26.2 C
Dar es Salaam
Monday, October 3, 2022

WALIOUAWA PALESTINA WAFIKIA 61

GAZA, PALESTINA


IDADI ya watu waliouawa kwa kupigwa risasi na majeshi ya Israeli kwenye mpaka wa mashariki ya Ukanda wa Gaza, imeongezeka na kufikia watu 61 wakiwamo watoto wanane na majeruhi 2,771.

Mauaji hayo ya kikatili yametokea wakati Wapalestina wakiandamana kukumbuka miaka 70 ya Nakba, yaani janga lililowapata Wapalestina pamoja na kupinga kuhamishiwa kwa ubalozi wa Marekani mjini Yerusalemu.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, majeshi ya Israeli waliwafyatulia risasi nyingi za moto na mabomu ya machozi wananchi wa Palestina mpakani na Israel mashariki mwa Ukanda wa Gaza.

Katika majeruhi 2771, miongoni mwao 27 wako katika hali mbaya, 122 wakiwa watoto na wanawake 44 na wanahabari 11 pamoja na mtoa huduma mmoja, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Mamlaka ya Palestina.

Maelfu ya Wapalestina walishiriki maandamano hayo ya amani yakienda sambamba na uhamisho wa Ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv kwenda Yerusalem licha ya ghadhabu ya Palestina na kelele za jumuiya ya kimataifa kupinga hatua hiyo.

Wakati huo huo, Rais wa Palestina, Mahmoud Abbas jana alioongoza mkutano wa dharura mjini Ramallah akisema kilichotokea Yerusalemu juzi si ufunguzi wa ubalozi bali chimbuko la ulowezi wa Marekani.

Aidha, Abbas ametangaza kushusha bendera nusu mlingoti kwa muda wa siku tatu kuanzia juzi kwa ajili ya kuomboleza roho watu waliouwawa.

Abbas ameitangaza jana kuwa siku ya mgomo kukumbuka janga la miaka 70 tangu kuundwa kwa taifa la Israel kwa gharama ya Wapalestina.

Akizungumzia kilele cha kumbukumbu ya Nakba jana, Rais Abbas alisema, ‘Leo ni moja ya siku mbaya sana inayowapitia wananchi wetu, ambao kamwe hawataacha mapambano ya amani hadi ushindi, kwa kusimamisha dola yenye mji mkuu wake Yerusalemu.”

Baada ya mkutano huo, Katibu wa Kamati Kuu ya Jumuiya ya Ukombozi wa Palestina (PLO) Saeb Erekat aliwaambia wanahabari jana watasaini haraka mikataba ya kuiingiza dola ya Palestina katika mashirika kadhaa ya kimataifa.

Erekat ameongeza kuwa PLO itawasilisha haraka nyaraka za kisheria kwa Mahakama ya Kimataifa ya Jinai kuhusu vitendo vya Israel.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
202,573FollowersFollow
554,000SubscribersSubscribe

Latest Articles