Na Markus Mpangala, Dar es salaam
HATIMAYE aliyekuwa mgombea wa urais wa Chadema na muungano wa vyama vya upinzani maarufu kama Ukawa (Umoja wa Katiba ya Wananchi), Edward Lowassa amehama kambi ya upinzani na kurudi chama tawala cha CCM.
Kabla ya kuhamia Chadema pamoja na upinzani mnamo Julai 12 mwaka 2015, Lowassa alikuwa mwanasiasa mashuhuri ndani ya CCM ambaye aliapa kutohama na atahakikisha angeteuliwa kugombea urais kwa tiketi ya chama hicho. hata hivyo hali haikuwa hivyo, kwani Lowassa alikatwa katika hatua za awali na nhakuingia katika tano bora.
Uamuzi wa Lowassa kurudi CCM huenda ulisukwa siku nyingi kutokana na mwenendo ulivyokuwa kati yake na serikali ya awamu ya tano. Lakini jambo muhimu ni kwamba Lowassa ni mwanasiasa ambaye anayo haki ya kuchagua, kuamua hatima yake na anafahamu anachokifanya. Inawezekana kwa sasa kukawa na maswali mengi juu ya uamuzi wake wa kurejea CCM, lakini angalau alitimiza ndoto zake za kugombea urais.
Lowassa amekuwa mwanasiasa wa kwanza aliyegombea urais kwa tiketi ya chama cha upinzani na kupata kura takribani milioni 6 ikiwa ni rekodi ya kipekee ambayo haijafikiwa na mgombea yeyote. Na zaidi rekodi ya kura hizo haijwahi kufikiwa na mgombea yeyote ndani ya Chadema tangu mwaka 2005 walipoanza rasmi kuweka wagombea kwenye nafasi ya urais.
Kuondoka kwa Lowassa kunatengeneza njia nyeupe kwa Mbunge wa Jimbo la Singida Mashariki nchini kwa tiketi ya Chadema, Mwanasheria wa chama hicho na Mnadhimu Mkuu wa Kambi ya Upinzani Bungeni, Tundu Lissu ambaye alishatangaza nia ya kuwania urais kwa tiketi ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).
Akizungumza na mwandishi wa BBC Dira ya Dunia, Zuhura Yunus, katika mahojiano yaliyofanyika mjini London mapema mwaka huu Tundu Lissu alieleza kuwa ikiwa chama chake kitamuunga mkono na kumteua kama mgombea basi atakuwa tayari kuwania kiti cha Urais na kupeperusha bendera ya chama hicho katika uchaguzi mkuu ujao mwakani.
Tundu Lissu ni moja ya wanasiasa wa upinzani ambao walikuwa wanatajwa mara kwa mara kuwania nafasi hiyo mwakani, baada ya waziri mkuu wa zamani Edward Lowassa kufanya hivyo mwaka 2015 mara baada ya kuhama CCM miezi michache kabla ya uchaguzi mkuu.
Duru za kisiasa tangu mwaka 2016 zilidokeza kuwa Tundu Lissu huenda akawa miongoni mwa wagombea urais kwa tiketi ya Chadema, lakini vilevile kauli iliyowahi kutolewa na Lowassa kuwa atagombea tena uraisi mwaka 2020 ilizua mjadala na kuweka mizani nani alifaa kuwania nafasi hiyo kati ya wanasiasa waliomo kwenye chama hicho.
Historia ya Chadema
Kila uchaguzi mkuu unapowadia Chadema kimekuwa na mgombea mpya katika nafasi ya urais. Uchaguzi mkuu wa mwaka 2005 Chadema walimteua Freeman Mbowe kugombea urais na kushika nafasi ya tatu nyuma ya Prof Ibrahimu Lipumba wa CUF na Jakaya Kikwete wa CCM aliyenyakua ushindi.
Mwaka 2010 Chadema walimteua Dkt Wilbroad Slaa ambaye alishika nafasi ya pili akibwagwa na Kikwete aliyekuwa akitetea kiti chake kwa awamu ya pili nay a mwisho. Uchaguzi wa 2015 Chadema walimpokea Lowassa kutoka CCM na kumpa tiketi ya kuwania urais, hata hivyo alibwagwa na rais wa sasa Dkt John Magufuli wa CCM.
Tangu kumalizika uchaguzi wa mwaka 2015 hadi sasa, Lowassa alikaririwa mara mbili akizungumzia nia yake ya kugombea urais katika uchaguzi wa mwaka 2020 bila kubainisha chama atakachotumia. Lowassa aliweka wazi nia hiyo Januari 14 mwaka 2016, alipozungumza na wafuasi wake wanaojulikana kama ‘Timu ya Mabadiliko’ wa Soko la Kariakoo jijini Dar es salaam.
Aidha, mwezi Julai mwaka 2017 Lowassa alirudia kauli yake na kusisitiza kuwa ataingia kwenye kinyang’anyiro cha kuwania urais ifikapo mwaka 2020. Tathmini hapa inaonyesha mchuano kati ya Lissu na Lowassa ni mkubwa mno.
Kwanini Lowassa alikuwa kikwazo kwa Tundu Lissu?
Kwa mujibu wa matokeo yaliyotangazwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi nchini Tanzania (NEC), mgombea wa CCM, Dkt.John Magufuli aliibuka mshindi baada ya kupata kura 8,882,935 sawa na asilimia 58.46. Edward Lowassa wa Chadema alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ya kura zote. Jambo ambalo lingeulizwa na Kamati Kuu ni uwezekano wa kupata mgombea mwingine wmenye uwezo wa kufikisha idadi hiyo ya kura kama ilivyokuwa kwa Lowassa. Kwa vyovyote vile Lowassa alikuwa kikwazo kwa Lissu katika dhana nzima ya kukubalika kwa wapigakura. Lowassa ni mtaji ambao Chadema wasingeweza kuutupa kondeni na kumteua mgombea mpya Tundu Lissu au mwanasiasa mwingine.
Sasa Lowassa ameondoka Chadema. Ameondoka kambi ya upinzani na kurejea kwenye chama alichokihama, CCM. Jambo hili linamwezesha Lissu kuvuka kikwazo cha kwanza cha kukubalika ndani ya chama na kwa wapigakura. Ikumbukwe Lissu tayari anazo kura za “huruma” kutoka kwa baadhi ya wapigakura kutokana na tukio la kushambuliwa kwake Septemba 7 mwaka 2017.
Kiongozi mmoja wa Chadema katika Kanda ya Ziwa, amewahi kuniambia haya; “Tundu Lissu ni mfano wa watu kama Dr.Slaa. Hana rasilimali fedha lakini ana watu nyuma yake wanaomkubali sana na ushawishi kwa siasa za upinzani. Lakini kwa nafasi ya urais sidhani kama atafanikiwa. Ndani ya chama wapo wanaomuunga Mkono lakini sio chaguo la mwenyekiti wala timu ya mwenyekiti. Na bado kuna suala ya ushirikiano na vyama vingine vya upinzani. Kama unaona harakati za Zitto Kabwe hadi sasa ni dhahiri anatamani sana angepata nguvu ya vijana na wanachama wa Chadema hasa kipindi hiki kuelekea kwenye chaguzi lakini kule ACT-Wazalendo hana wanachama wengi,”
Uamuzi wa Lowassa kuondoka Chadema sasa unaonesha kuwa Tundu Lissu amevuka kihunzi cha kwanza, ambapo cha pili ni kumshawishi Mwenyekiti wa chama hicho Freeman Mbowe kuwa yeye ni chaguo sahihi katika kinyang’anyiro cha urais mwaka 2020.
Katiba ya Chadema Ibara ya 7(7)(16), inaeleza moja ya kazi za Kamati Kuu ya chama hicho ni kufanya utafiti wa wagombea uraisi na mgombea mwenza na kuwasilisha ripoti yake Baraza Kuu, ambalo hupendekeza majina kwa mkutano ambao una mamlaka ya kuwateua.