AFDB, JAPAN KUBORESHA NISHATI

0
492
Rais wa Benki ya Afrika, Dk. Akinwumi Adesima

ADDIS ABABA, ETHIOPIA

SERIKALI ya Japan na Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), zimeingia kwenye makubaliano ya kuanzishwa kwa mchakato wa nishati kati ya Japan na Afrika, ambayo yanalenga kumfanya kila mwananchi kupata nishati ya uhakika ifikapo mwaka 2025.

Makubaliano hayo yalitiliwa saini kando na mkutano wa wakuu wa nchi za Afrika uliomalizika hivi karibuni jijini Addis Ababa, Ethiopia.

Akizungumza kwenye sherehe za utiaji saini makubaliano hayo, Rais wa Benki ya Afrika, Dk. Akinwumi Adesima, alisema mchakato huo utatoa mchango mkubwa katika Bara la Afrika kufikia malengo ya pamoja ya kidunia kuhusu nishati na kubadilisha mifumo yake bila gharama  kubwa kulinganisha matumizi ya nishati mbadala na rasilimali nyingine.

“Hatua hii imetokana na majadiliano yaliyoanzishwa na viongozi wa Afrika wakati wa mkutano wa 6 wa kimataifa wa Tokyo kuhusu maendeleo ya Afrika, TICAD-VI uliofanyika jijini Nairobi mwaka 2016 na pia ziara ya uongozi wa Benki ya Afrika, nchini Japan, Serikali ilithibitisha utayari wake wa kusaidia mkakati wa maendeleo ya nishati kati ya Japan na Afrika,” alisema.

Alisema Japan iko tayari kutoa dola za Marekani bilioni 6 kufadhili miradi ya operesheni ambayo itapeleka umeme majumbani, shuleni, mahospitalini, kwenye kilimo, viwanda na nishati mbadala za kupikia.

Akizungumza kwa niaba ya Naibu Waziri Mkuu wa Japan ambaye pia ni waziri wa fedha, Taro Aso, Balozi wa Japan nchini Ethiopia, Shinichi Saida, alisema ana imani kupitia mchakato huu, nchi yake itachangia pakubwa kufikia malengo na kupeleka umeme kwenye maeneo mengi ya Afrika.

Alisema Benki ya Afrika na Serikali ya Japan zitafanya kazi kwa karibu katika kutekeleza makubaliano yenyewe ndani ya majuma machache yajayo na kabla ya mwisho wa mwaka 2017.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here