JPM : TUMBILI NI WAO SI KAFULILA

1
770

Na Waandishi Wetu


RAIS Dk. John Magufuli, amewakosoa baadhi ya watendaji wa Serikali waliombeza aliyekuwa Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila, wakati wa sakata la kashfa ya Escrow.

Rais Magufuli alisema Kafulila ameonesha uzalendo mkubwa ambao hauwezi kusahaulika katika historia ya Tanzania na kumpongeza kwa hatua yake ya kujitoa muhanga kutetea rasilimali za Watanzania.

Akizungumza na wananchi wa Kata ya  Nguruka jana katika uzinduzi wa mradi mkubwa wa maji uliopo Tarafa ya Nguruka katika Wilaya ya Uvinza alisema atakuwa mnafiki akishindwa kumpongeza Kafulila kwa kazi kubwa aliyoifanya ya kuibua ubadhirifu uliofanywa na Kampuni ya Kufua Umeme ya IPTL.

Alisema Kafulila alitukanwa sana alipo ibua sakata la Escrow na kuitwa majina mengi ya kudhalilishwa kama tumbili na mengine mengi ya ajabu kwa sababu ya uzalendo wake wa kutetea Taifa.

“Mimi ninafahamu unapoibua kitu cha kizalendo lazima usemwe, hivyo ninampongeza Kafulila kwa uzalendo wake kwa nchi na nitaendelea kumpongeza maisha yangu yote” alisema.

Rais Magufuli alisema maendeleo hayana chama ndio maana Kafulila alijitoa kwa hali ya juu na kutetea fedha za umma zilizo kuwa zikiibwa na mafisadi wachache na kujinufaisha wao wenyewe.

“Ninajua Kafulila ulitukanwa sana wakati wa kuibua sakata la Escrow, wapo watu walikuita tumbili mimi najua  wewe sio tumbili, wao ndiyo matumbili.

“Kafulila wewe hongera alisimamia wizi tuliokuwa tunafanyiziwa IPTL. Ni wizi wa ajabu na wengine wakamtisha kumpeleka mahakamani, wakamtukana weee! Na wengine wakamwita tumbili, sasa tumbili amefanya kazi kubwa kwa ajili ya Watanzania.

“Tunahitaji wazalendo katika nchi hii, nchi hii ilikosa uzalendo ikawa na watu watafutaji, ukimchagua kiongozi anatafuta pesa yake badala ya kwenda kuongoza kwa ajili ya watu ambao ni masikini.

“Tulikosa uzalendo wa utanzania, tukashindwa kumwogopa Mungu kwamba mali ni za muda tu baadae tutaziacha na kwenda kwenye shimo moja tu (kaburini) tutakapozikwa kule kaburini. Ninawaomba Watanzania tujenge uzalendo.

“Kafulila wewe najua ni wa chama kingine, lakini umefanya kazi kubwa ya kulinda maslahi ya nchi, kwa hiyo nitakuwa mnafiki sana nisipo kupongeza. Kitu ulichokifanya kwa taifa ni kikubwa naomba nikupongeze kwa hilo,” alisema.

Alisema kiongozi mzuri ni yule ambae anatetea wananchi bila kujali chama wala siasa za uchochezi, hivyo atahakikisha kuwa wananchi hawateseki na wale ambao wameiba fedha za Serikali wanazirudisha bila kujali nyadhifa walizonazo ili pesa hizo zitumike katika kuleta maendeleo.

Rais Magufuli aliwaahidi wananchi wa Nguruka kuwa atahakikisha anatatua kero ya maji na umeme katika kata yao, wakati katika suala la umeme atamtuma Waziri wa Nishati na Madini ili aweze kutatua tatizo hilo na kuwasaidia.

Rais Magufuli amemaliza ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mkoani Kigoma kwa kuweka jiwe la msingi katika mradi mkubwa wa maji katika Kata ya Nguruka uliogharimu zaidi ya Sh bilioni 2, ambao unatarajiwa kukamilika Desemba 30 mwaka huu.

Kafulila

Akizungumza na MTANZANIA jana, Kafulila ambaye alikuwa Mbunge wa Jimbo la Kigoma Kusini kupitia (NCCR- Mageuzi), alimshukuru Rais Magufuli kwa kutambua kazi aliyokuwa akiifanya na sasa imeanza kuleta matokeo mazuri.

“Kwa kweli nafarijika na inanipa moyo wa kizalendo zaidi ninapoona Rais anaunga mkono sakata la Escrow ambalo mimi ndo nililiibua wakati nikiwa mbunge japo nilipitia kwenye kipindi kigumu.

“Nimefarijika sana mkuu wa nchi kuguswa na kutambua mchango wangu  katika vita hatari ya ufisadi wa IPTL / ESCROW, natambua kwenye vita hii hakuna chama.

“Niliteseka sana ndani na nje ya jimbo kutokana na vita hii, zilifanyika kila hila na njama lakini Namshukuru Mungu kuwa upande wangu hata nimebaki hai,’’alieleza Kafulila.

Aliendelea kueleza.  “Ukweli nimefarijika sana kuona mkuu wa nchi amelizungumzia jambo hili jimboni kwa wananchi walionipenda sana amezungumzia kwa hisia na uzito wa kutosha binafsi kwenye vita ya ufisadi nchini ninamuunga mkono Rais ,”alieleza Kafulila.

Kafulila alimshauri Rais ajenge mfumo wa taasisi imara za uchunguzi na uendeshaji wa mashtaka katika eneo hilo ili kuhakikisha vita hiyo inakuwa ya mafanikio makubwa.

Msuguano

 

Kafulila alipoibua sakata hilo alipata upinzani mkubwa  ndani na nje ya Bunge, ambapo kulikuwa na mvutano mkali kati yake na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, wanasiasa na watendaji wengine wa Serikali waliohusishwa na sakata hilo.

 

Wakati Bunge likiwa linaendelea mwaka 2014 katika hali isiyokuwa ya kawaida  kuliibuka na mvutano mkali baada ya Kafulila kuomba mwongozo juu ya ESCROW na wizi uliofanyika.

Werema wakati huo akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali alipotakiwa kutoa maelezo, kwanza alianza kushambulia vielelezo vya Kafulila kuwa ni vipeperushi visivyokuwa na maana hali hiyo ilipelekea Mbunge wa Ubungo wakati huo, John Mnyika (Chadema) kudai kuhusu utaratibu lakini mwenyekiti  wakati huo Mussa Zungu alipotezea.

AG aliendelea  kumtaka Kafulila wakutane nje kama anamambo mengine ila bungeni kunautaratibu wake (walikuwa wakimwingilia wakati anazungumza wakionesha kutokubaliana naye).

Majibishano yalipozidi Werema alipandwa na hasira alisema. “Kafulila wewe ni sawa na tumbili asiyeweza kuamua mambo ya msituni,” alisema na baadae Kafulila aliposimama naye alimwita Werema mwizi.

 

Kutokana na mvutano huo Werema alionesha dalili za kutaka kumfuata Kafulila akampige, lakini baadhi ya mawaziri walimzuia na kumsihi atulize hasira.
Baada ya Bunge kuahirishwa wakiwa nje Jaji Werema alilalamika hadharani kuhusu Kafulila kumwita mwizi ndani ya Bunge na ndipo jaji huyo alipotaka kumvamia tena Kafulila.

“Mimi nakwambia Kafulila nitakukata kichwa, we subiri tu labda ukiniomba msamaha” alisema Werema kwa sauti ya hasira.

Kutokana na maneno hayo Kafulila naye alijibu. “Huwezi kunikata kichwa, huwezi, yaani uniue, hapana huwezi tena nakwambia huwezi,” alisema Kafulila.

Ampongeza Sakaya

Wakati huo huo akiwa mkoani Tabora, Rais Dk. Magufuli amempongeza Mbunge wa Jimbo la Kaliua, Magdalena Sakaya (CUF), kwa kazi nzuri anayoifanya katika kuwaletea wananchi maendeleo licha ya kuwa anatoka chama cha upinzani.

Dk. Magufuli alitoa kauli hiyo jana wilayani Kaliua mkoani Tabora alipokua akizindua barabara ya Kaliua-Kazilabwa yenye urefu wa kilomita 56 iliyojengwa kwa kiwango cha lami na Kampuni ya Chico ya China.

Dk. Magufuli alisema kuwa ni heri kuwa na mbunge wa upinzani anayetekeleza mambo ya Chama Cha Mapinduzi  kuliko kuwa na mbunge wa CCM anayetekeleza ya upinzani kwani huo ni usaliti mkubwa kwa chama.

“Nasema haya kwa sababu nafahamu hata wakati wa kampeni niliyashudia haya, ndiyo maana nasema ni bora kuwa na mbunge wa CUF, Chadema anayetekeleza mambo ya CCM kuliko wa CCM anayetekeleza mambo ya vyama vingine.

“Najua mwili wake wote na akili yake yote ni CUF lakini damu yake ni CCM” alisema Dk. Magufuli.

Akizunguzia ujenzi wa barabara hiyo Dk. Magufuli alisema imejengwa kwa fedha za Serikali bila mfadhili kuchangia, ambapo aliwataka wananchi kutozidisha uzito wa mizigo na kuchimba mchangan kado ya barabara ili idumu kwa muda mrefu.

Aliutaka Wakala wa Barabara (Tanroads) kubomoa nyumba zote zitakazojengwa katika hifadhi ya barabara bila kutoa taarifa.

“Kuna zoezi litaanza hivi karibuni la kubomoa nyumba ziliopo kando ya reli, hakikisheni zote zinaondoka, tunaaza kujenga reli ya kisasa lazima nyumba zote ziondoke kupisha ujenzi, najua wapo viongozi wengine wa CCM wanapitishapitisha maneno wa kubomoa anzeni na za hao wa CCM” alisema Dk, Magufuli.

Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa kilomita 56 umegharimu zaidi ya sh bilioni 61.9 ambazo ni pamoja na gharama za ujenzi, usimamizi na fidia kwa wananchi waliopisha utekelezaji wa mradi huo.

Wakati huo huo Dk. Magufuli amemwagiza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa, kutangaza zabuni ya ujenzi wa barabara ya Kaliua hadi Urambo yenye urefu wa kilomita 28 kwa kiwango cha lami ndani ya mwezi mmoja kutoka sasa.

“Tafuteni mkandarasi kama hamjampata ndani ya mwezi mmoja apatikane msaini mkataba, pesa zipo hata mkitaka kesho njooni mchukue” alisema.

Akizungumzia kero zinazowakabili wakulima wa tumbaku Dk. Magufuli alisema suala hilo amemwachia Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alishughulikie na kisha kumpelekea taarifa.

Alizitaka mamlaka husika kutotumia nguvu kubwa kuwaondoa waliovamia misitu badala yake wawaeleweshwe ili watafahamu madhara ya uharibifu wa mazingira.

Kuhusu suala la mimba shuleni, Rais Magufuli aliwataka wanaume wanaowapatia wanafunzi ujauzito kujiandaa kwenda jela miaka 30 ili wakatumie nguvu zao kuzalisha wakiwa gerezani.

Habari hii imeandaliwa na Editha Karlo, Kigoma, Leonard Mang’oha na Asha Bani, Dar

Mwisho

1 COMMENT

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here