25 C
Dar es Salaam
Wednesday, April 24, 2024

Contact us: [email protected]

Kafulila: Tibaijuka achunguzwe mabilioni ya ITPL

Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka

PATRICIA KIMELEMETA NA SHABANI MATUTU, DAR ES SALAAM

MBUNGE wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi), ametaka viongozi wa Serikali, Bunge na Mahakama wanaotajwa kulipwa fedha za IPTL zilizokuwa kwenye Akaunti ya Escrow akiwamo Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Tibaijuka wahojiwe.

Alisema kuwa Profesa Tibaijuka ni mmoja wa viongozi wa Serikali ambaye amekiri kupewa fedha hizo, hivyo ni vyema vyombo vinavyohusika vikamuhoji.

“Vigogo wa Serikali, Bunge na Mahakama wanaotajwa kulipwa fedha kupitia akaunti ya VIP wanapaswa kuchunguzwa na PCCB (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa), kwakuwa akaunti hiyo ilipokea fedha za Escrow. Hivyo ni wito wangu kwa PCCB imuhoji Profesa Tibaijuka kwakuwa amekiri kupokea fedha hizo,” alisema Kafulila alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana.

Kafulila amesema pia kuwa Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh, akabidhi ripoti ya uchunguzi wa ufisadi wa Sh bilioni 200 kabla hajaacha ofisi Ijumaa.

“Hii ni kwa sababu yeye mwenyewe kabla hajaagizwa na Bunge aliomba siku 45 Machi 20, hadi leo ni zaidi ya siku 160 zimepita na hajakabidhi ripoti hiyo wala kutoa taarifa yoyote.

“Majibu anayotoa kuwa watafanya waliobaki, yanatia shaka hasa ukizingatia muda uliokwisha hadi sasa. Anaposema kazi hii ni sawa na majukumu mengine ya kawaida ni kielelezo cha kukimbia wajibu wake katika suala hili tete ambalo limesababisha hadi sasa nchi wahisani wasichangie bajeti kusubiri uchunguzi huu,” alisema Kafulila.

Alisema pia kuwa akauti ya VIP iliyopo Benki ya Mkombozi, ilipaswa kufungwa hadi uchunguzi ukamilike kwani ni mfaidika wa hela za Escrow zinazochunguzwa.

“Hiwezekani Benki ya Ulaya imesimamisha Akaunt ya VIP Uholanzi kwa shaka ya kupokea hela zinazochunguzwa za Escrow, lakini Tanzania bado VIP haijafungwa kusubiri uchunguzi,” alisema Kafulila.

Alisema pia kuwa taarifa zilizopo ni kwamba PCCB wameshakabidhi ripoti ya suala hilo Ikulu badala ya Bunge lililoomba kufanyika kwa uchunguzi huo.

“Hii ni kinyume cha utawala bora na ni mwanya wa uchakachuaji wa ripoti kama ilipotokea mwaka 2000 ambapo ripoti ya PCCB kuhusu wahusika walioingiza nchi kwenye mkataba mbovu wa IPTL walifichwa na Ikulu na kusababisha nchi kuendelea na mkataba wa kinyonyaji wa miaka 20,” alisema Kafulila.

Gazeti hili lilipomtafuta Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue, ili kuzungumzia suala hilo, alisema Ikulu haijapokea taarifa hiyo.

ZITTO
Naye Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe, amesema suala hilo litazidi kuvuruga imani ya wananchi kwa utawala wa Rais Jakaya Kikwete kama wahusika wa suala hilo hawatachukuliwa hatua.

Alisema kutokana na hali hiyo, wanasiasa wanapaswa kuhamasisha ili kusaidia kuwafikisha waliotekeleza kashfa ya IPTL, PAP mbele ya sheria mara watakapokuwa wamepata vielelezo vinavyohitajika.

“Katika hali ya kawaida unaweza kujiuliza inakuwaje mtambo wa kufua umeme ulete mgogoro kisheria na katika vyombo vya habari kwa karibu miongo miwili na ukaruhusiwa kuvuruga vipaumbele vya uzalishaji umeme nchini.

“Pia inakuwaje mradi huu uchangie kutokea hasara kubwa kwa sekta ya umma na binafsi, hii inaonyesha kuwa mradi huu ni kielelezo cha utawala mbovu ndani ya Wizara ya Nishati,” alisema.

Kutokana na hali hiyo, alisema kuna maswali kadhaa ambayo hayajajibiwa ikiwa ni pamoja na kwanini Tanesco iliilipa IPTL kwa muda mrefu bila ya kuhoji malipo ya uwezo wa mitambo ni kwa muda gani mtambo wa IPTL ulikuwa haufanyi kazi na ni wakati gani ulipoanza tena, lakini pia wananchi wanapaswa kujiuliza kuwa nani alilipia matengenezo yake wakati ukiwa haufanyi kazi.

Alihoji pia kiasi cha fedha zilizobaki katika akaunti ya Escrow kama ni kweli ipo, IPTL inafanya kazi gani, nani anamiliki, hali yake ikoje, je hivi sasa inapata fedha za uendeshaji wa mitambo na ni kiasi gani, halafu kuna makubaliano gani kati ya kampuni hiyo na Tanesco.

- Advertisement -

Related Articles

1 COMMENT

  1. Kama mama Profesa Tibaijuka kapokea hela ya Escrow, basi tumekwisha!!!! hela ya utumishi wa Umoja wa Mataifa haikumtosha na kugeukia ya maskini jeuri wa Tanzania!! unbelievable! kama ni uongo mhe Kafulila ashitakiwe.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles