24.8 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Biashara ya madini ifanyike kwenye masoko siyo hotelini- Samia

Na Brighiter Masaki, Dar es Salaam

Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, leo amefungua Kongamano la kimataifa la Uwekezaji katika Sekta ya Madini lenye lengo la kutangaza fursa za Uwekezaji katika Sekta za Madini ziliopo Nchini.

Akizungumza mapema leo Februari 22, jijini Dar es Salaam, wakati wa ufunguzi wa Kongamano la Kimataifa la uwekezaji katika sekta ya madini Samia amesema lengo ni kutangaza fursa na kuwaunganisha pamoja Wachimbaji na watoa huduma kwenye Shughuli mbalimbali zinazofanyika Migodini.

Kongamano hilo la siku tatu lenye kauli mbiu “Sekta ya Madini kwa Uchumi Imara na Maendeleo Endelevu” limefunguliwa katika Kituo cha mikutano cha Kimataifa cha Mwalimu Nyerere JNICC Jijini Dar es Salaam.

“Rais Dk. John Magufuli ni Baba wa madini kwa sababu kupitia kwake tumefaidika na rasilimali zetu ambazo zamani zilitoroshwa na kuipotezea Serikali mapato na kuiacha nchi kwenye dimbwi kubwa la umasikini,” amesema Samia.

Amesema Mkutano wa Kimataifa wa Uwekezaji katika Sekta ya Madini Tanzania ni wa muhimu kwani unaikutanisha Serikali na wadau wa sekta hiyo pia, ni jukwaa la kuujulisha ulimwengu kuhusu fursa za uwekezaji tulizonazo katika sekta hii.

“Mkutano huu unafanyika kipindi ambacho dunia inakabiliwa na janga la ugonjwa wa corona, ni wakati mgumu sana kwa mataifa mbalimbali ila ndani ya nchi yetu tumeendelea kumuomba Mungu huku tukiendelea na jitihada za kuchukua tahadhari zote zinazoelekezwa na Wizara husika ya Afya.

“Serikali yetu inawakaribisha wadau kuendelea kuwekeza nchini, katika sekta ya madini bado sehemu nyingi za nchi yetu zina hazina kubwa ya madini ambayo hayajaguswa hivyo, kupitia Serikali tunaweza kujenga ubia wa pamoja na wawekezaji katika kufanya biashara hiyo.

“Sekta ya madini inapitia changamoto kutokana na janga la Corona linaloitikisa Dunia lakini Tanzania imeendelea kuwa miongoni mwa nchi tano za wazalishaji wakubwa wa dhahabu barani Afrika,” amesema Samia.

Ameongeza kuwa; “Sekta ya madini inaendelea kukua, kufikia mwaka 2025 tunatarajia sekta ya madini itatoa mchango unaofikia asilimia 10 katika Pato la Taifa. Aidha, Mwaka wa Fedha 2020/21,

“Wizara ya Madini imepangiwa kukusanya Sh bilioni 526.7 ambapo katika kipindi cha Julai, 2020 hadi Januari, 2021 Wizara hiyo imeshakusanya Sh bilioni 360.74.

“Rais Dk. Magufuli ametoa fursa ya kuchimba madini na kufanya biashara, tuitumie fursa hii kwa uaminifu na kuhakikisha wote tunanufaika na sekta hii, wale ambao ni wachache wanaotaka kuturudisha nyuma tutashughulika nao kwani tunatamani sekta hii iwe rafiki na ifanyike kwa uwazi ili kila aliyewekeza aione faida.

“Yapo matukio ya utoroshaji wa madini yanayoendelea nchini, nalaani matukio haya. Nawaomba wachimbaji wote tuache utoroshaji na badala yake tuangalie mbele kwa sababu hakuna kitu ambacho mchimbaji alikihitaji akakikosa.

“Nawaomba wanaotaka kuleta madini kutoka nchi mbalimbali kuwa tuna masoko yanayofanya biashara hiyo hivyo wafanye biashara kupitia masoko hayo na sio kukutana hotelini,” amesema Samia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles