TIMU ya soka ya Azam FC jana ilifanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA na kuzifuata Yanga na Yanga, baada ya kuifunga Panone FC mabao 2-1 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Ushirika, mjini Moshi.
Azam wameingia hatua hiyo na kuungana na nyingine zilizofuzu hatua hiyo za Yanga, Simba, Tanzania Prisons, Ndanda FC, Mwadui FC, Coastal Union na Geita Gold.
Katika mchezo wa jana Azam waliokuwa ugenini, walijikuta wakifungwa bao la kwanza na Panone dakika ya 48 kupitia kwa Godfrey Mbuda, aliyefunga kwa kichwa.
Azam, ambao walicheza kwa tabu kwenye uwanja huo ambao haukuwa na nyasi, walifanikiwa kusawazisha dakika ya 63 kupitia kwa beki wake wa kimataifa, Pascal Wawa, aliyeunganisha vyema mpira wa kona iliyochongwa na Erasto Nyoni.
Baada ya bao hilo, Azam walifanya mabadiliko kwa kuwatoa Ame Ally, Frank Domayo na Salum Abubakar ‘Sure Boy’ na nafasi zao kuchukuliwa na Kipre Tchetche, Jean Mugiraneza na Didier Kavumbagu, huku Panone ikimtoa Adam Soba na kumwingiza Said Salum.
Mabadiliko hayo yaliisaidia zaidi Azam na kuwawezesha kupata bao la pili dakika ya 77 kupitia kwa mshambuliaji Allan Wanga, aliyeunganisha kona iliyopigwa na Nyoni.
Azam ilifanikiwa kuingia hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la FA baada ya kuichapa African Lyon mabao 4-0.