25.3 C
Dar es Salaam
Monday, July 4, 2022

Wasichana 300 waliokatishwa masomo wapata fursa nyingine

Na CLARA MATIMO – MWANZA

WASICHANA 300 wanaoishi Wilaya ya Ilemela mkoani Mwanza, ambao walikatisha masomo kutokana na changamoto mbalimbali, wanatarajia kupatiwa mafunzo yatakayowawezesha kufikia malengo yao.

Mafunzo hayo yatatolewa na Shirika lisilo la Serikali la Mikono Yetu linalojishughulisha kuwawezesha wanawake na wasichana kumiliki rasilimali zalishi  ili waweze kujikwamua kiuchumi, ikiwemo ardhi na mifugo kupitia mradi wa Msichana ni Tai kwa ufadhili wa Shirika la Kimataifa la Novo Foundation la nchini Marekani.

Akizungumza jijini hapa  hivi karibuni  katika hafla ya uzinduzi wa mradi huo  kwa viongozi wa Kata ya Buswelu iliyopo wilayani humo,  Meneja Programu wa Shirika la Mikono Yetu, Sophia Nshushi, alisema lengo la mradi huo ni kuwawezesha wasichana ambao hawakuhitimu masomo yao kutimiza ndoto zao kwa kuwapatia mafunzo yatakayowawezesha kujikwamua kiuchumi.

“Mikono Yetu tunaamini hata wasichana walio nje ya shule wana ndoto ambazo walishindwa kuzitimiza wakati wanasoma, wapo ambao walipata ujauzito na wengine maradhi mbalimbali, hivyo wakashindwa kuendelea na masomo, kupitia mradi wa Msichana ni Tai  watainuka tena na kuendelea na harakati za kutimiza ndoto zao.

 “Hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius  Nyerere aliamini katika nguvu ya mwanamke akasema  “mwanamke ni tai sio kuku, anaweza kutumia mbawa zake akaruka na akafikia malengo yake”, ndiyo maana Mikono Yetu tukaona tulete mradi huu ili tuwape nafasi wasichana walioshindwa kutimiza ndoto zao,” alisema Sophia.

Ofisa mradi huo, Halima Juma, alisema wanufaika ni wasichana kuanzia miaka tisa hadi 17,  watafundishwa mbinu mbalimbali za ujasiriamali, afya ya uzazi, haki na wajibu wa msichana pamoja na jinsi ya kujiamini ili waweze kufikia ndoto zao, hivyo kuepuka kuwa tegemezi pamoja na vitendo vya ukatili.

“Mradi huu ni wa miaka mitatu, tutaanza kuutekeleza Agosti mwaka huu hadi mwaka 2023  katika Kata ya Buswelu iliyopo Wilaya ya Ilemela,  tutawafikia wasichana 300 pamoja na wazazi ama walezi wao 300, hivyo  tutakuwa na jumla ya wanufaika 600, tumeamua kushirikiana na wazazi ama walezi ili tupate matokeo chanya,” alisema Halima.

Ofisa Mtendaji wa Kata ya Buswelu, Nhikilo Joseph, aliwataka wazazi na walezi wa wasichana ambao watanufaika na mradi huo kushirikiana na Shirika la Mikono Yetu bega kwa bega  katika kuutekeleza mradi huo kwa sababu  unafufua matumaini kwa wasichana.

- Advertisement -

Related Articles

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

Stay Connected

90,904FansLike
195,649FollowersFollow
545,000SubscribersSubscribe

Latest Articles