30.6 C
Dar es Salaam
Saturday, November 23, 2024

Contact us: [email protected]

Kwaheri Mzee Mkapa, tutakukumbuka daima

SAFARI ya maisha ya Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa hapa duniani ilihitimishwa rasmi jana alasiri  baada ya kuzikwa  katika kijiji alichozaliwa, Lupaso, Wilaya ya Masasi mkoani Mtwara.

Safari hii ya majonzi ya mwisho ya Rais Mkapa ambayo jana iliongozwa na Rais John Magufuli, imeacha  simanzi na masikitiko makubwa kwa maelfu ya Watanzania kutokana na mchango wake wa hali na mali kwenye ujenzi wa taifa letu. Hakika tutamkumbuka daima mzee Mkapa.

Rais Mkapa ambaye aliongoza Tanzania kwa miaka 10 kuanzia 1995 hadi 2005, alipatwa na mauti usiku wa Julai 23, akiwa hospitalini jijini Dar es Salaam alikokuwa akitibiwa ugonjwa wa malaria.

 Hata hivyo, baada ya uchunguzi wa madaktari wake, iligundulika kuwa kifo chake kilisababishwa na mshtuko wa moyo ambao kwa kitaalamu unaitwa cardiac arrest.

Tangu tukio la kufariki dunia kwa Mkapa kutokea, watu mbalimbali kutoka ndani na nje ya nchi wamekuwa wakitoa salamu za pole kwa Rais Magufuli na familia ya marehemu Mkapa kama ishara ya upendo na kuenzi mchango wake kwa taifa na mataifa mengine duniani.

Wote tuna huzuni isiyo na kifani kwa kuondokewa na kiongozi huyo mwenye maono na mzalendo aliyeipenda nchi yake kwa dhati kabisa. Ndio maana hata Rais Jakaya Kikwete alisema jana mafanikio ya kiuchumi ya nchi hii yanatokana na juhudi za mzee Mkapa.

Ndiyo maana kama taifa tunapaswa kuendelea kuenzi yale mema yote ambayo Rais wetu Mkapa ametuachia au kutujengea msingi imara wa uendeshaji wa nchi yetu.

 Hakuna ubishi kwamba Rais Mkapa katika utawala wake alitumia uwezo wake wote kujenga mifumo imara ya uchumi na ile ya kuendesha Serikali ambayo imekuwa msaada mkubwa kwa viongozi waliomfuata baada ya yeye kustaafu urais.

 Hivyo basi kama taifa, Rais Mkapa kwetu ataendelea kuishi miaka nenda rudi kutokana na kazi nzuri aliyoifanya kwa taifa lake na hivyo  kuwa katika orodha ya viongozi watakaokumbukwa na vizazi vya sasa na vijavyo.

Ni rai yetu kwamba kama nchi tunapaswa kuweka yale yote aliyofanya Rais Mkapa katika uongozi wake kwenye kumbukumbu rasmi na kwenye mipango ya nchi, ili kizazi kijacho kitambue kuwa nchi hii imewahi kupata kiongozi bora kabisa aliyefuata kwa karibu nyayo za Baba wa Taifa hili, Mwalimu Julius  Nyerere.

Ndiyo maana tunawasihii Watanzania wote kwa imani zao, waendelee kumuombea  Rais Mkapa kwa Maulana amweke mahala pema peponi.

Kwa mumba wetu, sisi kama binadamu hatuna ukamilifu, hivyo rehema zake ni muhimu kwa maisha ya sasa na baada ya kifo. Kwaheri mzalendo na mpenda nchi yako,  tutakukumbuka daima. Mungu ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
591,000SubscribersSubscribe

Latest Articles