesday, October 20, 2021

USHIRIKISHWAJI WATAALAMU SEKTA YA KILIMO BADO HAUTOSHI

Na LEONARD MANG’OHA


TANZANIA ni miongoni mwa nchi zilizo na rasilimali kubwa ya ardhi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati pamoja na vyanzo vingi vya maji kama vile mito, maziwa na mabwawa makubwa kwa madogo.

Ikiwa na eneo la zaidi ya kilomita za mraba 965,000, hekta milioni 44, ni ardhi inayofaa kwa shughuli za kilimo lakini ni asilimia 23 tu ya eneo hilo ndilo hutumika kwa kilimo, jambo linaloonyesha kuwa bado kilimo hakijafanyika kwa kiwango kikubwa.

Wakulima wengi wanatumia mbinu duni za kilimo, wakilima kwa jembe la mkono bila kutumia mbolea wala kupata ushauri wa kitaalamu na huku wakitegemea mvua za misimu ambazo si za kuaminika.

Serikali yenyewe pia haijaona haja ya kuanzisha mashamba makubwa ya umwagiliaji yatakayowezesha kuzalisha kwa ufanisi ambayo mbali na kuzalisha pia yatatoa ajira kwa vijana wengi.

Wafanyabiashara wengi bado hawajaona fursa katika sekta hii ambayo wanaweza kuzalisha na kuanzisha viwanda vidogo vya kusindika mazao yao kabla ya kuyaingiza sokoni.

Serikali kwa nafasi yake inapaswa kuhakikisha inaweka mazingira yatakayowavutia watu wengi kuingia katika sekta ya kilimo, ikiwa ni pamoja na kutenga maeneo maalumu ya kuendesha shughuli za kilimo na kuhakikisha inapelekwa miundombinu ya maji ili kuendesha kilimo chenye tija.

Kama hili litafanyika, vijana wanaohitimu ngazi mbalimbali za elimu wataona umuhimu wa kuendesha shughuli za kilimo na kupunguza  tatizo la ukosefu wa ajira.

Profesa Damian Gabagambi ambaye ni Mtaalamu wa Uchumi na Mhdhiri kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo Sokoine (SUA), anasema sekta ya kilimo inapaswa kufanywa kuwa kiongozi wa uchumi wa Tanzania.

Anasema hilo linaweza kufikiwa ikiwa watunga sera watakuwa wakitoa mitazamo ya kuimarisha kilimo inayotoka mioyoni na si kwa mitazamo ya kisiasa.

Prof. Gabagambi anafafanua kuwa, ni jukumu la Serikali kuhakikisha wanakusanya na kuunda makundi yanayoweza kukopeshwa na kufanya kazi zao kwa utaratibu maalumu.

“Nchi inaendelea kutokana na dira za watawala, kama watawala watatumia kichwa kuongoza mambo yote, hakuna maendeleo yoyote yatakayofikiwa.

“Watunga sera waelewe kuwa kilimo ni taaluma na tunao wataalamu wa kilimo hapa SUA je, wanawatumia?” alihoji Profesa Gabagambi.

Anasema SUA inapaswa kutumika kutafuta majibu ya matatizo yanayoikabili sekta ya kilimo ili kukabiliana na changamoto zilizopo na kukipa umuhimu.

Mhadhiri wa Masuala ya kilimo kutoka SUA, Profesa Susan Msola, anasema ni lazima kuzingatia namna bora ya kuendesha shughuli za kilimo, ikiwa ni pamoja na uangalizi wa kitaalamu kuhakikisha linatoa mazao bora na mengi.

Anasema wakulima wengi hawafuati ushauri wa kitaalamu, jambo analosema kwa kiasi kikubwa husababishwa  na uhaba wa wataalamu.

Anataja tatizo la kukosekana kwa masoko ya mazao yanayozalishwa kuwa ni miongoni mwa mambo yanayowavunja moyo wakulima wengi, hivyo ni vema kuhakikisha upatikanaji wa masoko ya ndani na nje ya nchi.

Kwa mtazamo wake, anaona ni vyema uzalishaji wa kilimo ukaimarishwa hasa kwa kuendeshwa kwa kilimo cha umwagiliaji ambacho anasema bado ni mdogo, hivyo mipango madhubuti inahitajika.

Mipango ya namna ya kuanzisha skimu za umwagiliaji na kusimamiwa kwa makini na kuepuka matumizi ya pembejeo duni, ikiwa ni pamoja na kuwatumia wabobezi katika sekta hiyo inayoelezwa kuwa uti wa mgongo wa uchumi wa Tanzania.

Anasema kwa sasa wako wataalamu wazuri wanaozalishwa na vyuo vya hapa nyumbani kama vile wahandisi wa kilimo na wazalishaji ambao iwapo watatumiwa vizuri, watasaidia kuimarisha kilimo.

Anasema SUA kama taasisi ya elimu pamoja na kuwezesha kutoa elimu kwa wataalamu mbalimbali, pia wamekuwa wakifanya tafiti ambazo zimekuwa zikitoa majibu hivyo wanapaswa kuunganishwa na watu wengine watakaoweza kufanyia kazi tafiti hizo kupitia wizara ya kilimo.

“Tunatumika pale tunapohitajika, ila ni lazima tuendelee kutumika zaidi ili kusaidia kutatua matatizo yanayojitokeza, utaalamu upo na wataalamu wapo nasi tunakubali kutumika,” anasema Profesa Msola.

Anasema kwa kiasi wamekuwa wakishirikishwa katika utungaji wa sera za kilimo, hivyo anaamini sera si tatizo sana bali jambo la msingi ni utekelezaji na kuweka mikakati ya namna ya utekelezaji wa sera hizo.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

66,457FansLike
162,594FollowersFollow
522,000SubscribersSubscribe

Latest Articles