PYONGYANG, KOREA KASKAZINI
HATUA ya Serikali za Marekani na Korea Kusini kutangaza kuwa zitasitisha mazoezi ya pamoja ya kijeshi, imetajwa kama kibao kinachotolewa na kiongozi wa Korea Kaskazini ambaye alitoa masharti ya kusitishwa mpango huo kama njia ya kufikia mwafaka na kupata amani katika rasi ya nchi hizo.
Kwa mujibu wa gazeti la Indian Times, Marekani na Korea Kusini zinapanga kusitisha mazoezi yao ya pamoja ya kijeshi yanayofanywa kila mwaka wakati Rais Donald Trump, akiendeleza juhudi za kuimarisha mahusiano na Korea Kaskazini.
Gazeti hilo limekariri taarifa ya Ofisa wa Marekani aliyezungumza na shirika la habari la AFP bila kutaja jina lake kuwa uamuzi huo umefanyika baada ya kuhitimishwa mkutano wa pili wa kilele kati ya Trump na kiongozi wa Korea Kaskazini, Kim Jong Un mjini Hanoi, nchini Vietnam, ambao ulimalizika bila makubaliano rasmi lakini kwa pande zote mbili kuashiria kuwa zitaendelea kuzungumza.
Nchini Korea Kusini, Ofisa wa Serikali alidokeza kuwa mazoezi hayo yatapunguzwa na si kufutwa kabisa. Pande zote mbili bado zinajadili kuhusu lugha ya kutumia katika taarifa yao ya pamoja ambayo inatarajiwa kutolewa katika siku chache zijazo.
Mazoezi hayo ya pamoja ya kila mwaka yaliyopewa jina la Foal Eagle, ndio makubwa kabisa kufanywa na washirika na kila mara huikasirisha Korea Kaskazini ambayo inayaona kuwa matayarisho ya wao kuvamiwa.