25.2 C
Dar es Salaam
Monday, August 15, 2022

Babu wa Loliondo aibuka tena

babuNa ABRAHAM GWANDU-ARUSHA

MCHUNGAJI mstaafu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Ambilikile Mwasapile maarufu kwa jina la Babu wa Loliondo, ameibuka tena upya mara hii si kwa kuwanywesha wananchi kikombe cha dawa bali ni baada ya kuwaongoza katika maandamano na kufunga barabara ili kushinikiza Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo, atatue mgogoro wa ardhi katika kijiji hicho.

Babu wa Loliondo aliyekuwa maarufu katika miaka ya nyuma kutokana na kutoa huduma ya dawa ya asili iliyodaiwa kutibu maradhi na wananchi wenzake walidai kuwa Diwani wa zamani wa Kata ya Samunge, Lemindi Njuda, ndiye aliyepora eneo la ardhi lililotengwa kwa ajili ya ujenzi wa shule jambo linalowashangaza.

Huku wakiwa wamebeba mabango na majani mabichi wakiashiria maandamano ya amani, wananchi hao wakiongozwa na Babu wa Loliondo walizuia msafara huo juzi ili waweze kusikilizwa kilio chao cha muda mrefu kuhusu eneo hilo.

Pia walisema pamoja na uamuzi wa baraza la kata lililotoa uamuzi katika shauri lililofunguliwa Aprili, mwaka huu kuwa ardhi hiyo ni mali ya shule lakini Jeshi la Polisi Wilaya ya Ngorongoro limekuwa likimlinda na kumkingia kifua diwani huyo na kukataa kutekeleza amri iliyomtaka kuondoka katika eneo hilo la shule.

“Tumeporwa ardhi yetu mkuu wa mkoa tusaidie,” lilisomeka moja ya bango lililobebwa na wananchi hao.

Baada ya kusoma mabango hayo, Gambo, alimwagiza Mkuu wa Wilaya ya Ngorongoro, Rashid Taka, aende kusikiliza kilio cha wananchi hao lakini walikataliwa huku wakiendelea kumsihi ashuke kwenye gari na kuwasikiliza.

Akizungumza kwa niaba ya wananchi hao, Babu wa Loliondo, alisema amejitokeza na kuongoza maandamano hayo ili kuhakikisha shule inarudishiwa eneo lake lililoporwa.

“Dhuluma Mungu hapendi, hili ni eneo la shule lakini watu wenye fedha wamelipora, niko mstari wa mbele kulipigania ili watoto na wajukuu wapate eneo la kujengewa shule,” alisema Babu wa Loliondo.

Naye Mtendaji wa kata hiyo, Zakaria Antony, alisema eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 15 limeporwa na diwani huyo ambaye pia ni mkulima na  mfanyabiashara na kulitumia kwa kilimo cha migomba.

Antony alisema wananchi wanashindwa kufanya shughuli za maendeleo hususani ujenzi wa madarasa na nyumba za walimu kutokana na ufinyu wa eneo la shule.

Akijibu malalamiko ya wananchi hao, Gambo, aliwaagiza polisi kufuta mara moja nakala ya barua iliyoandikwa na Mkuu wa Kituo cha Polisi Loliondo kwa kuwa yeye hana mamlaka ya kufanya hivyo bali anapaswa kutekeleza amri ya mahakama ya baraza la kata na si vinginevyo.

“DC hakikisha wewe na OCD, kamati nzima ya ulinzi na usalama mnasimamia kikamilifu utekelezaji wa amri iliyotolewa na baraza la ardhi ili kuruhusu shughuli za maendeleo ya shule hiyo ziweze kufanyika bila vikwazo,” alisema Gambo.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
198,784FollowersFollow
550,000SubscribersSubscribe

Latest Articles