22.2 C
Dar es Salaam
Friday, October 11, 2024

Contact us: [email protected]

ASKOFU KKKT AJINUSURU MTEGO WA KUTENGWA

 

Na WAANDISHI WETU-MTWARA/DAR


ASKOFU wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kusini Mashariki, Dk. Lucas Mbedule, ametii maagizo ya Baraza la Maaskofu wa KKKT kwa kuwaomba radhi waumini.

Askofu huyo ni miongoni mwa maaskofu wengine wawili waliotuhumiwa kusaliti waraka wa Pasaka kwa kuzuia usisomwe katika dayosisi zao.

Katika Kikao cha Halmashauri Kuu ya KKKT kilichofanyika hivi karibuni jijini Arusha na kile cha Baraza la Maaskofu, Askofu Mbedule na Askofu wa Dayosisi ya Kaskazini na Kati, Solomon Massangwa, walitakiwa kuomba radhi.

Tukio la kuomba radhi kwa askofu huyo lilifanyika jana wakati wa ibada iliyofanyika katika Kanisa la KKKT Usharika wa Mtwara Mjini.

Alisema amemwandikia barua Mkuu wa KKKT, Dk. Fredrick Shoo na maaskofu wote wa kanisa hilo, huku akisema yuko pamoja na maaskofu wenzake kwa sababu alishiriki kuuandaa waraka huo.

Askofu huyo alisema alishindwa kuusoma waraka huo kwa sababu zilizojitokeza wakati huo na kuwaomba radhi waumini wa kanisa hilo.

“Dayosisi yote ya Kusini Mashariki iko pamoja na kanisa zima katika yale ambayo tumeyapanga, kwahiyo naomba tuendelee kushirikiana,” alisema Askofu Mbedule.

WAUMINI

Baadhi ya waumini waliozungumza na MTANZANIA, walisema licha ya askofu huyo kuomba msamaha, bado hawajajua kwanini alishindwa kuusoma waraka huo.

“Tumesikia barua yake ya kuomba msamaha wa kutosoma waraka wa maaskofu ikisomwa, lakini hatujajua kwanini hakuusoma. Huenda hata mgogoro tulionao ukawa umechangia kutosomwa kwa tamko hilo,” alisema Elizabeth Moshi.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya kanisa hilo, zilieleza kuwa askofu huyo pia anajiandaa na mkutano mkuu wa dayosisi hiyo ambao utafanyika Mei 17, mwaka huu.

“Wazee walishakataa juu ya mkutano wa Mei 17, mwaka huu ambao aliuandaa Askofu Mbedule. Tunaona akiendelea kukusanya michango na kuutangaza kuwa bado upo, hili linatutia mashaka,” alisema mmoja wa waumini, Steven Macha.

ASKOFU MALASUSA

Askofu Malasusa pia alijadiliwa katika kikao hicho na baraza kutangaza kumtenga kwa kusema kwamba, haruhusiwi kuliwakilisha kanisa mahali popote hadi atakapoomba radhi.

Hata hivyo, uamuzi wa Baraza la Maaskofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) kumwadhibu kwa kumtenga Askofu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Dk. Alex Malasusa, kwa tuhuma za usaliti, huenda ukamweka katika wakati mgumu zaidi ikiwa ni pamoja na kuupoteza uaskofu iwapo hatatimiza sharti la kuomba msamaha.

Mwishoni mwa wiki iliyopita, MTANZANIA Jumamosi liliripoti habari za ndani, likieleza kiini cha tuhuma hizo za usaliti dhidi ya Askofu Malasusa, kinaelezwa ni uamuzi wake wa kuzuia waraka wa Pasaka ulioandaliwa na maaskofu 27 wa kanisa hilo, usisomwe katika Dayosisi ya Mashariki na Pwani anayoiongoza.

MTANZANIA lilimtafuta Askofu Malasusa ili kufahamu iwapo ataliomba kanisa msamaha kama alivyoelekezwa na kikao hicho cha Baraza la Maaskofu baada ya kupewa muda wa kujitafakari hadi ifikapo Septemba, lakini hakupatikana.

Hata hivyo, juhudi za MTANZANIA jana za kumpata Askofu Malasusa kufahamu iwapo ataliomba kanisa msamaha kama alivyoelekezwa na kikao hicho cha Baraza la Maaskofu, hazikuzaa matunda.

Gazeti hili pia lilimtafuta Katibu Mkuu wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani, Godrey Nkini, ili kuzungumzia suala hilo lakini alisema si msemaji.

“Hilo suala na mengine yanayohusu KKKT yanazungumziwa na Katibu Mkuu au Mkuu wa KKKT,” alisema Nkini.

Juhudi za kumtafuta Mkuu wa KKKT, Askofu Dk. Fredrick Shoo, kupitia simu yake ya kiganjani, hazikuzaa matunda kwani mara kadhaa alipopigiwa hakupokea na hata alipotumiwa ujumbe mfupi wa maneno hakujibu.

Kwa habari zaidi jipatie nakala ya gazeti la MTANZANIA.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
590,000SubscribersSubscribe

Latest Articles