24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Bukoba wazuiwa kujenga nyumba mpya

wilfred-lwakatareARODIA PETER na  Veronica Romwald, DAR ES SALAAM

WAKALA wa Jiolojia Tanzania (GST), umewataka wakazi wa Mkoa wa Kagera kutojenga nyumba kwa muda wa miezi mitatu tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani humo.

Tetemeko hilo lilitokea Septemba 10, mwaka huu na kusababisha vifo vya zaidi ya watu 17, majeruhi zaidi ya 200 na kuharibu nyumba 2,063.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Mjiolojia Mwandamizi wa wakala huo, Gabriel Mbogoni, alisema hali hiyo inatokana na hofu ya matetemeko mengine yanayotarajiwa kutokea mkoani humo.

“Ni kweli limepita lile tetemeko la awali,  tumewashauri wananchi wasijenge kwanza makazi mengine ya kudumu kwa sababu bado ardhi haijatulia, matetemeko madogo madogo yataendelea kutokea katika maeneo tofauti tofauti,” alisema.

Mbogoni ambaye pia ni mtaalamu wa matetemeko, alisema hivi sasa yupo mkoani humo pamoja na wataalamu wengine kwa ajili ya kufanya utafiti kabla ya kutoa ripoti maalumu.

“Wananchi waendelee kukaa kwa tahadhari, timu kubwa ya wataalamu kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Wakala wa Jiolojia Tanzania, Chuo cha Ardhi wote hawa tupo Kagera tunafanya utafiti ya kina juu ya tetemeko hili”alisema

Rwakatare

Wakati huo huo, Mbunge wa Bukoba Mjini, Wilfred Lwakatare (Chadema), amewataka wananchi wa mkoa huo kusaidia mkoa wao bila kusubiri kazi hiyo ifanywe na Serikali pekee.

Lwakatare alitoa rai hiyo Dar es Salaam juzi usiku wakati wa  harambee ya kuchangia waathirika wa tetemeko hilo, ambalo limeleta maafa makubwa na uharibifu wa miundombinu.

Alisema wananchi wanaoishi nje ya Kagera, licha ya kuwa na uwezo mkubwa wameutelekeza mkoa huo, jambo ambalo linatishia ustawi na maendeleo yao.

Kwa takwimu za kiuchumi, mkoa huo hivi sasa ni miongoni mwa mikoa mitano masikini nchini.

“Hii ni aibu ndugu zangu, ni jambo la kushtua  wenyeji nje ya Kagera hawana habari na kinachoendelea, janga litufumbue macho mkoa wetu unakwenda na maji. Tuache kubweteka tujipange upya, Serikali haiwezi kututoa hapa tulipo bila sisi kuweka nguvu ya ziada.

“Kwa mfano, hili tetemeko ni janga ambalo halikutarajiwa, wenzetu hawaonyeshi response (kuwajibika) yoyote ya kuguswa na hili tukio, wanadhani Serikali ndiyo itamaliza matatizo yote.

“Tabia hii imeanza kuota mizizi katika miaka ya karibuni imetuondoa wana Kagera katika mstari, wengine wanadhani tunafanya siasa katika mambo kama haya ya kibinadamu.

“Juzi iliitishwa harambee iliyoongozwa na Rais mstaafu mzee Mwinyi (Ali Hassan),watu wa Kagera hawakujitokeza wakati suala hili lilikuwa letu,” alisema.

Kuhusu madhara ya tetemeko, mbunge huyo alisema jambo la kusikitisha hadi sasa hakuna msaada wowote uliokwishatolewa kwa waathirika hao.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles