26 C
Dar es Salaam
Monday, January 17, 2022

BANDA ASIMAMISHWA, SHAURI LA SIMBA LAPIGWA KALENDA

Na JENNIFER ULLEMBO-DAR ES SALAAM


BEKI wa timu ya soka ya Simba, Abdi Banda, amesimamishwa kucheza mechi za Ligi Kuu Tanzania Bara, hadi hapo Kamati ya Nidhamu ya Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) itakapotoa uamuzi  mapema wiki hii.

Uamuzi huo ulitolewa Ijumaa iliyopita baada ya kufanyika kikao cha Kamati ya saa 72 ya Uendeshaji na Usimalizi wa ligi, ili kusubiri suala lake la kumpiga ngumi kiungo wa Kagera Sugar, George Kavilla, kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF. 

Kagera iliandika barua ya malalamiko kwa kamati hiyo ikidai kuwa Banda alionyesha utovu wa nidhamu kwa kumpiga ngumi Kavilla wakati akiwa hana mpira katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara uliochezwa Aprili 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Kaitaba mjini Bukoba.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana na Ofisa Habari wa TFF, Alfred Lucas, ilieleza kuwa Banda alifanya kitendo hicho katika mchezo dhidi ya Kagera Sugar ambao waamuzi hawakukiona, hivyo uamuzi wa kumsimamisha umezingatia Kanuni ya 9(5) ya Ligi Kuu.

Pia kamati hiyo imebaini kuwa Banda alifanya kitendo kama hicho katika mechi namba 169 kati ya Simba na Yanga iliyochezwa Februari 25, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

“Klabu ya Kagera iliwasilisha barua ya malalamiko dhidi ya kitendo cha beki huyo wa Simba cha kumpiga ngumi Kavilla wakati akiwa hana mpira ambapo mwamuzi wa mchezo huo hakuchukua hatua yoyote.

“Kosa hilo ni la kinidhamu, hivyo kamati imemsimamisha Banda kwa mujibu wa Kanuni ya 9(5) wakati akisubiri suala lake kusikilizwa na kutolewa uamuzi na Kamati ya Nidhamu ya TFF, ambapo kamati hiyo inatarajia kukutana wakati wowote wiki ijayo,” ilieleza taarifa hiyo.

Mbali na kamati hiyo kumsimamisha Banda, pia imeahirisha shauri la klabu ya Simba juu ya malalamiko ya kutaka kupewa ushindi wa pointi tatu na mabao matatu kutokana na timu ya Kagera  kumchezesha mchezaji Mohamed Fakhi katika mchezo huo wakati akiwa na kadi tatu za njano.

Shauri la Simba limeahirishwa hadi Aprili 13, mwaka huu kwa sababu kamati bado inafuatilia baadhi ya vielelezo vinavyohusu malalamiko hayo kabla ya kufanya uamuzi.

 

Katika hatua nyingine, Kamati ya saa 72 imeagiza suala la daktari Abel Kimuntu kukataa kuwasilisha taarifa yake kuhusu tuhuma za kupulizwa dawa kwenye chumba cha kubadilishia nguo kwa wachezaji wa Majimaji katika mechi namba 170 ya Ligi Kuu dhidi ya Stand United lipelekwe kwenye Kamati ya Nidhamu.

Suala hilo limepelekwa Kamati ya Nidhamu ya TFF ili hatua za kinidhamu dhidi yake zichukuliwe kwa kushindwa kutoa ushirikiano kwa mwendeshaji wa ligi juu ya jambo hilo.

Wakati huo huo, kamati hiyo imeagiza klabu ya Yanga iandikiwe barua ya onyo na kutakiwa kuhakikisha wanachama wake wanaacha  mtindo wa kumwaga maji vyumbani.

“Yanga hawakuingia vyumbani katika mchezo wa dhidi ya Azam FC kutokana na maji yaliyokuwa yamemwagwa na wanachama wa klabu hiyo (makomandoo) muda mfupi kabla ya timu kuwasili uwanjani,” ilieleza taarifa hiyo.

Pia kamati hiyo imeagiza kituo cha Songea kilichopo Uwanja wa Majimaji kuandikiwa barua ya onyo ili kuhakikisha vurugu hazitokei kwa mara nyingine uwanjani hapo.

Onyo hilo limetolewa kutokana na timu ya Toto Africans kufanyiwa fujo na viongozi wake wawili kuumizwa wakati wakiwa njiani kurejea hotelini, baada ya  kumalizika kwa mchezo wao wa ligi kuu dhidi ya Majimaji.

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
174,717FollowersFollow
531,000SubscribersSubscribe

Latest Articles