25.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

BALOZI SEFUE ATEULIWA JOPO LA WATU MASHUHURI

Na Mwandishi Maalumu- Addis Ababa


MWANADIPLOMASIA mahiri nchini  ambaye pia aliwahi kuwa Katibu Kiongozi-Ikulu, Balozi Ombeni Sefue, ameteuliwa kuwa Mtanzania wa kwanza kuingia katika Jopo la Watu Mashuhuri katika Mpango wa Afrika Kujitathmini Katika Utawala Bora (APRM).

Kwa mujibu wa Katibu Mtendaji wa APRM tawi la Tanzania, Rehema Twalib anayehudhuria mikutano ya Umoja wa Afrika na APRM mjini Addis Ababa, Ethiopia, Balozi Sefue ameidhinishwa kwenye kikao cha juu ya Wakuu wa Nchi za Umoja wa Afrika ambao ni wanachama wa APRM, kilichofanyika juzi juzi.

“Haikuwa kazi rahisi kupata nafasi hii. Nchi nyingi za Afrika zilileta majina ya watu wao mashuhuri kuingia katika jopo hili muhimu. Balozi Sefue licha ya kuwa na utumishi uliotukuka kama mwanadiplomasia mkongwe pia aliungwa mkono kwa nguvu zote na Serikali ya Awamu ya Tano ya Tanzania,” alisema Katibu Mtendaji huyo.

APRM ni Mpango wa Afrika uliobuniwa na Wakuu wa Umoja wa Afrika kwa lengo la kuwa na chombo kitakachosaidia kuhimiza nchi wanachama kuenzi utawala bora na utoaji wa huduma bora za uchumi, biashara na za jamii kwa wananchi wao kupitia mfumo wa kujitathmini zenyewe na kukosoana.

Kwa mujibu wa tovuti ya APRM, Jopo la Watu Mashuhuri ni chombo cha juu cha kuwashauri wakuu wa nchi wanachama wa APRM katika uendeshaji wa mpango huo na husimamia mchakato mzima wa kujitathmini.

Wajumbe wa jopo hilo ambao hudumu kwa miaka minne hupendekezwa na nchi zao na baada ya mchakato mrefu wenye ushindani majina ya waliokidhi vigezo huwasilishwa na kuidhinishwa  na kikao cha juu katika APRM-Mkutano wa Wakuu wa Nchi na Serikali.

Tanzania ni miongoni mwa wanachama 35 kati ya nchi 54 wa Nchi za AU zilizojiunga na APRM na ilijiunga rasmi na mpango huo tangu mwaka 2004.   Tanzania ilikwisha kufanyiwa tathmini ya kwanza ya utawala bora na inaendelea kutekeleza mapendekezo yaliyotolewa.

Katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Wakuu wa Nchi za APRM, Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya aliwapongeza wajumbe wa jopo hilo na kuwataka kushiriki vema katika kuihuisha APRM na kuwa chombo chenye thamani kubwa kwa Afrika kama walivyotarajia waasisi wake kina Thabo Mbeki, Olusegun Obasanjo, Benjamin Mkapa na wengine.

Balozi Sefue ataungana na wajumbe wengine wapya ambao ni pamoja na Profesa Ibrahim Agboola Gambari (Nigeria), Balozi Mona Omar Attia (Misri)   Fatma Zohra Karadia (Algeria), Askofu Don Dinis Salomão Sengulane (Msumbiji) na Profesa Augustin Loada (Burkina Faso).

Wajumbe wa zamani wanaoendelea ni pamoja na  Profesa Youssouf Khayal (Chad) ambaye kwa sasa atakuwa Mwenyekiti wa Jopo hilo na Brigitte Mabandla (Afrika Kusini) ambaye atakuwa Makamu Mwenyekiti.

Mkutano huo pia ulijadili ripoti za tathmini za nchi katika maeneo ya utawala bora kwa nchi za Kenya (ikiwa ni ripoti ya pili kuwasilishwa), Sudan, Chad, Senegal, Djibouti pamoja na ripoti ya utekelezaji ya Zambia.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles