24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

MWAMBUSI: WASHAMBULIAJI WALIKOSA UTULIVU

Na THERESIA GASPER-DAR ES SALAAM


KOCHA msaidizi wa Yanga, Juma Mwambusi, amesema washambuliaji wa timu hiyo walikosa utulivu wa kitikisa nyavu katika mchezo wao wa awali wa Kombe la Shirikisho barani Afrika dhidi ya MC Alger ya Algeria, hali iliyosababisha kukosekana kwa mabao mengi.

Yanga ilicheza nyumbani juzi katika dimba la Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam na ilifanikiwa kuibuka na ushindi wa bao 1-0, uliowaweka katika wakati mgumu wa kusonga na kuingia hatua ya makundi.

Bao pekee lililowapa ushindi mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara mbele ya Waarabu, lilipachikwa wavuni na kiungo Thaban Kamusoko.

Mwambusi alizungumza hayo juzi baada ya kumalizika kwa pambano hilo, huku akielezea nafasi sita za kufunga walizotengeneza na kuambulia bao moja ambalo litawapa wakati mgumu watakapocheza ugenini mchezo wa marudiano.

“Tulitawala mchezo kwa kikubwa lakini washambuliaji walikosa umakini katika ufungaji ambapo walipoteza nafasi nyingi tulizotengeza, tukiwa wenyeji tulikuwa na uwezo wa kufunga idadi kubwa ya mabao kulingana na nafasi tulizopata,” alisema Mwambusi.

Alisema kutokana na matokeo waliyoyapata, watakuwa na kibarua kigumu ugenini watakaporudiana na MC Alger, hivyo watalazimika kuongeza umakini ili kupata matokeo mazuri na kuingia hatua ya makundi.

Aidha, Mwambusi aliongeza kuwa wapinzani wao walikuwa na malengo ya kupata sare au bao la ugenini lakini mipango yao haikufanikiwa baada ya kuwadhibiti kutokana na kuwasoma mbinu zao kabla ya kukutana.

“Kiwango na uwezo walioonyesha MC Alger ni wa chini tofauti na tulivyowaona, hivyo itatubidi tuanze kuandaa mbinu za kujihami mapema kabla ya kwenda kucheza nao ugenini,” alisema.

Alisema wapinzani wao wanaweza kubadilika katika mchezo wa marudiano na kuwapa wakati mgumu, hivyo lazima wajipange upya kwani wachezaji waliokuwa majeruhi tayari wamerejea kikosini kuongezea nguvu.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles