27.3 C
Dar es Salaam
Tuesday, September 17, 2024

Contact us: [email protected]

MAMBO 6 YATIKISA BUNGE WIKI HII


Na GABRIEL MUSHI - DODOMA    |

MAMBO sita yametikisa vikao vya Bunge la 11 vilivyoendelea kufanyika wiki hii jijini hapa, wakati wizara mbalimbali zikiendelea kuwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya bajeti zao.

Miongoni mwa mambo hayo, ni ununuzi wa ndege za Shirika la Ndege Tanzania (ATCL) na ujenzi wa reli ya kisasa (SGR).

Mijadala mbalimbali iliyotikisa Bunge ilitokana na michango ya wabunge, wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi, Mawasiliano na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mbali na ununuzi wa ndege hizo aina ya Bombardier na ujenzi wa reli ya kisasa, pia jina la Rais Dk. John Magufuli, lilizua gumzo kila lilipotumika kwa upinzani na CCM sambamba na jina la nchi ya Rwanda ambalo Naibu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson, alilazimika kulitolea ufafanuzi.

Pia wabunge hawakusita kuzungumzia kwa kina uamuzi wa Serikali kufungia nyimbo za wasanii kwa kile kilichodaiwa ni kukiuka maadili, hali iliyolazimu baadhi kudai huu si wakati wa kuvaa madera au pekosi. 

BOMBARDIER/ATCL

Mapema wiki hii, wabunge waliendelea kuparurana kuhusu mjadala wa ununuzi wa ndege mpya aina ya Bombardier, huku baadhi yao wakidai Serikali imewekeza zaidi ya Sh trilioni moja katika ununuzi wa ndege hizo.

Pia walisema kuna hatari ndege nyingine mbili za Serikali kukamatwa nje ya nchi baada ya ATCL kufunguliwa kesi nyingine ya madai ya zaidi ya Sh bilioni 80 jijini London, Uingereza.

Akichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kwa mwaka 2018/2019, Mbunge wa Ubungo, Saed Kubenea (Chadema), alisema Serikali inatakiwa kuangalia ilipojikwaa na kuanguka kwa sababu tayari ATCL imefunguliwa kesi nyingine London.

“Tunadaiwa zaidi ya dola milioni 38, zaidi ya shilingi bilioni 80. Tayari Serikali imelipa pauni 15,000 kwa ajili ya malipo ya awali ya mawakili London, kutokana na mikataba iliyosainiwa na Kampuni ya Walis, wameenda kufungua kesi wanatudai, kuna hatari ya Bombardier zetu zikakamatwa tena kama ilivyotokea kule Canada,” alisema.

Mjadala huo wa Bombardier uliendelea kupamba moto wakati Mbunge wa Kawe, Halima Mdee (Chadema), aliposema Serikali imetupa fedha zaidi kwenye shirika hilo kwa sababu mwaka jana ilitenga Sh bilioni 500 na katika bajeti ya mwaka huu 2018/2019 imetenga tena Sh bilioni 495 katika ununuzi wa ndege.

“Hoja si kupinga ununuzi wa ndege, hoja hapa ni fedha tunazowekeza ambazo ni matrilioni ya shilingi. Je, zinakwenda kuzalisha au tunakwenda kuzitupa na kupotea,” alisema.

Naye Mbunge wa Kilolo, Venance Mwamoto (CCM), alimtaka Rais Magufuli kutosikiliza kelele zinazopigwa na baadhi ya watu kuhusu juhudi za kuiboresha ATCL. 

SH TRILIONI 1.5

Katika michango hiyo ya wabunge, sakata kuhusu zilipo Sh trilioni 1.5 zilizoibuliwa na Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe (ACT- Wazalendo), baada ya kuchambua ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), liliendelea kupamba moto.

Mbunge wa Rombo, Joseph Selasini (Chadema), alimwomba Rais Magufuli amwagize Msajili wa Hazina kwenda na makabrasha yake kwa CAG yakakaguliwe upya namna zilivyotumika Sh trilioni 1.5.

Selasini alisema kiwango hicho cha fedha ambacho hakionekani, kingefaa kutumika kutekeleza miradi ya maendeleo.

Aliwataka wabunge kuacha kujadili suala hilo kisiasa na kusoma vitabu vya CAG, kwa sababu katika mwaka wa fedha 2015/2016 pia CAG alibainisha upotevu wa Sh trilioni 1.088 ambazo hazikufahamika zimetumika vipi.

Hata hivyo, ripoti ya CAG katika ukurasa wa 40, inaonyesha kiwango hicho kilichopotea ni Sh trilioni 1.8.

Hoja hiyo iliungwa mkono na Mbunge wa Tanga, Musa Mbarouk (CUF) na Mbunge wa Vunjo, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ambao kwa pamoja walisema fedha hizo zingesaidia kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo. 

UJENZI RELI YA KISASA

Ujenzi wa SGR ulitikisa Bunge baada ya Mbunge wa Nzega, Hussein Bashe (CCM), kubainisha kwa kina namna mpango wa ujenzi wa reli hiyo unavyokiuka Ilani ya Uchaguzi ya CCM.

Akichangia mjadala kuhusu hotuba hiyo, Bashe, alisema licha ya kwamba anaunga mkono ujenzi wa reli hiyo, lakini kinachomsikitisha ni mabadiliko yaliyojitokeza katika ujenzi huo, unaoelekea kuifanya Rwanda kuwa kitovu cha biashara ya bandari katika nchi za Afrika Mashariki (EAC).

“Reli hii ilitakiwa ijengwe kutoka Dar es Salaam-Tabora, Tabora-Mwanza, Tabora-Kigoma, Kaliua-Mpanda- Kalemii, Uvinza–Msongati.

“Kitabu cha bajeti mwaka huu kinaonyesha tunapitisha shilingi trilioni 1.5 kwa ajili ya ujenzi wa reli na shilingi trilioni 1.4 zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa awamu ya kwanza na ya pili,” alisema.

Pia alisema Serikali imetenga Sh bilioni 100 kujenga reli kutoka Isaka kwenda Rwanda, yenye umbali wa kilomita 371 itakayogharimu zaidi ya Dola za Marekani bilioni 1.5 hadi 2 (Sh trilioni nne).

Alisema takwimu zinaonyesha karibu asilimia 40 ya mzigo unaotokana na bandari ya Dar es Salaam unakwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wakati Rwanda ni asilimia 12 tu.

Bashe aliungwa mkono na idadi kubwa ya wabunge akiwamo Mbunge wa Mtwara Vijijini, Hawa Ghasia (CCM). 

JINA LA RWANDA

Hoja kuhusu kutajwa kwa jina la nchi ya Rwanda, ilizua gumzo wakati Bashe alipoendelea kushikilia hoja ya kutounga mkono bajeti ya Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano hadi Waziri Profesa Makame Mbarawa, atakapofafanua hoja zake.

Bashe alisema anaona Serikali ikifanya kosa kwa kutekeleza mambo yaliyobuniwa na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) chini ya aliyekuwa rais, Donald Kaberuka, aliyetengeneza mpango kazi wa njia ya kaskazini kutoka Mombasa kwenda Kigali na kutoka Dar es Salaam- Isaka- Kigali ili kuifanya Kigali kuwa kitovu cha kusafirisha mizigo.

“Hili si jambo jema kwa nchi yetu, si jema kwa Watanzania kiujumla. Ninachotaka kusema hatuna fedha ya kutoka Makutupora-Tabora, tunaweka fedha ya kujenga Isaka-Rwanda! Tutasafirisha kwa reli hadi Makutupora, halafu tutasafirisha kwa helikopta kwenda Rwanda?” alihoji.

Hoja hiyo Bashe ilimlazimu Dk. Tulia kutolea ufafanuzi wa matumizi ya majina ya nchi, ikiwamo Rwanda, baada ya wabunge kuzozana kuhusu matumizi ya jina hilo pindi wanapochangia hoja.

“Huwezi kusimama hapa na kuituhumu nchi kuwa inaua Watanzania, hapana ila kama ukiizungumzia nchi hiyo, ukazungumzia jambo jema kwa Tanzania, ni sawa sawa.

“Bunge ni chombo kikubwa, hakijadili mambo ya nchi nyingine kwa ubaya. Nimelazimika kutoa ufafanuzi huo kwa sababu wabunge wataanza kukatazana kutoa maelezo au kutaja jina la nchi aseme mwongozo haujawahi kutolewa, mwongozo ndiyo huo kwamba wabunge kama ambavyo unaweza kumsifia mtu akafurahi, vile vile ukimsemea jambo baya atajisikia vibaya,” alisema. 

JINA LA RAIS MAGUFULI

Matumizi ya jina la Rais Magufuli yaliibua gumzo wiki hii baada ya wabunge wa upinzani kuwataka viongozi wa Serikali kumshauri vizuri ili asije kukumbwa na tuhuma mbalimbali baada ya kustaafu.

Aidha, mawaziri na wabunge wa CCM nao walipinga wapinzani kutumia jina la Rais Magufuli kushawishi Bunge.

Mmoja wa wabunge hao wa upinzani, ni Mbunge wa Simanjiro, James ole Milya (Chadema), aliyesema ni muda mwafaka washauri wa rais kumshauri achukue hatua kuhusu upotevu wa Sh trilioni 1.5.

“Wamshauri vizuri, kwa sababu Rais Magufuli hatadumu milele. Ataondoka kwenye madaraka, nyie hamumwelekezi amekosea. Ni vizuri kumshauri vizuri kwa sababu fedha za umma ni za umma, mtu huwezi kuchukua kama unachukua fedha zako mfukoni. Kuna taratibu za kuchukua fedha hizo,” alisema.

Kauli hiyo ilimwibua Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla, aliyesema Milya amevunja kanuni ya 64 ya Bunge kwa kutumia jina la rais kufanya ushawishi kwa wabunge.

Mjadala huo uliendelea pia wakati Mbunge wa Kawe, Mdee (Chadema), akitoa mchango wake katika bajeti hiyo.

Mdee alisema kinga aliyonayo rais kikatiba inaweza kuondolewa iwapo hatatekeleza majukumu yake ipasavyo.

Kauli hiyo ya Mdee iliibua mvutano baada ya Naibu Waziri wa Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Stella Manyanya, Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi na Mbunge wa Siha, Dk. Godwin Mollel (CCM), kumwomba Spika Job Ndugai kutoa taarifa kuwa jina la rais linatumika vibaya.

Hata hivyo, kadhia hiyo ilimkumba Mbunge wa Mbinga, Sixtus Mapunda (CCM), baada ya kusifia utendaji wa Rais Magufuli, hatua iliyomwibua Mbunge wa Tunduma, Frank Mwakajokwa (Chadema), aliyesema Mapunda anatumia jina la rais kushawishi Bunge. 

FUNGIAFUNGIA WASANII

Hoja nyingine iliyoibua mtikisiko wiki hii ni kuhusu mtindo wa Serikali kufungia wasanii wanaoimba nyimbo zisizokuwa na maadili.

Wabunge wengi walilalamikia uamuzi huo wakati wakichangia hotuba ya bajeti ya Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo akiwamo Mbunge wa Geita Vijiji, Joseph Kasheku Musukuma (CCM), aliyeitaka Serikali kutoa elimu kwa wasanii wa filamu na muziki kuhusu maadili badala ya kuwafungia kazi zao.

Aliishauri Serikali kutambua kwa sasa si zama za kuvaa madera au vipekosi, hivyo wasanii wanahitaji kupewa uhuru.

“Lakini kwa ‘style’ zinazoendelea kwa waziri, hii tasnia tunaenda kuipoteza, kipindi cha katikati kumetokea fungia fungia, ila sasa kinachotokea msanii anafanya kazi nzuri, akikosea kidogo kwenye kuonyesha mpasuo, waziri anafungia, sasa namuuliza unafungia miziki ya Watanzania kwa sababu ya kuonyesha mpasuo wakati mnaangalia ya kina Rihanna kwenye youtube,” alisema.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
589,000SubscribersSubscribe

Latest Articles