24.2 C
Dar es Salaam
Friday, April 26, 2024

Contact us: [email protected]

ACT WAZALENDO WAMWANGUKIA JPM

Na TUNU NASSOR,-DAR ES SALAAM


CHAMA cha ACT Wazalendo kimemwomba Rais Dk. John Magufuli kuendeleza mchakato wa kuwapatia Watanzania Katiba mpya itakayowasaidia kuwatumbua viongozi wasiokuwa na sifa.

Akizungumza na waandishi wa habari jana, Naibu Katibu Mkuu (Bara), Msafiri Mtamelwa alisema kitendo cha Rais Dk. Magufuli, kudai kuwa suala la Katiba mpya haikuwa ajenda yake ni kuwanyima haki wananchi kuwa na mamlaka juu ya viongozi wasiofaa.

“Tunamwomba Rais Magufuli arudi kuanza na Katiba ya jaji warioba ambayo ilionyesha kutoa mamlaka makubwa kwa wananchi.

“Urais ni taasisi ambayo hata akiingia mtu mwingine anatakiwa kuendeleza kazi alipoishia aliyetoka hivyo kusema si ajenda yake hili si sawa,” alisema Mtamelwa.  

Mtemelwa pia aliwaomba wanachama wake wenye sifa kujitokeza kuomba kuteuliwa kuwa wagombea wa nafasi ya ubunge wa Bunge la Afrika mashariki katika uchaguzi utakaofanyika Aprili 4, mwaka huu.

Alisema chama hicho kina watu wengi wenye sifa za kushika nafasi hiyo, hivyo wajitokeze kujaza fomu kabla ya siku ya mwisho kuchukua fomu ambayo ni kesho jioni.

“Tunaamini kuwa ACT Wazalendo kitatoa wabunge hodari watakaokwenda kuiwakilisha nchi ndani ya Jumuiya hiyo kwa kujenga hoja makini,” alisema Mtamelwa.

Pamoja na hali hiyo aliwakumbusha wakazi wa Arusha kuhudhuria Mkutano Mkuu wa kidemokrasia utakaofanyika Machi 25, mwaka huu jijini humo.

 “Maandalizi ya mkutano huu yamekamilika kwa asilimia 90 hivyo tunatoa wito kwa wakazi wa Arusha kuhudhuria mkutano huu ambao utajadili masuala mbalimbali kwa mustakabali wa Taifa letu,” alisema Mtamelwa.

Katika hatua nyingine Mtamelwa amempongeza Rais mpya wa Chama cha Wanasheria Tanganyika(TLS), Tundu Lissu kwa kuchaguliwa kwa ushindi wa kishindo kushika wadhifa huo.

“Si kazi rahisi mtu kutoka upinzani kuweza kushinda nafasi hiyo muhimu huku akiwa amepitia misukosuko mingi hivyo tunamwomba awe mwangalifu kwa kuwahakikishia Watanzania hata walio katika upinzani wanaweza kuongoza,” alisema Mtemelwa.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
586,000SubscribersSubscribe

Latest Articles