Benki ya kilimo kuviwezesha vyama vya ushirika kuanzisha viwanda

0
613

Derick Milton, Simiyu

Benki ya Maendeleo ya Kilimo Nchini (TADB), imesema ipo tayari kuviwezesha vyama vikuu na vyama vya msingi katika zao la Pamba (Amcos) ili viweze kuazisha viwanda vidogo na vikubwa vya kuchambua zao hilo na kuongeza nyororo wa thamani.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki hiyo Japhet Jastine, kwenye kikao cha kujadili jinsi gani ya kuongeza thamani kwenye zao la pamba kilichoandaliwa na mfuko wa kuendeleza sekta ya fedha Tanzania (FSDP) na kukutanisha sekta mbalimbali za kifedha.

“Tunataka hivi vyama vya ushirika kuviwezesha ili viweze kuwa na uwezo wa kuanzisha viwanda vikubwa na vidogo vya kuchambua pamba, wawe na uwezo wa kuchambua, kupata pamba mbegu, kuzalisha mafuta ambapo wataajiri watu wengi kupitia viwanda hivyo vidogo lakini wakulima wataweza kunufaika moja kwa moja,” amesema.

“Leo hii mkulima anauza pamba Sh 1200 kwa kilo moja, lakini anayechambua pamba anauza pamba nyuzi, mbegu, mafuta na mashudu sasa hapo mkulima hanufaiki na zao lake anaendelea kunyonywa tu, tunataka hizi Amcos zikijengewa uwezo zianzishe hivi viwanda uko walipo wakulima vijijini, waongeze ajira lakini pia mkulima anufaike na pamba yao kwa uwepo wa kiwanda kijijini kwake ambacho kinachambua, kuzalisha mbegu, mafuta na mashudu,” aliongeza Jastine.

Amesema kuwa benki hiyo imeona fursa hiyo na wako tayari kusaidia vyama hivyo ili viwe na viwanda vyake vidogo na vikubwa kwenye maeneo yao vijijini kwa wakulima, huku pia akihaidi kusaidia kujengwa kwa maghala makubwa ya kisasa ya kuweza kuhifadhi pamba iliyochambuliwa kwa ajiri ya kuitafutia soko.

“ Lakini ili tuweze kufanikisha haya yote lazima tuvijengee uwezo hivi vyama vya msingi (Amcos) na vyama vikuu viwe himara, bila kuvibadilisha kuwa vyama vya kibiashara hatuwezi kufanikiwa hata kidogo, lazima vibadilike viwe vyama vya kibiashara, tunataka sasa kufanya hata hilo kuvibadilisha mtazamo na utendaji kazi wake, viwe vya kibiashara zaidi,” amesema Jastine.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here