24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

Asilimia moja ya Watanzania wana matatizo ya akili – Waziri

Ramadhan Hassan – Dodoma

SERIKALI imesema asilimia moja ya Watanzania wana matatizo ya akili licha ya kwamba bado Serikali haijafanya utafiti kujua takwimu halisi za tatizo hilo.

Hayo yalielezwa jana bungeni na Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile, wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Viti Maalumu, Kemilembe Lwota (CCM).

Katika swali lake, mbunge huyo alisema utafiti wa nchi mbalimbali ikiwamo Marekani, unaonyesha katika kila watu wanne, mmoja ana ugonjwa wa akili, Uingereza kwa kila watu watano mmoja ana tatizo la akili.

“Mheshimiwa Spika, nadhani hata wewe ni shahidi, hata humu ndani wakati mwingine tunajiuliza tupo salama kiasi gani, nataka kufahamu Serikali imefanya utafiti kujua ni watu wangapi wanakabiliwa na tatizo la akili Tanzania, na matokeo yakoje?” alihoji Lwota.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile alikiri kuwa matatizo ya afya ya akili yanazidi kuongezeka na kwamba Shirika la Afya Duniani (WHO) limeweka msukumo katika kuliangazia tatizo hilo.

Alisema takribani asilimia moja ya jamii ya Watanzania wana matatizo ya akili.

“Takribani asilimia moja ya jamii ya Watanzania tunaamini wana matatizo ya akili, inawezekana hata humu ndani tunachangia kwenye hiyo asilimia moja, tuna changamoto kama hizo,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema Serikali bado haijafanya utafiti wa kina kuangalia uzito wa jambo hilo ukoje na aina ya magonjwa ya akili yaliyopo nchini.

Awali katika swali la msingi, Mbunge wa Viti Maalumu, Fatma Toufiq (CCM) alihoji ukatili dhidi ya wanawake na watoto bado unaendelea kwa kiwango kikubwa hapa nchini.

“Je, Serikali ina mkakati gani wa kuwahudumia kwa unasihi na unasaha wahanga wa ukatili,” alihoji Fatma.

Akijibu swali hilo, Dk. Ndugulile alisema Serikali inatambua uwepo wa vitendo vya unyanyasaji na ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini.

“Kwa kuliona hilo, Serikali iliandaa mpango kazi wa kitaifa wa miaka mitano wa kutokomeza vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ambao unatekelezwa kwa kipindi cha 2017/18 – 2021/22,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema mpango mkakati huo unaainisha mikakati mbalimbali ya kupambana na kudhibiti ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake na watoto.

“Serikali imeanzisha vituo 11 vya mkono kwa mkono (One stop centres) kwenye mikoa ya Dar es Salaam, Pwani, Mbeya, Iringa, Kilimanjaro, Shinyanga, Mwanza, Arusha na Simiyu kwa ajili ya kuwahudumia waathirika wa vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto,” alisema Dk. Ndugulile.

Alisema kuwa katika vituo hivyo, huduma za kipolisi, ushauri nasaha na huduma za afya zinatolewa kwenye kituo kimoja.

“Lengo la Serikali ni kuwa na kituo angalau kimoja kwa kila mkoa na hii inaenda pamoja na kuwajengea uwezo wahudumu katika eneo la utoaji huduma husika,” alisema Dk. Ndugulile.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles