ALGIERS, ALGERIA
MAMIA kwa maelfu ya waandamanaji walifurika mitaani juzi katika miji mbalimbali nchini Algeria, ambapo wanapinga Rais Abdelaziz Bouteflika, kuwania katika uchaguzi wa urais ujao kwa awamu ya tano.
Rais Bouteflika, mwenye umri wa miaka 81, anaendelea kukabiliwa na maandamano ya watu wenye hasira ambao wamekuwa wakilalamikia kupanga gharama za maisha pamoja na kupinga rais huyo mkongwe kugombea tena katika uchaguzi ujao.
Maandamano haya ambayo yalianzishwa hasa na vijana, hivi karibuni vyama karibu vyote vya upinzani vilijiunga na vijana hao na kupinga Abdelaziz Bouteflika, kuwania tena muhula wa tano katika uchaguzi ujao.
Tangu wiki iliyopita, karibu vyama vyote vya upinzani vimejiunga na waandamanaji. Wanafunzi pia wamehamasishwa wiki hii, hata waandishi wa habari, ikiwa ni pamoja na vyombo vya habari vya Serikali, ili kupinga udhibiti na shinikizo wanazozipata katika kazi yao.
Mapema wiki hii Waziri Mkuu wa Algeria, alitangaza kuwa Rais Bouteflika, atapeleka fomu yake leo ambayo ni tarehe ya mwisho kwa wagombea waliochelewa wanaotaka kuwania urais katika uchaguzi ujao.