30.2 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Bouteflika akubali yaishe, kutogombea tena urais

ALGERS, ALGERIA

RAIS Abdelaziz Bouteflika ametangaza kwamba hatogombea tena urais kwa muhula wa tano kwa lengo la kumaliza maandamano ya wiki kadhaa kuipinga hatua yake hiyo.

Katika barua yake iliyosomwa kupitia televisheni ya taifa – APS, Bouteflika ameapa kwamba hatogombea tena uchaguzi wa urais, baada ya kuitawala nchi hiyo kwa miaka 20.

Aidha ameahirisha uchaguzi mkuu uliokuwa ufanyike Aprili 18 na anakusudia kufanya mageuzi kadhaa katika mfumo wa kisiasa na katiba nchini hapa.

Katika taarifa yake hiyo, Bouteflika alieleza kwamba ameufikia uamuzi huo ili kufanya marekebisho katika Serikali yake haraka iwezekanavyo na kwamba mabadiliko hayo yanatokana na madai ya wananchi wa Algeria.

Alibainisha kuwa ataunda jopo ambalo litapanga tarehe mpya ya uchaguzi wa urais.

Baada ya taarifa hiyo, maelfu ya wananchi walijitokeza mitaani kushangilia, honi za magari zilikuwa zikisikika barabarani kwenye maeneo ya kati ya miji nchini hapa, huku baadhi ya Waalgeria wakipeperusha bendera za taifa.

Taarifa zinaeleza kuwa polisi hawakuonekana mitaani wakati wa shamrashamra hizo.

Katika kipindi cha wiki mbili zilizopita nchi hii imekumbwa na maandamano ya kuipinga hatua ya Rais Bouteflika mwenye umri wa miaka 82 kugombea urais.

Aidha, waandamanaji hao kwa muda mrefu wamelalamikia matatizo ya rushwa pamoja na sera mbaya za kiusalama.

Kiongozi huyo amekuwa akionekana hadharani kwa nadra tangu alipougua kiharusi mwaka 2013, na alirejea Algeria Jumapili jioni baada ya kupatiwa matibabu yaliyosemekana kuwa ni ya kawaida mjini Geneva, Uswisi.

Wakati hayo yanajiri, Waziri Mkuu, Ahmed Ouyahia alitangaza kujiuzulu wadhifa wake na rais alisema kuwa yatafanyika mabadiliko kadhaa katika baraza lake la mawaziri.

Hata hivyo, nafasi ya Waziri Mkuu imezibwa na Noureddine Bedoui, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani na amepewa jukumu la kuunda Serikali mpya katika taifa hili la Afrika ya Kaskazini.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles