27.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 19, 2024

Contact us: [email protected]

Sh mil 600 kujenga kituo cha afya

Amon Mtega -Mbinga

SERIKALI imetoa Sh milioni 600 ambazo zitatumika kwa ujenzi wa Kituo cha Afya Mapera, Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga mkoani Ruvuma.

Ujenzi huo utahusisha  majengo sita ya kituo hicho ambayo ni maabara, chumba cha upasuaji, wodi ya wazazi, mochwari, jengo la kufulia nguo, nyumba  ya mtumishi na miundombinu mingine.

Hayo yamesemwa na Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbinga, Dk. Louis Chomboko  kwa Mbunge wa Mbinga Vijijini, Martin Msuha (CCM)  aliyetembelea ujenzi wa kituo hicho.

Alisema  majengo hayo yatakapokamilika, yataboresha afya za wananchi wa kata hiyo na bonde zima la Hagati.

Dk. Chomboko aliwashukuru wananchi wa Kijiji cha Mapera kwa kukubali kutoa maeneo yao takribani ekari sita kujenga kituo hicho.

 Alisema awali makadirio ilikuwa watumie Sh milioni  400, lakini kiwango kimeongezeka  hadi kufikia milioni 600 kutokana na kuongeza majengo mengine,  ikiwamo jengo la wagonjwa wa  nje (OPD) ambayo yatajengwa kadiri fedha zitakavyopatikana.

Kwa upande wake, Msuha alisema katika Kata ya Mapera na Bonde la Hagati, kulikuwa na changamoto kubwa ya upatikanaji huduma za afya.

Alisema ujenzi wa kituo cha Mapera unatokana na kilio cha wananchi wa eneo hilo ambao  wanalazimika kwenda hadi Mbinga Mjini kufuata baadhi ya huduma kama  ya upasuaji mkubwa na mdogo.

Msuha aliishukuru Serikali kutoa fedha  kujenga kituo hicho, kwani kitawezesha wananchi wa maeneo hayo kupata huduma karibu.

Alisema mbali na fedha hizo, Serikali imetoa fedha kwa ujenzi wa barabara ya lami kutoka Mbinga hadi Wilaya ya Nyasa, yenye urefu wa kilomita 57 na kuridhia ununuzi wa gari la wagonjwa (ambulance).

Aliwataka wananchi kutunza majengo yatakayojengwa na kujiepusha kuhujumu mradi huo ambao kwa kiwango kikubwa utamaliza changamoto za huduma za matibabu.

“Serikali  imepeleka  Sh milioni  299.7 Bonde la Hagati kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo, huku ofisi ya mbunge kupitia Mfuko wa Jimbo, ikipeleka Sh milioni 50 ambazo zimetumika kuanzisha vitalu vya kahawa,” alisema.

 Kwa upande wake, Ofisa Mtendaji Kata ya Mapera, Nassibu Mapunda, alisema Serikali imetoa Sh milioni 417 kutekeleza mradi huo na nguvu ya wananchi imesaidia kuchangia Sh milioni 4.7, wakati halmashauri  ya wilaya imechangia Sh milioni 10.

Mmoja wa wakazi wa kijiji hicho, Anthony Komba, alimpongeza  Msuha kwa kuhakikisha  kituo hicho kinajengwa ili  kumaliza usumbufu kwa wananchi.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles