20.2 C
Dar es Salaam
Saturday, August 13, 2022

BoT wapewa meno kushughulikia matapeli sekta ndogo ya fedha

RAMADHAN HASSAN-DODOMA

WAZIRI wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango ameitaka Benki  Kuu ya Tanzania (BoT) kusimamia utapeli na michezo michafu ambayo inachezwa na watoa huduma ndogo za fedha nchini ambapo amedai amekuwa akipokea simu kila siku kutoka kwa watu wakimlalamikia kuibiwa kupitia huduma hizo.

Agizo hilo alilitoa jana jijini hapa wakati akizindua Mpango wa kutoa elimu ya sera na sheria ya huduma ndogo za fedha ambapo alisema licha ya Benki Kuu kuonesha imejizatiti lakini wanatakiwa kuushughulikia  utapeli na michezo michafu ambayo imekuwa ikichezwa na watoa huduma wa sekta ndogo ya  kifedha nchini.

“Rai yangu kwa Benki kuu mmesema mmejizatiti na mimi nasisitiza msimamie sekta hii kikamilifu ili huu utapeli na michezo michafu ambayo inachezwa na watoa huduma ndogo za fedha kwa upande mmoja lakini pia wapokea huduma kwa upande mwingine vikome.

“Hili mlisimamie kwa dhati kabisa, tumechoka na vilio wanaonipigia simu yaani wamenyanyasika wengine wameugua wengine wameuziwa mali wamepoteza maisha. Mmejizatiti ndio  lakini tatizo ni  kubwa Benki Kuu lazima muhakikishe mnatoa kipaumbele kusimamia sekta ya huduma za fedha,”alisema Dk Mpango.

Dk Mpango alisema matarajio yake ni kwamba utekelezaji wa mpango huo utaleta matokeo chanya ikiwa ni pamoja na kuimarika kwa usimamizi wa sekta ndogo ya kifedha chini ya BoT

“Kwa kufanya yote haya tutasaidia kuimarika kwa usimamizi wa sekta ndogo ya fedha chini ya BoT ili tuwe na fedha ya sekta iliyoendelevu na kupunguza umaskini,”alisema.

Dk Mpango alisema imani  yake ni kwamba watoa huduma wote wa sekta ya fedha watajisajili na kupokea leseni kutoka kwa mamlaka husika na kutekeleza matakwa yao kisheria wakati wote.

“Napenda kutoa rai mafunzo kama hayo yawe endelevu na yaende nchi nzima tumieni vyombo vya habari, tumieni sanaa na walimu waliostaafu ili tuwafikie wananchi wanyonge, kwa wingi,”alisema.

Katika hatua nyingine Dk  Mpango aliitaka BoT kuingia katika mfumo wa kidijital katika kuendesha shughuli zake kutokana na dunia kuingia katika uchumi wa teknolojia.

“Niwakumbushe kwamba tunaishi katika uchumi wa teknolojia ya habari na mawasiliano na sasa dunia inaenda kwa kasi sana kwenye uchumi wa digitali kwahiyo Benki Kuu ifuatilie mambo kupitia mitandao,”alisema Waziri huyo.

Kwa upande wake, Mwakilishi wa Benk Kuu, (BoT) Richard Wambali, alisema Mpango huo wa elimu kwa umma kuhusu sera, sheria na kanuni za huduma ndogo za fedha nchini, utaisaidia Benki Kuu na Serikali katika kuhakikisha kuna uelewa wa kutosha wa sera, sheria na kanuni.

“Kwa njia hii, jukumu la usimamizi wa sekta ndogo ya fedha nchini litatekelezwa kwa ufanisi. Elimu kwa umma itawezesha pia wadau kuyajua maudhui mapana ya sera, sheria na kanuni, itawasaidia wananchi kujua haki na wajibu wao kwa mujibu wa sheria na kanuni.

“Nitoe rai kwa watoa huduma kutumia muda wa miezi 12 iliyotolewa na sheria kuweka mifumo na taratibu za biashara kuendana na matakwa ya Sheria na Kanuni ili, ifikapo Oktoba 31, 2020, wawe wamekwishaomba na kupata leseni kutoka Benki Kuu au mamlaka zilizokasimishwa,”alisema.

Naye, Mkurugenzi wa Uendeshaji kutoka  Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT), Irine Mlola, alisema watahakikisha elimu hiyo inamfikia kila Mtanzania ili waweze kufaidika na huduma ndogo za kifedha.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,592FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles