31.7 C
Dar es Salaam
Thursday, March 28, 2024

Contact us: [email protected]

Homa ya ini tishio kwa wenye VVU

Na AVELINE KITOMARY  -DAR ES SALAAM

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu amesema homa ya ini aina ya B (Hepatitist B), ndiyo inayoongoza kwa maambukizi nchini kwa asilimia 4.0.

Amesema homa hiyo na ile ya Hepatitis C imekuwa tatizo kubwa kwa watu wenye maambukizi ya virusi vya ugonjwa wa Ukimwi.

Katika taarifa yake aliyoitoa juzi wakati wa siku ya maadhimisho ya homa ya ini duniani, Ummy alisema wizara imeandaa mwongozo wa uchanjaji wa chanjo ya homa ya ini aina ya B ambao utatumika kwa watu wazima walioko hatarini zaidi kuambukizwa.

“Chanjo hii imetolewa hospitali zetu za rufaa za ngazi ya taifa, hospitaali 27 za mikoa na baadhi ya hospitali za halmashauri, inatolewa kwenye vituo vilivyoko mipakani na huduma hii inatolewa kwa bei elekezi ya Sh 10,000 kwa kipimo na dozi ni Sh 10,000.

 “Wizara imekuwa ikiratibu utoaji wa chanjo ya homa ya ini ya hepatitis B  bila malipo kwa watoto wachanga  kuanzia mwaka 2002 kwenye  mchanganyiko wa “Pentavalenti”, chanjo hii imekuwa ikitolewa mara tatu ambayo ni wiki sita baada ya kuzaliwa, wiki ya  10 na wiki ya 14,” alisema Ummy.

Alisema zaidi ya Watanzania milioni 20 walioko chini ya umri wa miaka 17, wamepatiwa chanjo ya homa ya ini, hivyo mikakati yao ni kuendelea kupunguza kasi ya ugonjwa huo nchini.

 “Takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO) zinaonesha mwaka 2015 kulikuwa na vifo milioni 1.34 kutokana na homa ya ini aina zote; A, B, C, D na E ambapo vifo vilivyotokana na B pekee vilikadiriwa kuwa 887,000.

“Watu milioni 257 duniani sawa na asilimi 3.5 walikuwa wanaishi na virusi vya homa ya ini aina ya B  huku kiwango cha maambukizi kikiwa kikubwa zaidi katika nchi za Afrika kwa asilimia 6.1 na Pasifiki ya Magharibi asilimia 6.2.

“Takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zinaonesha kuwa hali ya maambukizi ya homa ya ini aina ya B na C kwa mwaka 2018/2019 ni asilimia 5.9 kwa hepatitis B na 1.9 kwa hepatitis C,” alieleza Ummy.

Alisema Serikali imekuwa na mpango mkakati wa miaka mitano (2018/2019 – 2022/2023) wa kujikinga na kukabiliana na homa ya ini ili kupunguza maambukizi na vifo ifikapo mwaka 2030.

“Mikakati hiyo imejikita zaidi katika huduma za utoaji chanjo kwa watoto na kwa makundi ya watu waliopo katika hatari zaidi, kuongeza utambuzi, upimaji na matibabu, kuendeleza uzuiaji wa maambukizi yanayoweza kutokea kwa njia mbalimbali, kutoa elimu ya afya kuhusu matumizi salama ya sindano na uimarishaji wa utoaji huduma dhidi ya ugonjwa wa homa ya ini,” alisema Ummy.

Alibainisha kuwa homa ya ini inasababishwa na virusi ambavyo vikiingia mwilini mwa binadamu hushambulia ini na hatimaye kulifanya lisinyae na kushindwa kufanya kazi vizuri.

“Mtu mwenye ugonjwa huo anaweza kutoonesha dalili kwa muda mrefu huku asilimia kubwa wakishindwa kupata matibabu mapema kwa kugundulika katika hatua ya mwisho ambayo ni kusinyaa kwa ini na saratani ya ini.

“Matibabu hufanyika kulingana na aina ya maambukizi, tiba hutolewa kulingana na dalili zinazoambatana na ugonjwa huo na kwa B  matibabu hutegemea hatua ya mgonjwa aliyofikia,  wakati mwingine mgonjwa hulazimika kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kwa kipindi chote cha uhai wake,” alisema Ummy.

Katika maadhimisho ya mwaka huu, kaulimbiu ni “Kizazi kijacho kisicho na maambukizi ya homa ya ini”.

Mwisho

Watakiwa kutowekeza nguvu kucheza watoto ngoma

Na Ashura Kazinja

 -Morogoro

WATENDAJI wa kata mbalimbali nchini wameshauriwa kuwahimiza wazazi kuacha kuwekeza nguvu zaidi katika kufanya sherehe za ngoma za watoto wao na badala yake wafanye shughuli za maendeleo pamoja na elimu.

Hayo yalibainishwa jana na Mtendaji wa Kata ya Ulaya, Wilaya ya Kilosa mkoani Morogoro, Juma Kizima, wakati akizungumza na wananchi baada ya kupata elimu ya ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali za umma (PETS) kutoka taasisi isiyo ya kiserikali inayojihusisha na masuala ya kutoa elimu kwa jamii ya Dira Oranization, iliyofadhiliwa na asasi isiyokuwa ya kiserikali ijulikanayo kama The Foundation For Civil Society (FCS).

Kizima alisema matukio ya ngoma ambayo hufanywa kwa siku tatu mfululizo yanaanza kushika kasi kwa wakazi wa maeneo hayo na mengine katika kipindi hiki cha baada ya mavuno ambapo wazazi wamekuwa wakiwekeza kwa muda mrefu kusherehekea na kusahau masuala ya michango ya shule.

Alisema kuwa ushiriki halali wa vikao vya kijiji au shule utasaidia wananchi kujua mengi ikiwemo maendeleo ya shule na kijiji kwa ujumla.

 “Mzazi kuandaa ngoma ambayo itachukua siku nyingi na sherehe zaidi italeta shida kwa mtoto baadae kutokana na mzazi kukosa suala la uwajibikaji.

“Wazazi wasiofuatilia maendeleo ya watoto wao wapo maeneo mengi hata hapa Ulaya, mwanafunzi anatoroka shule mzazi haulizi, ajaenda shule mzazi haulizi, kesho akipata mimba ndio anaanza kuuliza kapataje, tubadilike wazazi,” alisema Kizima.

Vilevile alieleza kuwa wazazi wanapaswa kutambua wajibu wao kwa jamii hasa kwa watoto ili kuwawezesha kufikia malengo yao ya kimaisha.

Naye Mkurugenzi mtendaji wa Dira, Erasmo Tullo, aliwataka viongozi wa kata kutumia dhana ya uwazi, uwajibikaji na ushirikishwaji itakayowaweka wananchi jirani na hivyo kuwaondoa hofu hasa kwenye miradi ya maeneo yao na kujenga imani ya pamoja.

Pia Tullo aliwataka wananchi kutambua kuwa wanapaswa kujua kuwa wana deni kubwa kwa kutoshiriki vikao vya maendeleo au vikao vya shule ambapo wanakosa fursa za ufuatiliaji wa matumizi ya rasilimali zao (PETS) kwani ni haki yao jambo litakalosaidia kuleta tija.

Hata hivyo, aliwataka viongozi kutambua kuwa hata kama wakiwa kama malaika wakiwaongoza watu ambao hawaelewi kinachoendelea hawatafika popote.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
214,997FollowersFollow
585,000SubscribersSubscribe

Latest Articles