Bombardier iliyokuwa imeshikiliwa Canada kuwasili leo

0
607

BENJAMIN MASESE-MWANZA

RAIS  Dk. John Magufuli leo atawaongoza Watanzania  kuipokea ndege  ya ATCL  aina ya Bombardier Q400 katika Uwanja wa Kimataifa wa Mwanza baada ya kuachiwa nchini Canada iliposhikiliwa baada ya kutengenezwa.

Akizungumza jana jijini Mwanza, Mkuu wa Mkoa huo, John Mongella alisema  tayari ndege hiyo imeachiliwa nchini Canada na imeanza safari kuja Tanzania  ambapo  itawasili saa nane mchana jijini Mwanza  leo na kupokelewa  na Rais Magufuli  na viongozi wengine wa kitaifa.

Mongella ambaye alichukua dakika nne kuzungumza huku akiwa ameambatana na  viongozi wa wizara ya Uchukuzi na ATCL, hawakutaka   kutoa nafasi  kwa waandishi wa habari kuuliza maswali huku akisema kila kitu kitaelezwa leo baada ya ndege kupokelewa uwanja wa ndege wa Mwanza.

“Kama mnakumbuka jana (juzi) Rais Magufuli akiwa anafungua semina ya wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) alitoa taarifa kuwa ndege yetu aina ya Bombardier Q400  iliyokuwa ikishikiliwa nchini Canada  imeachiwa, hivyo nipo hapa kuwaeleza kwamba tayari ndege hiyo imeanza kuja Tanzania.

“Naomba niwaambie wananchi wa Mwanza na mikoa jirani kwamba kesho (leo) saa nane mchana itawasili katika uwanja wa Mwanza na kupokelewa na Rais Magufuli na viongozi wengine wa kitaifa, wananchi tunaomba wafike pale  linapojengwa jengo la mizigo, maandalizi yamekamilika.

“Mambo yote yataelezwa hapo hapo kama mnavyoona hapa nimeambatana na viongozi wa wizara husika na wa ATCL ambao ndio wanasimamia shirika la ndege, hivyo wananchi wajitokeze kwa wingi kwani imenunuliwa kwa fedha zetu wenyewe, baaa ya kusema hivyo asanteni,”alisema kwa ufupi  na kunyanyuka na kuondoka huku waandishi wakipaza sauti  ya kutaka kuuliza maswali lakini Mongella akijibu kwamba maswali ya nini tena.

Juzi Rais Magufuli alisema ndege hiyo imeachiwa lakini hakufafanua iliachiwa lini na kwa makubaliano gani ambapo aliwataka Watanzania kujiandaa kuipokea jijini Mwanza kwa siku ambayo watatangaziwa.

Ndege hiyo ilikamatwa chini Canada hivi karibuni baada ya mkulima, Hermanus Steyn kuishtaki Tanzania   ikiwa ni mara ya pili kufungua mashtaka kama hayo.

 Agosti mwaka huu nchini Afrika Kusini ndege nyingine ya ATCL ilishikiliwa baada ya mkulima huyo kufungua kesi kwenye mahakama ya Afrika kusini.

Mkulima huyo  anadai  fidia ya dola  za Marekani milioni 33 ambapo shauri hilo  lilisababisha mahakama ya Jimbo la Gauteng kuzuia ndege ya Tanzania aina ya Airbus A220-300 kuondoka nchini Afrika Kusini.

Hata hivyo Serikali ya Tanzania ilimshinda mkulima huyo mahakamani katka ngazi ya rufaa na hatimaye Septemba 3, mwaka huu mahakama hiyo  iliamuru ndege hiyo kuachiliwa.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here