NA MWANDISHI WETU, DAR ES SALAAM
BUNDI ni kama ameanza kuing’ang’ania klabu ya soka ya Simba, baada ya uongozi kutangaza kumsimamisha kwa muda usiojulikana nahodha msaidizi wa timu hiyo, Hassan Isihaka, kwa madai ya kuonyesha vitendo vya utovu wa nidhamu.
Mbali na sakata la kufungiwa kwa beki huyo wa kati, uongozi unapigana chini kwa chini kuhakikisa unanasa saini ya mlinzi wake wa kulia, Hassan Ramadhani ‘Kessy’, ambaye mkataba wake umemalizika na amekuwa akiwazungusha kwa kutaka kulipwa dau kubwa.
Kamati ya Utendaji ya klabu ya Simba jana ilitangaza uamuzi wa kumsimamisha Isihaka kutokana na kumtolea maneno yasiyo na staha kocha wa timu hiyo Mganda, Jackson Mayanja, kabla ya mchezo wa Kombe la FA dhidi ya Singida United, uliochezwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana, imeeleza kuwa kitendo hicho si cha kiungwana na kilifanywa mbele ya wachezaji wengine na kukiuka waraka wa maadili, ambapo licha ya kusimamishwa, kamati imeagiza beki huyo alipwe nusu mshahara kwa kipindi atakachokuwa anatumikia adhabu yake.
Aidha, kamati hiyo imewataka wachezaji wengine kuzingatia nidhamu na weledi katika kipindi chote watakapoitumikia Simba.
Inadaiwa kuwa Isihaka alitofautiana na Mayanja kutokana na kuwekwa benchi muda mrefu, lakini baadaye kocha alimweleza kuwa anataka apumzike kutokana na kucheza mechi nyingi.
Jambo la kushangaza ni kwamba beki huyo alipangwa kucheza dhidi ya Singida United juzi, kitendo ambacho hakutarajia na kumfanya aropoke kwa kutaka kujua kama muda aliotakiwa kupumzika umekwisha.
Kwa upande wa Kessy, inadaiwa kwamba amekuwa akizungushana uongozi wa Simba juu ya maslahi anayotaka, huku akisusa kujiunga na wenzake mazoezini, ikiwa ni pamoja na kambi ya Morogoro ambayo timu iliondoka jana.
Chanzo cha habari za uhakika ambazo zimelifikia MTANZANIA, kinaeleza kuwa awali Kessy alitaka alipwe dau la Sh milioni 30 kwa pamoja, lakini baada ya muda mfupi alibadili mawazo na kutaka kulipwa kiasi cha Sh milioni 60, jambo ambalo limewachanganya viongozi.
Hata hivyo, kikosi cha Simba kiliondoka jana kuelekea mkoani Morogoro ambako kitaweka kambi ya muda mfupi kujiandaa na mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Mbeya City, utakaofanyika Jumapili hii katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Simba iliondoka kwenda Morogoro ikiwa ni siku moja baada ya kufanikiwa kutinga hatua ya robo fainali ya michuano ya Kombe la FA, baada ya kuichapa Singida United mabao 5-1 katika mchezo uliopigwa juzi Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.
Kabla ya kuondoka, Mayanja aliliambia MTANZANIA kuwa kambi hiyo ni maalumu kwa ajili ya kujiimarisha zaidi kabla kukutana na Mbeya City, ambapo amepanga kuifanyia kazi kubwa safu ya ushambuliaji.
“Nitatumia muda mfupi uliobaki kuzisoma vizuri mbinu za wapinzani wetu ili tuweze kupanga mikakati kabambe ya kukabiliana nao, kwani hii itakuwa ni mara yangu ya kwanza kucheza nao tangu nianze kibarua cha kuinoa Simba,” alisema.
Habari za uhakika mbazo zimelifikia gazeti hili, zinadai kuwa Simba wameamua kuweka kambi Morogoro ili kuwakwepa mashabiki ambao bado wana hasira na baadhi ya wachezaji kutokana na kipigo walichopata cha mabao 2-0 dhidi ya watani wao wa jadi, Yanga.
Chanzo hicho kimeeleza kuwa Simba wanaogopa kelele za mashabiki zinaweza kuwaathiri kisaikolojia wachezaji wakati wakijiandaa na mchezo wao dhidi ya Mbeya City.
Chanzo hicho kilieleza kuwa, Simba hawajawahi kuweka kambi mkoani humo kujiandaa na mechi ya Ligi Kuu isipokuwa ile ya Yanga.