27.1 C
Dar es Salaam
Friday, March 29, 2024

Contact us: [email protected]

Yanga yafuata marashi ya ushindi Pemba

YANGA MAZOEZININA ADAM MKWEPU, DAR ES SALAAM

MABINGWA watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga, jana walirejea Pemba kuweka kambi ya muda mfupi kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wao dhidi ya Azam FC, baada ya kugundua siri ya ushindi visiwani humo.

Kwa mara ya pili mfululizo Yanga imekuwa ikiweka kambi yake Pemba na kufanikiwa kuwaliza mahasimu wao, Simba, mara ya kwanza ikiwa ni Septemba 26, mwaka jana waliposhinda mabao 2-0, kabla ya kutoa tena kipigo kama hicho Februari 20, mwaka huu.

Yanga, ambao ni vinara kwenye msimamo wa ligi, wakiongoza kwa kufikisha pointi 46 sawa na Azam kwa tofauti ya wastani wa mabao ya kufunga na kufungwa, watakutana na wapinzani wao katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Kwa mara zote Yanga wamekuwa wakiweka kambi yao ya siri katika hoteli ya kifahari ya Misali Beach Resort iliyopo Pemba na kuweka ulinzi mkali, huku wakifanya mazoezi Uwanja wa Gombani, visiwani humo.

Yanga wamepania kujiimarisha zaidi pamoja na kuwa ndiyo timu pekee yenye safu imara ya ulinzi Ligi Kuu, kutokana na mabeki wake kuruhusu kufungwa mabao machache ukilinganisha na timu nyingine zinazoshiriki ligi hiyo, wakiwemo Azam, ambao wamefungwa mara 11.

Kocha Mkuu wa Yanga Mholanzi, Hans van der Pluijm, anaonekana kuvutiwa zaidi na kambi ya Pemba kutokana na matokeo mazuri wanayopata, hasa wanapokutana na mahasimu wao, Simba, jambo linalozidi kumpa ujasiri wa kuwafunga Azam na kurahisisha mbio za ubingwa msimu huu.

Yanga, ambao pia ni wawakilishi wa Tanzania katika michuano ya Klabu Bingwa Afrika, wanajiandaa na mchezo wao wa raundi ya kwanza dhidi ya APR ya Rwanda, baada ya kufanikiwa kuiondosha Cercle de Joachim ya Mauritius kwa jumla ya mabao 3-0, ikiwa ni ushindi wa bao 1-0 ugenini na 2-0 nyumbani.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles