30.2 C
Dar es Salaam
Sunday, September 25, 2022

BABA WA BIBI HARUSI KUIKOSA HARUSI YA KIFALME UINGEREZA

LONDON, Uingereza


HARUSI ya mwanamfalme wa Uingereza Harry na mwigizaji maarufu wa Marekani, Meghan Markle imepata pigo baada ya baba ya bibi harusi kutangaza kutohudhuria hafla hiyo itakayofanyika kwenye Ukumbi wa Windsor Castle, Jumamosi wiki hii.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari nchini Marekani, Thomas Markle amesema hatahudhuria harusi hiyo ya kifalme akihofia kumuaibisha bintiye.

Markle alitangaza kutohudhuria harusi hiyo baada ya kukiuka masharti ya kutopigwa picha kabla ya harusi hiyo, kitendo ambacho kufichuka kwake kulimfedhehesha na kumsababishia maradhi ya mshtuko wa moyo.

Markle anaamini mkewe wa zamani waliyetengana, Doria Ragland ni chaguo bora la kumsindikiza bintiye kwenye harusi hiyo itakakayofanyika katika Kanisa la St. George, Windsor baada ya uamuzi wake wa kushtusha wa kutoenda Uingereza.

Meghan ameripotiwa kumsihi baba yake abadili uamuzi huo, lakini Markle (73) anataka kujichimbia Mexico kutafakari yaliyotokea.

Doria alitarajia kupanda ndege kuelekea Uingereza kutoka Los Angeles, Marekani jana ili kumsindikiza bintiye, akiwa kama chaguo mbadala la baba mtu.

“Huu ni wakati mgumu kwa Markle siku chache kabla ya harusi. Kamati ya Harusi ya Mwanamfalme Harry inaomba uvumilivu na heshima kwa Mzee Markle,” ilisema taarifa ya jumba la Kifalme.

Markle alikiuka wito wa Ofisi ya Malkia wa Uingereza wa kujiepusha na wapigapicha, ambao hawajaidhinishwa na kuhakikisha kuwa maandalizi yanafanyika kisiri.

Lakini Mzee huyo alijitokeza na kupigwa picha hadharani na mpigapicha asiyejulikana na kisha kuuza picha zake kwa Sh. milioni 100 kwa mujibu wa jarida la Daily Mirror.

Picha hizo zilionyesha Mzee Markle akipimwa suti ambayo angevalia siku ya harusi. Mzee huyo kwa sasa anahisi kuwa alitapeliwa.

Lakini pia baadhi ya jamaa za Markle wamezuiwa kuhudhuria hafla hiyo kutokana na kigezo kwamba ni walevi chakari na huenda wakazua rabsha.

Licha ya kukumbwa na masaibu hayo, mbwembwe za kukaribisha harusi hiyo zinaendelea kutanda kote duniani.
Nchini Kenya, Hoteli ya Windsor Golf inatoza ada ya Sh milioni moja ya Kenya sawa na Sh milioni 20 za Tanzania kwa wanandoa kwenda kutazama harusi hiyo kwenye runinga jijini Nairobi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
201,896FollowersFollow
553,000SubscribersSubscribe

Latest Articles