Na Markus Mpangala
AFADHALI ya jana. Hiyo ndiyo kauli pekee ambayo inafaa kutumika kwa sasa kuzungumzia kuvunjika kwa kikao kilichowakutanisha Rais wa Marekani, Donald Trump na Kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un mjini Hanoi nchini Vietnam, barani Asia.
Ni afadhali ya kikao chao kilichofanyika nchini Singapore mnamo Juni 2 mwaka jana kuliko hiki cha Februari 28 mwaka huu. Kikao cha mwaka huu kimeshuhudia Rais Trump akilazimika kuondoka kikaoni baada ya kushindwana na mwenzake, Kim Jong-Un, na kuzua mjadala mkubwa duniani. Makala haya yanafafanua mambo ya msingi kuhusu vikao vya aina hiyo.
Je, nini hasa kilichotokea mjini Hanoi?
Inaelezwa kuwa kwenye kikao hicho hakukuwa na makubaliano yoyote, kwani kila upande ulishikilia msimamo wake. Korea Kaskazini inatakiwa kuacha matumizi na urutubishaji wa silaha za nyuklia kama sharti la kufikia mwafaka wa mgogoro baina yake na mataifa makubwa. Kim Jong Un anatakiwa kuangamiza vituo vyote vya majaribio ya silaha hizo.
Duru za kidiplomasia zinasema kuwa, Kim Jong Un alisisitiza kuwa ili atekeleze masharti aliyopewa ni muhimu kwa Umoja wa Mataifa kuondoa vikwazo vyote dhidi ya Korea Kaskazini ambavyo vinahusiana na mipango ya kutengeneza silaha.
“Lilikuwa suala la kuondoa vikwazo. Kimsingi walitoa masharti ya kuondolewa vikwazo kwa njia wanayotaka wao, lakini hatukuweza kufanya hivyo,” alikaririwa Rais Trump na gazeti la New York Times.
Kimsingi hoja hii inatuletea swali, Kim Jong Un alitaka kuondoa vikwazo bila kikao cha Umoja wa Mataifa? Jibu rahisi ni kwamba Kim Jong Un anategemea ushawishi wa Marekani katika kuondoa vikwazo, kwahiyo kikao cha Umoja wa Mataifa kinatumika kuidhinisha makubaliano, jambo ambalo linahitaji mchakato na lisingewezekana kufanywa na timu ya Trump kwa wakati huo wala kukubaliana nalo.
Kwa mantiki hiyo, hoja za Korea Kaskazini ziliwaondoa Marekani kwenye mjadala, kwani suala lilikuwa linahusu Umoja wa Mataifa moja kwa moja. Kwa namna nyingine hii ni mbinu ya kidiplomasia kusogeza mbele majadiliano dhidi ya Korea Kaskazini, hali ambayo haitashangaza kama suala la vikwazo dhidi ya nchi hiyo litazungumzwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.
Aidha, Marekani ilitoa hoja kuwa ni lazima vinu vya nyukilia vilivyoko eneo la Yongbyon vinavyotumika kufanya utafiti, urutubishaji na kuzalisha silaha za nyukilia za Korea Kaskazini viondolewe kama sehemu ya majadiliano ya amani baina yao. Eneo la Yongbyon nchini Korea Kaskazini ni maarufu kwa upatikanaji wa kemikali ya plutonium, lakini nchi hiyo ina takriban vinu viwili vinavyozalisha uranium.
Hoja ya pili iliyosababisha Marekani ione kikao hicho hakikuwa na manufaa hivyo kuondoka mezani ni msimamo wa Korea Kaskazini kuwa ipo tayari kuondoa vinu vya Yongbyon pekee na si vinu vyote vya nyukilia vya Korea Kaskazini. Marekani imekataa matakwa ya Korea Kaskazini ya kutaka kuondolewa kwa vikwazo vyote.
Ikumbukwe kwenye kikao cha kwanza kati ya viongozi hawa wawili, kilichofanyika nchini Singapore Juni mwaka 2018, kilikosolewa kwa kutofikiwa kwa matarajio, lakini hata yale yaliyotarajiwa kuwa yangefikiwa katika kikao cha pili nako kumezua hisia kwamba Trump ameshindwa au hana ushawishi wowote kwa Korea Kaskazini, licha ya kufanya kikao cha pili cha jijini Hanoi. Kushindikana kwa awamu hii ni changamoto kwa Trump.
Msimamo wa Korea Kaskazini
Mara baada ya kumalizika kikao hicho tumeona Korea Kaskazini ikifunguka zaidi na kuelezea msimamo wake. Kwa mujibu gazeti la China Daily, Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa nchi hiyo, Ri Yong Hon, amesema msimamo wao hautabadilika, hata kukiitishwa kikao cha tatu.
Waziri Ri Yong Hon amesisitiza kuwa nchi yake ilitaka unafuu wa sehemu tu ya vikwazo, na sio kuondolewa vyote. Amevielezea vikwanzo hivyo ni vile ambavyo vinazuia uchumi na maisha ya watu wao.
Ameongeza kuwa nchi yake iliwasilisha mapendekezo yenye uhalisia, ikiwamo kuangamiza kituo cha utafiti wa nyukilia cha Yongbyon, chini ya uangalizi wa Marekani.
Hata hivyo, kwa mtazamo wa Waziri Ri, kikao cha pili kimeonesha kuwa Korea Kaskazini na Marekani zimefikia hatua kubwa na nzuri zaidi ya majadiliano na huenda mwafaka wa kuangamiza vinu vya nyukilia utapatikana chini ya viongozi hao.
Kwa upande Msemaji wa Ikulu ya Marekani, Sara Sanders, Rais Donald Trump na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, wana matumaini kuwa maofisa wa pande zote watayarejesha tena mazungumzo hayo katika kikao cha tatu cha kutafuta ufumbuzi zaidi.
Historia imejirudia
Kwa mujibu wa gazeti la The New York Times, wakati wa utawala wa Rais Ronald Reagan, kuliwahi kutokea majadiliano makali mwaka 1986 yaliyofanyika mjini Reykjavik, nchini Iceland, yakizihusisha nchi mbili; Marekani na Urusi. Kwenye kikao hicho kulijadiliwa juu ya taratibu na kanuni za matumizi ya silaha baina ya mataifa hayo. Lakini hapakuwa na mafanikio yoyote ambapo Rais Reagan alilazimika kuondoka kikaoni. Mwaka mmoja baadaye Serikali ya Urusi ilikuja na mapendekezo mazuri ambayo yaliivutia Marekani, ndipo mkataba ukasainiwa. Hivi ndivyo inavyotegemewa kwenye vikao vya Trump na Kim Jong Un.
Baada ya kuvunjika kikao cha mwaka huu kumekuwa na wasiwasi kwamba huenda Korea Kaskazini itaendeleza majaribio ya nyukilia kama mbinu yake ya kuchochea moto kuelekea wazo la kuitishwa kikao cha tatu cha viongozi hao.
Kwanini Kim hukutana na Xi Jinping?
Swali hili pia linaulizwa mara nyingi. Kabla ya kikao cha Juni 2 mwaka jana, Kim Jong Un alikwenda nchini China kuzungumza na Rais Xi Jinping. Safari ya Kim kutoka Korea Kaskazini pia ilipitia China badala ya anga la Korea Kusini.
Januari mwaka huu kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong-un, alifanya ziara nyingine nchini China yaliyokuwa na lengo la kufanya mazungumzo na Rais wa nchi hiyo, Xi Jinping. Ziara hiyo ilitajwa kuwa sehemu ya mikakati ya kupanga ajenda za mkutano wa pili kati ya Rais Kim Jong na Rais wa Marekani, Donald Trump.
Kim alifanya ziara hiyo akiwa na maofisa wa serikali yake, ikiwa ni mara ya nne katika kipindi cha chini ya mwaka mmoja. China ni mshirika muhimu wa kidiplomasia wa Korea Kaskazini na moja ya vyanzo vikuu vya biashara na misaada.
Duru za kisiasa zinasema kuwa ziara hizo huwa zinakuwa na makusudi ya kuziambia nchi za magharibi kuwa Korea Kaskazini ina njia mbadala ya kujikimu kiuchumi tofauti na ile iliyozoeleka ya Marekani na Korea Kusini.
Hadi sasa hakuna mafanikio makubwa yaliyofikiwa na viongozi hawa wawili, Kim Jong Un na Trump, ingawa nafasi ya kuendelea na vikao bado ingalipo.