24.8 C
Dar es Salaam
Saturday, April 27, 2024

Contact us: [email protected]

Bodi ya Nishati Vijijini yaahidi makubwa Msomera

Na Veronica Simba, REA – Handeni

Bodi ya Nishati Vijijini (REB) imefanya ziara Msomera, wilayani Handeni yaliko makazi mapya ya wananchi wanaoendelea kuhamia kwa hiari kutoka Hifadhi ya Taifa Ngorongoro, ambapo ahadi kutoka pande mbalimbali zimetolewa katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa ipasavyo.

Mwenyekiti wa Bodi, Balozi Meja Jenerali Mstaafu Jacob Kingu, aliyeongoza Msafara huo Machi 26, 2024 ameahidi kuwa Wakala wa Nishati Vijijini (REA) unaosimamiwa na Bodi hiyo, utatekeleza kikamilifu, jukumu lake la kupeleka nishati ya umeme kwa wakazi wa eneo hilo ambalo hadi sasa linaendelea vizuri.

Sehemu ya miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Msomera.

“Wakandarasi wetu wako eneo la kazi na tutahakikisha tunatekeleza kikamilifu kazi yetu kana ilivyokusudiwa,” amesisitiza.

Aidha, Balozi Kingu amesema jambo la msingi linalopaswa kuzingatiwa na wadau wote wanaohusika katika zoezi hilo ni ushirikiano ili azma ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Samia Suluhu Hassan iweze kutimia.

“Sote tushirikiane na sote tupeane taarifa kwa wakati. Naamini itawezekana iwapo sote tutaunganisha nguvu kwa pamoja,” amesema.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu pamoja na Wajumbe Bodi hiyo wakimsikiliza Kaimu Operesheni Kamanda wa ujenzi wa nyumba katika Kijiji cha Msomera, Luteni Kanali Edward Mwanga kuhusu maendeleo ya mradi huo wakati wa ziara ya Bodi pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) walipotembelea kukagua usambazaji wa miundombinu ya umeme katika Kijiji hicho wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga, Machi 26, 2024.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Albert Msando ameahidi kuwa yeye pamoja na viongozi wenzake watahakikisha vifaa vyote vinavyotumika katika kutekeleza Mradi wa upelekaji umeme katika eneo hilo vinabaki salama.

Amesisitiza kuwa, hawataruhusu wala hawatakuwa tayari kuona kifaa chochote kikipotea au kutumika vibaya huku akitolea mfano tukio lililotokea siku chache zilizopita ambapo alisema baadhi ya watu waliojaribu kuiba vifaa vya Mradi walikamatwa na wanaendelea kushikiliwa na vyombo vya ulinzi na usalama.

“Nimemwelekeza Mwendesha Mashtaka pamoja na OCD kwamba tutaifishe Gari na kuchukua hatua za kisheria kwa yeyote aliyehusika na tukio hilo ili iwe fundisho kwamba vifaa vinavyokuja kwenye miradi ya umeme usithubutu kugusa,” amesema.

Msando ameiahidi Bodi ya Nishati Vijijini kuwa endapo watajitokeza watu kushirikiana na wahalifu wa aina hiyo, Ofisi yake haitasita kuwachukulia hatua ili malengo ya REA na Bodi yaweze kufikiwa.

Naye Kaimu Kamanda wa Operesheni, Luteni Kanali Edward Mwanga, pamoja na kupongeza kazi nzuri inayofanywa na REA katika kupeleka umeme eneo hilo, pia ameiahidi Bodi kuendelea kutoa ushirikiano katika kuhakikisha miradi ya umeme inatekelezwa kikamilifu.

Mwenyekiti wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Balozi Meja Jenerali Mstaafu, Jacob Kingu akizungumza mara baada ya kukagua miundombinu ya umeme katika Kijiji cha Msomera wilayani Handeni, Mkoa wa Tanga wakati wa ziara ya Bodi hiyo pamoja na Menejimenti ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA) kukagua maendeleo ya usambazi umeme katika kijiji hicho. Tukio hilo limefanyika, Machi 26, 2024.

Katika pongezi zake, ametoa shukrani kwa REA kufikisha umeme eneo la kuzalishia tofali ambapo ameeleza kuwa imesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama za uendeshaji zilizokuwa zinatokana na matumizi ya jenereta.

“Tunapofyatua tofali kwa kutumia jenereta, gharama zinakuwa kubwa sana, hivyo kuwepo kwa umeme kumepunguza gharama za Mradi,” amefafanua.

Wakala wa Nishati Vijijini imekuwa ikitekeleza Mradi wa REA Awamu ya Tatu Mzunguko wa Pili katika kijiji cha Msomera ambapo ujenzi wa Mradi umekamilika kwa asilimia 100 kwa wigo wa awali na jumla ya sh bilioni 3.7 zimetumika kugharamia Mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu.

Aidha, usambazaji wa umeme Awamu ya Pili ya ujenzi wa nyumba 5,000 Msomera umekamilika kwa asilimia 100 katika hatua ya kwanza inayohusu kupeleka umeme wa msongo wa kati (kilovoti 33) kwa umbali wa kilomita 12.9 eneo la Kitalu F ambapo matayarisho ya vifaa vya ujenzi kama vile kufyatua tofali na utengenezaji wa vifaa vya chuma yatakuwa yakifanyika. Kazi hii imetekelezwa kwa gharama ya sh bilioni 6.5

Moja ya nyumba iliyowekwa umeme katika Kijiji cha Msomera.

Mkandarasi M/S China Railway Construction and Electrification Bureau Group Company Ltd atatekeleza Mradi huu kwa gharama ya sh bilioni 14.2

Bodi ya Nishati Vijijini iko mkoani Tanga kushiriki vikao kazi na hivyo inatumia fursa hiyo pia kutembelea baadhi ya miradi ya nishati vijijini inayotekelezwa mkoani humo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles