26.2 C
Dar es Salaam
Monday, March 27, 2023

Contact us: [email protected]

Agizo la JPM ladaiwa kupuuzwa Muheza

Oscar Assenga -Muheza

RAIS Dk. John Magufuli ameombwa kuwachukulia hatua watumishi wa Halmashauri ya Wilaya ya Muheza mkoani Tanga wanaodaiwa kushindwa kutekeleza agizo lake la kutaka mgawanyo wa shamba la mkonge la Kibaranga uzingatie wakazi wa maeneo hayo.

Ombi hilo limetolewa juzi na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Tanga, Yosepher Komba (Chadema), wakati wa mkutano wake na wakazi wa Kijiji cha Upare.

Komba alisema ipo haja kwa watumishi kuzingatia agizo la rais la kutaka kila mwananchi apewe hekari tatu kwa shughuli za kilimo.

Alisema wananchi wamekuwa wakilalamika juu ya kutokutendewa haki katika ugawaji wa shamba hilo, ambalo ni moja kati ya mashamba sita yaliyofutiwa hati na kukabidhiwa halmashauri.

Komba alisema wakati rais alipokuja kuweka jiwe la msingi la mradi wa bomba la mafuta, alitoa agizo na kutaka wakazi wa maeneo haya wapewe kipaumbele na hakuweka masharti yoyote.

Alisema vikwazo vinavyowekwa kwa wananchi juu ya taratibu za kupata maeneo kwa shughuli za kilimo, ni kwenda kinyume na agizo la rais.

Wananchi wakitoa malalamiko yao, walisema kumekuwapo na upindishwaji wa haki na zaidi wananchi wa Amani na maeneo mengine, wamekuwa wakipewa kipaumbe kupata maeneo ya kulima kuliko ilivyo kwa wazawa.

Ummy Mwinjuma, mmoja ya waathirika wa tatizo hilo, alisema kumewekwa masharti magumu ya kupata mgawo huo, ikiwa pamoja na kutakiwa kulipia, vitambulisho vya kupigia kura na zaidi wanawake walioolewa hawastahili kupata.

Alisema agizo la rais halikusema wanawake walioolewa wasipatiwe maeneo ya kulima.

Steven Anthony alisema kinachofanywa na halmashauri hiyo ni kuwakwamisha wananchi wanaostahili kupatiwa maeneo hayo.

Alisema kumewekwa utaratibu wa kila mwananchi awe na kitambulisho, malipo ya bikon Sh 20,000 ambazo zinadaiwa zilikusanywa na ofisa mtendaji wa kijiji ambaye sasa yupo masomoni tangu mwaka jana.

“Sisi wananchi wa Kibaranga, tunapenda maendeleo, tunarudishwa nyuma na viongozi wetu, wanakuja watu kutoka Amani wanapewa maeneo ambayo tulishayaandaa kwa kilimo,” alisema Anthony.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
211,206FollowersFollow
564,000SubscribersSubscribe

Latest Articles