26.5 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 26, 2023

Contact us: [email protected]

Askofu: Sitta mchochezi

Samuel Sitta
Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba ambaye pia ni Waziri wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta

NORA DAMIAN, DAR ES SALAAM NA MAREGESI PAUL, DODOMA

MWENYEKITI mstaafu wa Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Askofu Dk. Peter Kitula, amesema kauli za kejeli zinazotolewa na Mwenyekiti wa Bunge Maalumu la Katiba, Samuel Sitta zimejaa uchochezi.

Sitta amekuwa akishutumiwa na watu mbalimbali kutokana na kauli zake anazozitoa pindi anapoendesha Bunge hilo.

Hivi karibuni, Sitta alisema wajumbe wanaounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) ni waigizaji na juzi alisikika akisema ‘Ukawa imekula kwao’.

Akizungumza na MTANZANIA jana, Askofu Kitula alisema Sitta anapaswa kuzungumza kwa utulivu na amani na aache kutoa kauli za uchochezi.

“Kauli za Sitta zimejaa uchochezi, azungumze kwa utulivu na amani. Sisi maaskofu hatuna mwelekeo wa chama chochote, lakini tunataka amani iwepo, aheshimu mawazo ya wajumbe na kutafuta mwafaka kwa amani,” alisema Askofu Kitula.

Pia askofu huyo alishauri Bunge hilo lisitishwe kwanza kwa sababu bila kuwapo ushirikiano wa wajumbe wengine itakuwa ni kazi bure.

Kuhusu kuendelea kushambuliwa kwa aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji mstaafu Joseph Warioba, Askofu Kitula alisema si sahihi na kwamba jaji huyo anadhalilishwa.

“Tulimwamini tukamkabidhi kazi hiyo, hata kama binadamu hawezi kuwa ‘perfect’ (mkamilifu) kwa taaluma yake, lakini huwezi kumdhalilisha kiasi hicho,” alisema.

Alisema kuendelea kumshambulia Jaji Warioba hakuleti sifa nzuri kwani yeye amefanya kama alivyoona.

Mjada wa sura za Katiba wahitimishwa kwa mipasho

Katika hatua nyingine, Bunge hilo limehitimisha mjadala wa Rasimu ya Katiba kwa kuwashambulia wajumbe wa Ukawa.

Pamoja na hayo, nusura mjadala huo uingie dosari baada ya Mbunge wa Nkasi Kaskazini, Ally Keissy Mohamed (CCM), kutaka kupigwa na wajumbe wanaotoka Zanzibar kwa kile kilichoelezwa kuwa aliwakejeli kwa maneno wakati alipokuwa akichangia rasimu hiyo.

Wakati wa mjadala huo juzi, wajumbe wengi walishindwa kujadili sura za rasimu ya Katiba na badala yake walitumia muda mwingi kuwajadili Ukawa kwa kile walichosema hawaridhishwi na mwenendo wa umoja huo.

Wajumbe hao waliwashambulia wenzao hao wakirejea mkutano mkuu wa Chadema uliohutubiwa mwishoni mwa wiki iliyopita na Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe.

Wakati wa mkutano huo, Mbowe aliwarushia maneno wajumbe wa Bunge hilo wanaoendelea kushiriki vikao vyake mjini Dodoma.

Pamoja na mambo mengine, wajumbe hao walionyesha kutoridhishwa na kauli ya Mbowe aliyewataka wananchi kuandamana nchi nzima ili kupinga mchakato wa Bunge hilo unaotarajiwa kuhitimishwa Oktoba 4.

Katika mchango wake juzi, mmoja wa wajumbe wa Bunge hilo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha UPDP, Fahmi Dovutwa, alisema kinachofanywa na Ukawa hakiwezi kuvumiliwa kwa kuwa wanakiuka sheria za nchi.

Kwa mujibu wa Dovutwa, Ukawa hawaridhiswi na mwenendo wa Bunge kwa kuwa Mwenyekiti wa Bunge hilo, Sitta, alikataa kuwapendelea.

Pamoja na hayo, Dovutwa alizungumzia suala la maandamano yaliyoitishwa na Mbowe na kuwataka viongozi wakuu wa Ukawa, wawe mstari wa mbele wakati wa maandamao hayo aliyoyaita ni haramu.

Mjadala juu ya Ukawa haukuishia kwa Dovutwa bali pia Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Asiye na Wizara Maalumu, Profesa Mark Mwandosya naye alijitosa kuwashambulia.

Katika mazungumzo yake, Profesa Mwandosya alisema kama kweli viongozi wa Ukawa ni wazalendo, watakapokuwa wakiandamana wawe mstari wa mbele kama ilivyo kwa Wajapani ambao hujiua kwa kujichoma kisu pindi wanaposhindwa kukubaliana na baadhi ya mambo.

Wengine waliowajadili Ukawa ni Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wazazi CCM, Abdallah Bulembo, Mbunge wa Mvomero, Amosi Makala, Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, George Simbachawene pamoja na Mbunge wa Mbinga Magharibi, Kapteni John Komba.

Pamoja na hoja hiyo kutikisa Bunge juzi, wakati mjadala unaanza wiki iliyopita, wajumbe wengi walizungumzia pia suala la elimu wanayotakiwa kuwa nayo wagombea wa ubunge.

Wakati wa mjadala huo, Mbunge wa Ngara, Deogratias Ntukamazina, alitaka Katiba ieleze kwamba wagombea ubunge wawe na elimu ya kuanzia kidato cha nne kwa vile majukumu yao ni mazito.

Kwa mujibu wa Ntukamazina, kitendo cha Katiba kuwaruhusu wagombea wanaojua kusoma na kuandika kinasababisha Bunge liwe na watu wenye uelewa mdogo kwa kuwa mtu mwenye elimu ndogo hana wigo mpana wa kuelewa mambo.

Hata hivyo, hoja hiyo ilipingwa na Mbunge wa Mtera, Livingston Lusinde, ambaye alisema elimu siyo kigezo cha uelewa kwa kuwa kuna wasomi wengi wanaoshindwa kumudu majukumu yao.

Hoja nyingine iliyotikisa mjadala wa rasimu hiyo ni suala la uraia pacha kwani baadhi ya wajumbe walitaka uraia huo uruhusiwe na wengine waliukataa kwa kuwa Watanzania hao walihamia nje ya nchi kwa kuwa walikimbia ugumu wa maisha.

Suala la Mahakama ya Kadhi nalo lilitikisa Bunge na wakati fulani kuwagawa wajumbe. Wakati wa mjadala wa hoja hiyo, Mbunge wa Tunduru Kaskazini, Abdallah Mtutura (CCM), aliwataka Waislamu waungane kuomba mahakama hiyo itambulike kikatiba kwa kuwa ni muhimu kwao.

Wakati mijadala hiyo ikishika kasi, wajumbe ambao ni wanawake hawakubaki nyuma kwani walitaka Katiba iruhusu wanawake na wanaume wawe na idadi sawa katika vyombo vya uamuzi.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. muda mwingi umetumika kuishambulia na kuikejeli ukawa yote mwenye wa BMK akiwa kinara?!?! hawaishi kubadili kanuni ili kufikia malengo yao ya kuinajisi rasimu ya tume ya jaji mstaafu. ubinafsi, ubinafsi x1000 umekithiri; eh Molla Tuokowe na janga hili

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,726FollowersFollow
574,000SubscribersSubscribe

Latest Articles