23.3 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Chuo cha NIT kununua ndege tatu

Na NORA DAMIAN-DAR ES SALAAM

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinatarajia kununua ndege tano za mafunzo kukabili upungufu wa rasilimali watu katika sekta ya anga nchini, hasa marubani.

Ndege hizo zitanunuliwa mwakani kwa ushirikiano wa Serikali na mkopo wa Dola za Marekani 21,250,000 ambazo ni takribani Sh bilioni 48.8 ambao chuo hicho umepata kutoka Benki ya Dunia (WB).

Akizungumza jana wakati wa mahafali ya 34, Mkuu wa chuo hicho, Profesa Zacharia Mganilwa, alisema mradi huo utakaoanza Februari mwakani unalenga kukiwezesha chuo hicho kuwa kituo cha umahiri cha mafunzo ya marubani, wahandisi wa matengenezo ya ndege na wahudumu wa ndani ya ndege.

“Sekta ya anga kwa sasa inakua kwa kasi kwa wastani wa asilimia 12 kwa mwaka na rasilimali watu katika sekta hii ina changamoto nyingi na kubwa.

“Tunaendelea kutoa mafunzo ya uhandisi wa matengenezo ya ndege, mafunzo ya wahudumu wa ndani ya ndege na tupo katika hatua za mwisho za maandalizi ya mafunzo ya urubani,” alisema Profesa Mganilwa.

Kwa mujibu wa Profesa Mganilwa, marubani waliopo nchini kwa sasa ni 400 wakati mahitaji halisi ni kati ya 700 na 800.

Alisema pia mradi huo pia utahusisha ununuzi wa vifaa vya teknolojia ya kisasa, ujenzi wa miundombinu ya kufundishia kama mahanga ya ndege, madarasa, maabara, karakana na mabweni.

Profesa Mganilwa alisema ili kuongeza uwezo wa chuo katika mafunzo bora na ya kiwango cha kimataifa, wana makubaliano ya ushirikiano na vyuo vikuu vya Chenyang Aerospace na Zhenhzhou vya nchini China na Shirika la AVIC la China ambalo lina chuo kinachofundisha marubani Afrika Kusini kinachodahili wanafunzi 200 kila mwaka.

Alisema pia wameanza utekelezaji wa mradi wa kukipandisha hadhi kuwa chuo kikuu cha usafirishaji kwa ufadhili wa Serikali ya China ambapo fedha zitatumika kujenga madarasa, maabara, kumbi za mihadhara, karakana, mabweni na ununuzi wa vifaa vya kufundishia na kujifunzia.

Profesa Mganilwa alisema ujenzi utaanza mara baada ya kukamilika kwa upembuzi yakinifu unaofanywa na timu ya wataalamu kutoka Chuo Kiku cha Southwest Jiaotong cha China.

Profesa Mganilwa alisema kwa sasa chuo hicho kinatekeleza mpango mkakati wa tatu wa miaka mitano (2016/2017 – 2020/2021) kwa lengo la kuzalisha wataalamu katika nyanja zote za usafirishaji watakaoweza kukabiliana na changamoto za maendeleo ya sekta hiyo na kushiriki azma ya Serikali ya kuwa nchi ya uchumi wa viwanda.

“Tumeanza kuhuisha mitaala ya stashahada na shahada ya uhandisi wa magari na mitambo na kuimarisha kituo cha ukaguzi wa magari ili kupunguza ajali za barabarani na kuongeza ufanisi kwa magari ya aina zote,” alisema.

Alisema pia wameendelea kutoa mafunzo na kuhuisha mitaala ya stashahada, shahada na stashahada ya uzamili katika usafirishaji wa reli na kwamba wameingia makubaliano ya ushirikiano na Chuo Kikuu cha Taifa na Uchukuzi cha Korea na Chuo cha Ufundi Stadi na Teknolojia cha Zhengzhou China.

Mkuu huyo wa chuo alisema katika kuboresha utoaji mafunzo ya reli, hivi sasa wanataaluma wawili wanaendelea na mafunzo ya shahada za uzamili katika uhandisi wa reli nchini Ethiopia kwa ufadhili wa Benki ya Dunia.

Naye mgeni rasmi katika mahafali hayo, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Atashasta Nditiye, alikitaka chuo hicho kuhakikisha kinatoa mafunzo bora yatakayosaidia kupatikana wataalamu wa kisasa katika sekta ya usafirishaji.

Aliwataka wahitimu kutumia maarifa na ujuzi walioupata kuleta maendeleo ya kwao binafsi na taifa kwa kujiajiri au kuajiriwa.

Katika mahafali hayo, wahitimu 1,543 walitunukiwa tuzo mbalimbali na kati yao wanawake ni 412 sawa na asilimia 27.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles