23.3 C
Dar es Salaam
Saturday, April 20, 2024

Contact us: [email protected]

Makonda anusurika mtego wa JPM

ANDREW MSECHU Na ELIZABETH HOMBO-DAR ES SALAAM

MKUU wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda ameukwepa mtego wa Rais Dk. John Magufuli kuhusu hatima ya ufukwe wa Coco.

Hatua hiyo inatokana na uamuzi wake wa kuanza kueleza mikakati itakayofanyika, ikiwamo kuundeleza ufukwe huo sambamba na kujenga mabanda kwa wafanyabiashara na vyoo vya kisasa.

Kutokana na maelezo hayo ya utangulizi, Rais Magufuli alisema amemkwepa kwa kumuwahi kwani ilikuwa kuna uamuzi mgumu dhidi yake.

Alisema ufukwe huo wa Coco unatia aibu kwa sababu hakuna hata choo hali ya kuwa mapato yanakusanywa kila siku.

Mkuu huyo wa nchi alitoa kauli hiyo jana Dar es Salaam, wakati wa uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa daraja la kisasa la Selander ambalo linapita baharini.

“Nimefurahi maneno ya RC (Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda) kuwa wataboresha pale Coco Beach kuliko kukaa vile kwa sababu panatia aibu kwa jiji kama la Dar es Salaam.

“Eneo lile halina hata choo, ni lazima tuzizungumze aibu, lakini wanakusanya mapato kila siku sasa sijui zinaenda wapi. Ukipaki gari pale ni shilingi 2,000. Sasa hatujui hizo fedha zinaenda wapi.

“Zimeshindwa hata kujenga mabanda yanayofanana na pale ili wananchi wakafanye biashara vizuri ili pawe mahali pa utalii.

“Sasa leo naona RC umenikwepa, umeniwahi ukasema hatua utakazozichukua, bahati yako nzuri maana leo nilikuwa nichukue maamuzi magumu,” alisema Rais Magufuli.

Alisema hatua ya Makonda kueleza kuhusu hatua walizochukua katika eneo la Coco Beach imempa ahueni katika maamuzi aliyokuwa anatarajia kuyatoa jana dhidi ya mkuu huyo wa mkoa.

MAKONDA ALIVYORUKA KIHUNZI

Awali katika hotuba yake, Makonda alimshukuru Rais Magufuli kwa kuhakikisha anairudisha Coco Beach kwa wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam, akisisitiza hatua hiyo inadhihirisha mapenzi ya dhati kwa watu wa mkoa huo.

Aliema baada ya Rais kurejesha ufukwe huo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alishatoa maelekezo ambayo tayari wameshakamilisha kwa kubuni mradi wa kufanya katika eneo hilo.

“Waziri Mkuu kwa maelekezo aliyoyatoa, tayari tumeyatekeleza na sasa tumekamilisha mradi wetu. Tulikuwa na mpango wa kukopa, lakini kwa maelekezo ya Wizara ya Fedha tumeandaa maandiko ya miradi na Serikali imetupa matumaini kwamba mradi wa kuboresha eneo hilo utapokamilika bado tutaweza kuanzisha miradi mingine zaidi, ili daraja na barabara hiyo litakapokamilika iweze kuwa na manufaa zaidi kwa wananchi,” alisema.

Alisema kutokana na namna mradi huo ulivyo, kukamilika kwa daraja hilo hasa katika eneo linalounganisha barabara za maeneo kadhaa eneo la Masaki, kutasaidia eneo la Coco Beach kufikika kwa urahisi, hivyo kurahishisha shughuli za kiuchumi katika eneo hilo.

JINA LA DARAJA

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli alipendekeza jina la daraja hilo libadilishwe kutoka Daraja la Selander, akisema kama ikiwezekana liitwe Tanzanite ili litumike kutangaza Tanzania na Jiji la Dar es Salaam.

“Dar es Salaam hivi sasa imebadilika sana, sasa inakuwa jiji la biashara, nitaondoka Dar es Salaam ikiwa nzuri, nitaondoka sasa itakuwa mahali pazuri pa kufanyia biashara kwa sababu miradi mingi inatekelezwa na itabadilisha sura ya Dar es Salaam.

“Ninaamini siku moja kurudi kuitembelea Dar es Salaam pamoja na kwamba mnaiita New Selander Bridge, lakini inawezekana likatafutiwa jina zuri la kuitangaza Tanzania na Dar es Salaam kwa sababu Selander itaendelea kuwepo.

“Waziri (Isack Kamwelwe),  mnaweza mkaitafutia jina zuri, mnaweza hata mkaiita Tanzanite Bridge, ninazungumza tu sijasema liitwe hivyo.

“Bahati nzuri makazi ya mabalozi wengi wanakaa hapa karibu na huwa wanakumbana na kero ya foleni hapa, nina uhakika watakapokuwa wanapita wataitangaza Tanzanite… najaribu tu kupendekeza, lakini ninyi mtalifikiria ili muone ni jina gani ambalo mtalipa daraja hili,” alisema Rais Magufuli.

Hata hivyo, wakati akimalizia hotuba yake, Rais Magufuli alisisitiza tena kwamba daraja la Kigamboni lilipewa jina la Daraja la Mwalimu Nyerere kwa kuwa lilikuwa wazo la Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere hivyo mawazo yanamwelekeza daraja jipya liitwe Tanzanite.

“Kwa daraja hili hapa, mawazo yake ni Tanzanite kwa hiyo ni vyema liitwe Tanzanite, lakini wizara inaweza kuamua kubuni jina jingine. Sasa siyo msubiri hadi lije kupewa jina la mtu hapa,” alisema.

Alisema mradi huo utahusisha ujenzi wa daraja lenye urefu wa kilomita 1.03 ambalo ni refu zaidi hapa nchini likifuatiwa na daraja la Rufiji Mto Ruvuma mita 720, daraja la Nyerere mita 680, daraja la Magufuli Kilombero mita 384.

“Mradi huu utaleta manufaa mengi, utatatua kero ya foleni kwa sababu hivi sasa nchi yetu hupoteza takribani Sh bilioni 400 kwa sababu ya foleni, pamoja na kuboresha mandhari ya jiji letu, sasa watani zangu Wazaramo wataamua kuja kufunga harusi kwenye daraja hili au wataenda daraja la Nyerere au wataenda kwenye Fly over ya Mfugale (Mhandisi Patrick Mfugale).

“Mradi huu utagharimu shilingi bilioni 556.1, Serikali yetu itatoa shilingi bilioni 49.457 na kiasi kingine cha Dola za Marekani milioni 91.32 sawa na shilingi bilioni 206.643 ni mkopo wa masharti nafuu kutoka kwa rafiki zetu wa Korea.

“Tunafahamu katika kazi yoyote ile changamoto hazikosekani. Hata hawa marafiki zetu Wakorea wamepitia kwenye changamoto nyingi. Miaka ya 1961 tulikuwa tukilingana nao uchumi.

“Lakini wenzetu wakaamua kufunga mikanda leo wametupa mkopo, sisi pia nina uhakika tukiamua tunaweza kuvuka vikwazo tunavyovipitia na kujitegemea kiuchumi kama ambavyo wao wamefika, hivyo nawasihi Watanzania tuendelee kushikamana na tuchape kazi, ili kuleta maendeleo ya nchi yetu,” alisema.

Alitoa wito kwa wakandarasi wanaojenga daraja hilo kukamilisha ndani ya muda wa miezi 30 waliopewa au kukamilisha kabla ya wakati.

“Ninafahamu Korea kuna mainjinia wazuri, hivyo nina hakika katika kipindi hiki cha miezi 30 kuanzia Oktoba mwaka huu waliopewa wataweza kukamilisha.

“Nitafurahi zaidi ukimaliza mapema kwa sababu sioni sababu ya kuchelewa wakati kila kitu kipo, naomba wafanye kazi usiku na mchana,” alisema Rais Magufuli.

Aliwataka wananchi kutumia fursa ya mradi huo kwa vijana kuomba kazi na kujituma, mama lishe kupika katika eneo hilo na wajasiriamali wengine kuwauzia bidhaa wanaofanya kazi katika mradi huo.

TANROADS

Akitoa maelezo ya ujenzi huo, Mkurugenzi wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Mhandisi Patrick Mfugale alisema mradi huo una lengo la kupunguza msongamano katika Barabara ya Ali Hassan Mwinyi, ukihusisha daraja lenye urefu wa meta 1,030 na barabara unganishi zenye urefu wa kilometa 5.2.

Alisema mradi huo ulibuniwa mwaka 2008 baada ya kubaini kwamba katika daraja la sasa la Selander hupitisha zaidi ya magari 60,000 kwa siku na utagharamiwa na Jamhuri ya Korea Kusini.

Alieleza kuwa ujenzi huo utakamilika bila kuathiri nyumba au uzio wa majengo yote yaliyopo katika eneo hilo ambazo nyingi ni za makazi na ofisi za balozi mbalimbali nchini, japokuwa utaweza kugusa hifadhi ya barabara katika maeneo hayo.

Alisema mradi huo ni moja ya miradi ya kipaumbele katika Jiji la Dar es Salaam kama lilivyo Daraja la Kigamboni na utakamilika ndani ya miezi 36 kuanzia sasa.

Mfugale alisema daraja hilo litakuwa na urefu wa kilometa 1.03 na upana wa meta 20, pia litakuwa na njia nne za magari na njia za wenda kwa miguu kila upande kwa upana wa mita 2.5

Alisema kutakuwa na nguzo kuu tano zinazoshikilia daraja hilo zitakazojengwa kwa zege kitaalamu kwenda chini na juu ya bahari, ambazo zitashikilia nyaya 120 zinazobeba daraja hilo.

Alieleza kuwa daraja hilo linalotarajiwa kuishi zaidi ya miaka 100 litaunganisha barabara za Kenyatta, Toure, Ufukoni na Barack Obama, ambazo kwa pamoja zitaunganishwa kutoka pande zote mbili za daraja hilo.

Kwa upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandishi Kamwelwe alisema ujenzi wa daraja hilo utasaidia kutoa ajira kwa Watanzania kwa mujibu wa sheria ya kazi ambayo itakuwa kwa mikataba ambapo watalipwa na kutozwa kodi.

Alisema katika ajira nyingi za kampuni za kigeni hawapendi kutoa mikataba iliyo wazi kwa Watanzania, lakini atasimamia kuhakikisha wanapata mikataba na kwamba malipo yatafanyika kwa taratibu za Tanzania.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles