27.1 C
Dar es Salaam
Wednesday, June 12, 2024

Contact us: [email protected]

Cameron: Nitaendelea uwaziri mkuu Waingereza wakiamua kujiondoa EU  

David-CameronLONDON, UINGEREZA

WAKATI Waingereza wakipiga kura leo kuamua iwapo wabaki au wajiondoe uanachama kutoka Umoja wa Ulaya (EU), Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron, amesema ataendelea kutumikia wadhifa wake huo.

Upigaji kura huo unatokana na mitazamo tofauti iliyojitokeza nchini hapa kwa kuwa baadhi ya Waingereza hawakufurahishwa na mfumo unaotumika katika umoja huo wenye makao makuu Brussels, Ubelgiji.

“Siwezi kubashiri matokeo. Hakuna anayejua nini kitatokea… Nitaendelea kutumikia wadhifa wangu na kamwe sitajutia kuitisha kura ya maoni,” aliliambia  gazeti la “Financial Times” la hapa jana.

Aidha viongozi katika makampuni mbalimbali nchini hapa wamewataka Waingereza waunge mkono jitihada zinazofanywa ili kuendelea kuwa mwanachama wa EU.

Takriban viongozi 1,300 wakiwamo 51 wa kampuni 100 zinazowakilishwa katika soko la hisa la jijini London, wameandika risala iliyochapishwa katika gazeti hilo, wakisisitiza hoja yao ya kutojitoa kwenye umoja huo kwani kutailetea Uingereza madhara makubwa ya kiuchumi.

Utafiti wa maoni ya umma unaonyesha kuwa kila upande una uwezo wa kushinda mchakato huo wa leo.

Akizungumza katika mkutano wa wajasiriamali wa Ugiriki mjini Athens juzi, Mwenyekiti wa Halmashauri Kuu ya Umoja wa Ulaya, Jean-Claude Juncker, amewatahadharisha Waingereza wasifikie hatua ya kujidhuru wenyewe.

“Kuwapa kisogo majirani zenu wa Ulaya na kuamua kujiweka kando ni kinyume na yote yale ambayo EU na Uingereza wanayapigania,” alisema.

Juncker ambaye alijiepusha kusema lolote kuhusu kura hiyo ya maoni katika miezi iliyopita, alisisitiza kuwa kujitoa kwao katika umoja huo kutaleta madhara makubwa katika ustawi wa nchi hiyo na hivyo watajidhuru wenyewe.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
588,000SubscribersSubscribe

Latest Articles