29.2 C
Dar es Salaam
Friday, August 19, 2022

Boeing kuimarisha programu ya ndege zake

WASHINGTON DC, Marekani

KAMPUNI ya kutengeneza ndege nchini hapa, Boeing imesema itaimarisha programu ya ndege yake chapa 737 MAX 8 ambayo ni sawa na iliyoanguka juzi nchini Ethiopia na kusababisha vifo vya watu 157.

Taarifa ya kampuni hiyo imekuja zikiwa ni saa chache baada ya Shirika la Mamlaka ya Anga la Marekani (FAA), kutangaza kuwa litafanya mabadiliko ya muundo wa ndege hiyo ifikapo Aprili.

Hata hivyo, Boeing haijasema kama hatua hiyo inahusiana na ajali ya ndege ya Ethiopia iliyotokea Jumapili iliyopita.

Katika ajali hiyo watu wote 157 waliokuwa ndani ya ndege hiyo aina ya Boeing 737 MAX 8 iliyokuwa ikielekea Nairobi, Kenya walipoteza maisha.

 Kampuni ya Boeing tayari imeshatuma salamu za rambirambi kwa ndugu wa marehemu.

Kutokana na ajali ya ndege hiyo, mashirika mbalimbali ya ndege duniani yamesitisha kurusha ndege zake za Boeing 737 MAX 8 katika juhudi za kuimarisha hatua za usalama.

Mashirika hayo ni pamoja China, Indonesia, Brazil na Mexico.

Mbali na mashirika hayo, pia Ethiopian Airlines juzi iliamua kutorusha ndege zake za Boeing 737 Max 8 ikiwa ni mojawapo ya hatua za usalama kufuatia ajali hiyo.

Ingawa sababu halisi ya kuanguka ndege hiyo ambayo ni mpya bado haijulikani, shirika hilo lilieleza kuwa limeamua kutozirusha ndege nne zilizosalia za chapa hiyo hiyo hadi ufafanuzi zaidi utakapotolewa.

Akitangaza uamuzi huo, Meneja wa Ethiopian Airlines nchini Kenya, Yilma Goshu alisema wamechukua hatua hiyo kama tahadhari kiusalama wakati uchunguzi ukiendelea.

“Ninapendelea kukuarifuni mapya. Tumeamua kutozirusha ndege zote za Boeing 737 Max 8 zilizokuwa zikitumiwa na shirika la ndege la Ethiopia na ambazo zinahusika na ajali hiyo ikiwa ni hatua mojawapo ya usalama.

“Lakini haimaanishi kwamba ajali hiyo ina mafungamano ya aina yoyote na ndege hizo. Tumeamua kuchukua hatua hizo za ziada kama tahadhari ili uchunguzi uweze kuendelea,” alieleza meneja huyo.

Shirika la ndege la Ethiopian Airlines limekuwa likitumia ndege tano za aina ya  Boeing 737 Max 8 na limekuwa likisubiri nyingine 25 ambazo tayari zimeshaagizwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,987FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles