24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BOA KUPITIA WEZESHA YATOA MIKOPO YA NYUMBA

Na Mwandishi Wetu


BENKI ya Afrika (BOA) imeipongeza Serikali kwa hatua yake ya kusaidia upatikanaji wa hati za viwanja nchini, hatua iliyorahisisha upatikanaji wa mikopo ya ujenzi kutokea benki hiyo.

Hayo yalisemwa na Meneja Masoko Utafiti na Maendeleo wa benki hiyo, Muganyizi Bisheko, wakati akizungumza kwenye kipindi cha East Africa Drive kinachorushwa na Kituo cha Radio cha EATV.

Bisheko alisema kwa sasa benki hiyo inaona kuwa hatua hiyo ya Serikali ya Rais John Magufuli ni muhimu katika kuinua maisha ya wananchi ambao wamerahisishiwa mikopo hiyo.

“Benki imeguswa na hatua ya Serikali katika kuhakikisha kila mwananchi mwenye kiwanja anapewa hati yake kwa wakati na kuhakikisha kuwa hati hizo zinatumiwa kama dhamana na hiyo ni hatua kubwa yenye tija kwetu kama benki kwa kuwa kwa sasa wananchi wanaweza kukopeshwa mikopo ya nyumba,” alisema Bisheko.

Hivi karibuni Benki ya BOA ilizindua aina mpya ya mkopo wa ujenzi wa nyumba unaoitwa ‘Wezesha’ ambapo mtu anaweza kukopa kiasi cha Sh milioni 40 hadi 500 kwa mrejesho wa miaka hadi 25 bila utaratibu wa kutoa malipo yoyote ya awali.

Naibu Mkurugenzi wa BOA, Wasia Mushi, aliizungumzia zaidi mikopo hiyo kwa kusema: “Programu hii ya mkopo wa ujenzi wa makazi mapya unawapa uwezo wateja wetu kubuni nyumba zao kadiri wanavyopenda, kulingana na mahitaji yao na ndani ya bajeti zao.

“Kwa kiwango kidogo kabisa cha riba na katika viwango vya punguzo, pia imetengeneza mazingira rafiki na kuondoa usumbufu kwa mteja pindi anapohitaji mkopo huu.”

Aidha, huduma ya mkopo ya ‘Wezesha’ inapatikana kwa watu wote wenye mishahara katika sekta za umma na binafsi na kwa kutoa muda wa miaka 25 ya kulipa deni, mkopaji atapata uhuru zaidi pindi atakapochukua mkopo.

Mpango huu wa ‘Wezesha’, unalenga kutoa suluhu kwa changamoto za makazi zinazowakabili Watanzania wengi ambao kwa mazingira ya kawaida hutumia zaidi ya miaka 10-15 kujenga nyumba ya kawaida ya kuishi. Wakati mwingine huwa haziishi kabisa.

Fursa hii ya kutatua changamoto ya makazi kwa Watanzania wengi, inaendana na ongezeko kubwa la watu kupata ardhi iliyopimwa, hivyo kuwapa watu nafasi ya kujenga nyumba wanazozitaka kwa masharti nafuu na rahisi ambapo kwa kuanzia mteja atatakiwa kuwa na kiwanja ambacho nyumba hiyo itajengwa.

Kwa mujibu wa takwimu, Tanzania ina uhaba wa nyumba kwa ajili ya makazi zaidi ya milioni tatu. Huku kukiwa na ongezeko la uhitaji huo kwa zaidi ya asilimia moja kila mwezi.

Muganyizi Bisheko, Meneja Masoko Utafiti na Maendeleo wa BOA, alisema: “Benki inatoa asilimia 100 ya ufadhili wa ujenzi ili watu wengi waweze kuumudu mkopo. Mara nyingi, hasa kwa mtu anayeanza maisha, kujiwekea akiba na kupata kiwango cha kulipia gharama za ujenzi wa makazi ni jambo gumu sana. Jambo hilo liliwezekana kwa wale wenye kipato kikubwa na endelevu, lakini kwa sasa na kwa uwepo wa Wezesha, si jambo gumu tena la kuchelewesha ndoto zako za kumiliki makazi ya kuishi, kwa kuweka akiba kwa miaka 2-5.”

Aliongeza: “Mara mteja wetu anapopata mkopo wa makazi, yeye ndiye atakayechagua mkandarasi wa kujenga nyumba yake miongoni mwa makandarasi waliochaguliwa na BOA. Mkopo utatolewa kulingana na hatua za ujenzi, kama vile msingi, boma, paa na umaliziaji. Na fedha hizo zitapelekwa kwenye akaunti ya mkandarasi anayejenga iliyofunguliwa kwenye Benki ya Afrika. Baada ya kukamilisha ujenzi, ripoti ya mkaguzi wa ubora itakabidhiwa kabla ya fedha za hatua nyingine ya mkopo kutolewa.”

Kwa mara ya kwanza benki hiyo ilizindua mkopo wa nyumba mwaka 2011 ambao ulikuwa unajumuisha mkopo wa ununuzi wa nyumba pamoja na uboreshaji wa nyumba.

“Pamoja na mikopo ya nyumba, benki pia imekuwa ikitoa mikopo kwa wakandarasi wa ujenzi ili kuongeza upatikanaji wa nyumba bora za makazi na wakati huo huo wakiwezesha watu wa kawaida kuzinunua nyumba hizo,” anasema Bisheko.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles